Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ally Simba akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Patrick Makungu (hayupo pichani) katika ufunguzi wa kongamano la siku mbili kuhusu sheria ya mtandao jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Patrick Makungu akifafanua jambo wakati akifungua kongamano la siku mbili kuhusu sheria ya mtandao ambalo limeshirikisha wadau mbalimbali wa mtandao, kongamano hilo limefanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau wakimsikiliza kwa makini Mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Patrick Makungu (hayupo pichani) wakati akifungua kongamano la siku mbili kuhusu sheria ya mtandao jijini Dar es Salaam.
Mtoa mada wa kwanza katika kongamano la siku mbili kuhusu sheria ya mtandao Bw. Said Kalunde akitoa mada iliyohusu uhalifu wa mtandao
Picha zote na Eliphace Marwa – Maelezo
---------------------
Serikali yaendelea kushirikisha wadau mbalimbali wa mitandao ili kuweza kupata sheria itakayosimamia matumizi salama ya mitandao hapa nchini. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la siku mbili mapema hii leo jijini Dar es Salaam mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Patrick Makungu alisema kuwa serikali inashirikiana na wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi kwa lengo la kupata maoni yao.
“Kongamano hili linakutanisha wadau muhimu ambao maoni yao yataweza kufanikisha kupatikana kwa sheria ya mtandao ambayo itakuwa ndiyo suluhisho la uhalifu wa mtandao ambao unaonekana kushamiri sana hapa nchini na duniani kwa ujumla,” alisema Profesa Makungu.
Aidha Profesa Makungu aliongeza kuwa katika kupambana na uhalifu wa mtandao Tanzania imeandaa miswada mitatu ya sheria ya usalama wa mtandao ambayo pia inatumika katika Shirikisho la Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC).
“Sheria hizo ni sheria ya mtandao, sheria ya usalama wa taarifa na sheria ya biashara mtandao kwa kufanya hivi tuko sambamba na Jumuiya ya afrika Mashariki, Shirikisho la Maendeleo Kusini mwa Afrika na Umoja wa Afrika ambao wote wana lengo moja la kupambana na uhalifu wa mtandao,” aliongeza Profesa Makungu.
Naye Mkurugenzi wa TEHAMA toka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ally Simba alisema kuwa kama hakuna sheria ya mtandao ni rahisi uhalifu wa mtandao kupunguza wawekezaji kwani usalama wa fedha unakuwa ni mdogo.
Serikali inaendelea kukusanya maoni ya wadau mbalimbali kuhusu sheria ya mtandao kwani mchakato wa kupata sheria uko katika hatua za mwisho na ambapo mwakani katika miezi ya mwanzoni sheria hii itakuwa tayari.
Post a Comment