Home » » 'CCM kisaidie wabunge kuwang’oa mawaziri'

'CCM kisaidie wabunge kuwang’oa mawaziri'

Written By JAK on Wednesday, November 27, 2013 | 6:08 AM



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi amekiomba chama hicho kuwasaidia wabunge wake na wananchi ili kuwang'oa mawaziri na watendaji wa halmashauri wazembe wasiotimiza majukumu na wajibu wao.

Pia ameomba washauri wa Rais Jakaya Kikwete wamshauri vyema kuhusu utendaji usioridhisha wa baadhi ya halmashauri nchini.

Kauli hiyo aliitoa mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana aliyekuwa amewasili wilayani Kyela kuanza ziara ya siku 11 kutembelea wilaya zote na kuangalia uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM mkoani Mbeya.

Akizungumza mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mbeya waliokusanyika wilayani Kyela kumpokea Katibu Mkuu Kinana aliyewasili kwa meli ya MV Songea kutoka Nyasa, Zambi alisema wako baadhi ya viongozi wasiotimiza wajibu wao na hao wanatoa taswira mbaya ya Serikali mbele ya wananchi.

Kutokana na tabia za baadhi ya watendaji serikalini na kwenye halmashauri mbalimbali nchini, Zambi alisema jambo hilo haliwezi kufumbiwa macho kwani wamekuwa wanaipa sifa mbaya Serikali kutokana na kuonekana haifanyi vizuri.

Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Mbozi Mashariki, alisema wabunge wa CCM wamekuwa wakipiga kelele bungeni wakiomba baadhi ya watumishi wa umma wakiwamo Mawaziri wasiowajibikana wachukuliwe hatua kwa kuwajibishwa, jambo ambalo limekuwa halifanyiki.

"Wako watendaji wa Serikali wasiowajibishwa na kusababisha madeni na hasara, licha ya wabunge kushauri wachukuliwe hatua lakini hakuna kinachofanyika, tunakiomba chama kilitazame jambo hili na kutuunga mkono," alisema Zambi.

Aidha, aliiomba Serikali kutazama kwa karibu utendaji wa baadhi ya watendaji wa halmashauri na halmashauri zenyewe, kwani zimekuwa zikifanya vibaya huku wahusika wakiendelea kupigiwa makofi.
Kutokana na vitendo hivyo, Zambi alisema baadhi ya watendaji wamesababisha wananchi kukosa imani na Serikali na kuitazama vibaya licha ya nia yake njema kwa kutaka kuleta maendeleo ya taifa kutoa huduma kwa kijamii.

Akijibu hoja iliyotolewa na Zambi, Kinana alisema jukumu la kuisimamia Serikali ni la chama na amewataka viongozi wa CCM kuhakikisha wanasimamia vyema jukumu hilo.

Kinana alisema, chama ndicho kilichopita kwa wananchi kuomba kura kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa chama kuisimamia Serikali kuhakikisha inatekeleza wajibu wake. Katika hatua nyingine, Kinana alisema hakuna kamati yoyote ya siasa yenye uwezo wa kumuondoa Katibu wa CCM wa Wilaya au wa Mkoa.

Alisema makatibu wa CCM wanateuliwa na Kamati Kuu ya CCM hivyo, hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuwaondoa zaidi ya mamlaka iliyofanya uteuzi wao.

"Najua kwa nini mnataka kuwaondoa makatibu wa Wilaya, ni kutokana na mambo ya maslahi yenu, lakini hamuwezi kufanya bali mnatakiwa kuwajadili kwenye vikao halali na kuwasilisha mapendekezo yenu kwa Katibu Mkuu," alisema.

Alisema CCM itaendelea kusimamia utendaji kazi wa makatibu wake katika ngazi mbalimbali na kwamba watakaobainika kufanya madudu watachukuliwa hatua na viongozi waliowateua.

By Magnus Mahenge, Kyela
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger