Home » » Balozi seif Ali Iddi akutana na ujumbe wa serikali ya uswisi

Balozi seif Ali Iddi akutana na ujumbe wa serikali ya uswisi

Written By JAK on Thursday, December 19, 2013 | 11:02 PM


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuweka kipaumbele katika kuendeleza mpango maalum wa kufanywa utafiti katika maeneo yote ya Kiuchumi, maendeleo na ustawi wa jamii. 

Kauli hiyo aliitoa wakati wa mazungomzo yake na Ujumbe wa Viongozi Wanane kutoka Serikali ya Uswisi  unaoongozwa na Waziri wa Sayansi, Utafiti na Elimu Bwana Mauro Dell Ambrogio aliokutana nao hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar. 

Balozi Seif alisema mpango huo utakwenda sambamba na ongezeko la mitaala pamoja na masomo ya utafiti kupitia skuli za Sekondari na vyuo vikuu ili Taifa lifikie daraja ya kujitosheleza kwa wataalamu wa fani hiyo kufikia daraja la Udaktari. 

Aliueleza Ujumbe huo wa Serikali ya Swisszerland ambao upo Zanzibar kuhudhuria Kongamano la Utafiti na Ubunifu Zanzibar la kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimebahatika kuwa na rasilmali nyingi baharini na Ardhini. Alifahamisha kwamba Rasilmali hizo hadi sasa bado hazijatumika vyema kutokana na ukosefu wa Taaluma ya kina ya utafiti ambazo baadaye zinaweza kusaidia ustawi wa kipato cha Wananchi walio wengi pamoja na Taifa kwa ujumla. 

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifafanua kwamba zipo baadhi ya tafiti zilizowahi kufanywa na baadhi ya wataalamu wa hapa nchini kwa kushirikiana pia na wale wa kigeni lakini mara nyingi tafiti hizo huishia kuwekwa maofisini bila ya kufanyia kazi zilizokusudiwa. Mapema Waziri wa Sayansi, Utafiti na Elimu wa Uswisi Bw. Mauro Dell Ambrogio ameipongeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na mipango yake ya kutilia mkazo suala la utafiti. Bwana Mauro alieleza kwamba utafiti popote pale ndio silaha na uti wa mgongo wa harakati za maendeleo katika taasisi zote ziwe za kiserikali, Mashirika ya Umma na hata sekta Binafsi. 

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Utafiti ya chuo Kikuu cha Basel Nchini Swisszerland Bwana Marcel Tanner aliyekuwa miongoni mwa ujumbe huo alisema Taasisi mbali mbali Duniani hivi sasa zimejikita zaidi katika kuona suala la Utafiti linapewa msukumo unaostahiki. 

Bwana Tanner alisema kuwa umuhimu wa tafiti hasa katika sekta za Afya na Kilimo ndio chachu inayosaidia kustawisha maendeleo na ustawi wa jamii popote pale Ulimwenguni. 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na akisalimiana na Waziri wa Sayansi, Utafiti na Elimu wa Uswisi  Bwana Mauro Dell Ambrogio na ujumbe wake walipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa mazungumzo.

 Balozi Seif akibadilishana mawazo na Waziri wa Sayansi,, Utafiti na Elimu wa Uswisi  Bwana Mauro Dell Ambrogio hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Serikali wa Uswisi ukiongozwa na Waziri wa Sayansi, Utafiti na Elimu Bwana Mauro Dell Ambrogio. Picha na Hassan Issa wa OMPR
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger