Home » » Ni ‘divisheni O’ si ‘divisheni 5’

Ni ‘divisheni O’ si ‘divisheni 5’

Written By JAK on Sunday, November 10, 2013 | 6:44 AM

 http://www.24tanzania.com/wp-content/uploads/2012/09/Deputy-Minister-for-Education-and-Vocational-Training-Philipo-Mulugo.jpg
 Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini imetoa kauli rasmi ya Serikali kuhusu upangaji wa viwango vya alama na madaraja ya ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na cha sita na kusisitiza kwamba watahiniwa wanaoshindwa mitihani hiyo wanapata Daraja Sifuri na si Daraja la Tano.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri, Philipo Mulugo wakati akiwasilisha Kauli ya Mawaziri ndani ya Bunge baada ya Spika, Anne Makinda katika moja ya vikao vya Bunge lililomalizika jana, kuitaka Serikali kuleta taarifa sahihi za madaraja hayo.

Akitoa taarifa, Mulugo alisema Oktoba 30, mwaka huu Wizara ilitoa taarifa kwa umma kuhusu upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na ufaulu katika mitihani ya vidato vya sita na nne.

Serikali ilibainisha kuwa daraja sifuri lilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na daraja la tano, jambo ambalo liliamsha mjadala na hisia kwa wananchi, wadau na wabunge, wakisema jambo hilo linaleta mkanganyiko katika sekta ya elimu nchini.

Katika taarifa hiyo ya Wizara, iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa Sifuni Mchome, watahiniwa wa daraja la tano ni walioshindwa na katika makundi ya mpangilio daraja moja mpaka tano liliwekwa ili kuwa na utaratibu unaoeleweka.

“Ni kweli Katibu Mkuu wa Wizara alipotoa taarifa kwa umma alitaja makundi hayo na lililoshindwa alisema litaitwa daraja la tano, jambo ambalo jamii haijazoea zaidi ya daraja sifuri,” alisema Mulugo.

Aliongeza kuwa kuanzia sasa Serikali inatamka rasmi kuwa kundi la watahiniwa walioshindwa mitihani hiyo na awali kuandikwa daraja la tano, litaendelea kujulikana kama daraja sifuri.

Hata hivyo, awali taarifa zilizotolewa na Wizara zilisema kuanzia mwaka 2013 alama 60 za watahiniwa zitapatikana katika mtihani wa kidato cha nne na nyingine 40 kidato cha pili, mitihani miwili ya mihula ya kidato cha tatu na mtihani wa majaribio na mazoezi ya vitendo.

Wizara ilisema lengo la kufanya hivyo ni kuimarisha mfumo wa uwazi kwenye mitihani na utaanza kutekelezwa kwa wahitimu wa kidato cha nne wa mwaka huu na wa kidato cha sita mwakani.

By Ikunda Erick na Gloria Tesha, Dodoma
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger