Home » » MHE CHIKAWE KATIKA MAHAFALI YA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA

MHE CHIKAWE KATIKA MAHAFALI YA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA

Written By JAK on Sunday, December 8, 2013 | 3:18 AM


Waziri wa Katiba Mheshimiwa Mathias Chikawe (Mb), jana tarehe 6/12/2013 amewatunuku Stashahada na Astashahada ya  Sheria jumla ya wahitimu 896 wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto katika Mahafali ya 13 ya Chuo hicho. Kati ya Wahitimu hao 267 ni wa Stashahada ya Sheria na wahitimu 629 ni wa Astashahada ya Sheria kwa Kampasi ya Lushoto na Mwanza.

Kabla ya kuwatunuku wahitimu hapo, mheshimiwa Chikawe kwa niaba ya Serikali aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Menejimenti ya Chuo kwa kukiendesha Chuo na aliwahakikishia kuwa Serikali inatambua mchango wanaoutoa katika kutoa elimu ya fani ya sheria na kwamba wahitimu wa Chuo wamechangia kwa kiasi kikubwa uboreshwaji wa utoaji wa haki hapa nchini.

Mhe Chikawe alisisitiza kuwa Serikali inaridhishwa na heshima ambayo Chuo imejijengea hapa nchini na kwamba nidhamu inayoonyeshwa na wanachuo kwa miaka yote ni kielelezo tosha cha namna gani wakufunzi na uongozi wa chuo unawajibika ipasavyo kuwaelimisha wanachuo. Na kwamba inaridhiswa na nidhamu ya wahitimu wa Chuo wanaoajiriwa katika sehemu mbalimbali. 

Mhe Chikawe aliwaambia wahitimu kuwa Sekta ya sheria ni sekta muhimu sana kwa maendeleo na mustakabali wa nchi yetu na kwamba Bila utii wa sheria na utawala bora Tanzania haiwezi kuendelea kisiasa,  kiuchumi na kijamii. Sekta hii inahitaji watumishi wenye maadili na kwamba bila kuwa na wanasheria na watumishi wenye maadili ya juu,  sekta hii itakuwa mwanzo wa migogoro badala ya kuwa mtatuzi wa migogoro. 

Mhe Chikawe alitumia fursa hiyo kukemea vitendo vyote vya ukosefu wa maadili wa watumishi katika sekta ya sheria na kuahidi kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa kwa kuwa vinawafanya wananchi wakose imani na vyombo vya kutoa haki na waichukie Serikali na hivyo kuongezeka kwa kutotii sheria na kujichukulia sheria mkononi. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua zinazostahili ili kuhakikisha sekta hii inabaki na watumishi wenye maadili. 

Mhe Chikawe alikipongeza Chuo kwa kupata Ithibati ya NACTE na aliwahimiza kukamilisha zoezi la uhuishaji wa Mitaala. Aliuhakikishia Uongozi wa Chuo kuwa atashirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili Chuo.

Pamoja na kutoa Shahada na Astashahada ya Sheria, Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kupitia kurugenzi yake ya Mafunzo endelevu ya Kimahakama hutoa na kuendesha mafunzo ya muda mfupi watumishi wote wa Mahakama na watumishi wa Sekta ya sheria kwa ujumla.
Mhe Mathias Chikawe, Waziri wa Katiba na Sheria akitoa hotuba yake wakati wa Mahafali ya 13 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama kabla ya kuwatunuku wahitimu 896 wa Chuo wa Stashahada na Astashahada ya Sheria.
Jaji Mstaafu John Mroso, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama akitoa maelezo ya maendeleo ya Chuo hicho kwa Mhe. Chikawe.
Jaji Ferdinand Wambali, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama akitoa maelezo kuhusu chuo na wahitimu ambao wametunukiwa Stashahada na Astashahada ya Sheria na Waziri wa Katiba na Sheria.
Baadhi ya wahitimu wa Stashahada ya Sheria wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakifuatilia mahafali ya 13 ya Chuo hicho jana tarehe 6/12/2013. 

KUTOKA MICHUZI
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger