Na Mashaka Mhando,Korogwe
MBUNGE wa Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani almaarufu kama 'Profesa Majimarefu', amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kuacha kuwashabikia wanachama wanaotaka uongozi mwaka 2014/2015 badala yake washirikiane na viongozi waliopo ili watekeleze ahadi na ilani ya chama hicho.
Akizungumza kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya CCM kata ya Kizara wilayani hapa juzi, mbunge huyo alisema ipo tabia ambayo imeota mizizi miongoni mwa viongozi wa chama hicho kuwaunga mkono watu wanaotaka nafasi za Udiwani na Ubunge na kuwapiga vita viongozi waliopo katika nafasi hizo kwa sasa.
"Jamani viongozi wenzangu wa matawi na kata, tunapowaunga mkono watu wanaotaka uongozi mwaka 2015 hatukijengi chama chetu badala yake tunakipaka matope kwanini msisaidiane na madiwani na wabunge waliopo kutatua kero na kutekeleza ahadi na ilani yetu iliyotuweka madarakani," alisema mbunge huyo.
Alisema yeye amekuwa haumizi kichwa kwa watu wanaopita kwenye jimbo hilo na kumkashifu kwa maneno mabaya ikiwemo kumchonganisha kwa wapiga kura kwa hakusoma hatua ambayo aliwaeleza kwamba walipomchagua mwaka 2010 aliwapa sifa zake na wao wakampa kura nyingi, wakawaacha wasomi.
"Ubunge ni miaka mitano mkiniacha nitarudi kuagua na nyie mnajua mimi sijasoma lakini mlinichagua mkulima mwenzenu na hakika kazi naiweza na nitaendelea kutekeleza ahadi zangu nilizoahidi bado nina mwaka mmoja na nusu, nikirudi huku mwaka 2015 kama sijatekeleza ahadi zangu mtanisuta, lakini nawaomba nipeni ushirikiano," alisema.
Profesa Majimarefu katika harambee iliyofanyika kwenye kata hiyo, aliwasaidia wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kwa kulipa michango yote iliyokuwa ikitakiwa kuchangia ukarabati wa ofisi hiyo kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 1.9 kufaniklisha ukarabati huo.
Mbunge huyo kabla ya harambee hiyo alitoa kiasi cha sh. 300,000 kwa ajili ya kununulia mifuko 20 ya saruji lakini walipokuwa kwenye harambee hiyo alishitushwa na taarifa ya Katibu wa CCM kata hiyo Shabani Hiza kwamba ujenzi wa ofisi hiyo ulikwama tangu walipokuwa wabunge waliopita ambao walisema hawakuwa wamechangia.
"Ndugu zangu mimi nitajitolea fedha za ukarabati wa ofisi hii ili iendane na hadhi ya chama chetu, lakini wajumbve wenzangu fedha ambazo mlikuwa mmepanga kuchangia ofisi hii nendeni mkalipe ada kwenye makadi yenu ili mwakani muweze kuchagua viongozi wa chama chetu,"alisema.
Mbunge huyo aliaahidi kutekeleza ahadi ya kata hiyo ya kukosa mawasiliano ya simu jambo ambalo linasababisha wananchi hasa wakulima washine kuingia sokoni kutokana na kutokujua hali ya soko ilivyo ikiwemo viongozi wa serikali kukosa taarifa na maagizo ngazi za juu.
Kata hiyo ina idadi ya watu 14,660 ambapo watu wenye uwezo kumiliki simu ni 4,000 kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa kata Hamissi Mkinta.
Mbunge wa Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani 'almaarufu Profesa Majimarefu' (kwanza kulia) akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mngazija Kimbwaimbwai, Diwani wa Kata ya Kerenge Idd Shebila wakiwa kwenye mkutano wa Halmashauri ya CCM kata ya Kizara, Korogwe
Wajumbe wakimsikiliza Mbunge wao
Seehemu ya wajumbe kwenye mkutano huo. Picha na Mashaka Mhando
Post a Comment