Juma KasejaJuma Kaseja
By Mwandishi Wetu
KIPA Juma Kaseja amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga na kusema sasa kazi itafanyika baada ya maneno kwisha.
Tangu juzi kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii taarifa za Kaseja kusajili Simba zilisambaa, ambapo Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alithibitsiha jana kuwa ni kweli kipa huyo aliyechezea Simba msimu uliopita amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga.
Kwa mujibu wa Kizuguto, mkataba huo wa Kaseja una thamani ya Sh milioni 40, huku kukiwa na habari za ndani kwamba atalipwa mshahara wa karibu Sh milioni tano kwa mwezi.
Kizuguti alisema, Kaseja ataanza kuitumikia Yanga katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu unaotarajiwa kuanza Januari 25 mwakani, pamoja na michuano ya kimataifa.
Alipoulizwa kuhusu hilo jana, Kaseja alikiri kusaini mkataba Yanga na kuongeza kuwa yeye hakuwa mchezaji wa Simba bali alikuwa huru.
“Ni kweli kama umesikia nimesajili Yanga hiyo ni kweli kabisa, sasa itafanyika kazi, maneno yatakwisha, nashukuru kwamba Yanga wameona thamani yangu na kuamua kunisajili, nami nitawatumikia kwa moyo mmoja, alisema Kaseja.
“Lakini pia napenda niwaweke wazi mashabiki wa soka kwamba mimi sikuwa mchezaji wa Simba, Simba nilishamaliza mkataba wangu nikawa huru sikuwa mchezaji wa timu yoyote, sasa nimesajiliwa Yanga nikiwa huru sio kwamba nimetoka Simba,” alisema Kaseja.
Kwa mujibu wa Kizuguto, kusainishwa kwa Kaseja ilikuwa ni mapendekezo ya benchi la ufundi la klabu hiyo, walimhitaji kwa ajili ya kuitumikia kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kuwania Klabu Bingwa Afrika, ambapo klabu hiyo itaiwakilisha Tanzania pamoja na yale ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Benchi la ufundi la Yanga limependekeza Kaseja asajiliwe kwa sababu ni kipa mzoefu sio tu katika mashindano ya ndani, bali ya kimataifa,” alisema Kizuguto.
Kaseja sasa anakwenda kuungana na makipa wawili aliowahi kufanya nao kazi Simba SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
Hii inakuwa mara ya pili Kaseja kusajiliwa Yanga, baada ya awali kusajiliwa mwaka 2009 akitokea Simba SC ambako baada ya msimu mmoja wa mkataba wake kumalizika akaachwa na kurejea Msimbazi.
Kaseja alimaliza mkataba wake na Simba mwishoni mwa msimu uliopita, lakini uongozi wa klabu hiyo haukutaka kumuongezea mkataba ikidai kuwa kiwango chake kimeshuka.

Post a Comment