Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Eneo Huru la Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru (aliyekaa
kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
Mhandisi Madeni Kipande (aliyekaa kulia) wakitia saini makubaliano ya
uendelezaji wa hekta 10 za eneo huru la bandari ya Mtwara mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni
Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia); Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara, Bw.Gregory Teu (kushoto) na mwanasheria wa TPA, Bi. Koku Kazaura (katikati).
=========== ========= ========
EPZA, TPA zafikia makubaliano kuendeleza eneo huru la Bandari Mtwara
Mamlaka
ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) na Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) zimefikia makubaliano ya uendelezaji wa hekta 10 za eneo
huru la bandari ya Mtwara.Makubaliano
haya ni awamu ya kwanza ya uendelezaji wa jumla ya hekta 110 za eneo
hilo huru la bandari ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya
uwekezaji mbalimbali.
Hekta
hizo 10 zitaendelezwa kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa na kisha
kugawiwa kwa makampuni ya kimataifa yanayofanya kazi za kutoa huduma
mbalimbali kwa makampuni yanayofanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi
katika mkoa wa Mtwara.
Kitakapomalizika,
kituo hiki cha huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti wa gesi na
mafuta mkoani Mtwara kitakuwa cha kipekee si kwa Tanzania pekee bali
katika ukanda mzima wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Utiaji saini makubaliano hayo ya kihistoria mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ulifanywa na Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm
Meru na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Madeni Kipande na
kushuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe na Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw.Gregory Teu.
Akiongea
wakati wa tukio hilo, Dkt. Mwakyembe alisema hatua hiyo inatoa fursa
kwa makampuni ya kimataifa yanayotoa huduma kwa kampuni za utafiti na
uzalishaji wa gesi na mafuta kuwekeza Mtwara na pia kutoa huduma zake
katika eneo hili la Afrika.
Waziri
huyo alisema tayari kampuni saba ziko tayari kuwekeza katika eneo hilo
na akazitaka mamlaka husika kuhakikisha zinafanya haraka na kwa usahihi
matayarisho yote yanayotakiwa ili kampuni hizo ziweze kuanza kufanya
kazi mara moja.“Mamlaka husika hazina budi kumaliza haraka na kwa usahihi matayarisho yanayotakiwa ili uwekezaji huu uanze mara moja,” alisema.
Alisema kabla ya hapo kampuni hizo zilikuwa zikitoa huduma zake kutokea Mombasa, Kenya na Afrika ya Kusini.Waziri Teu alisema hatua hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania.“Mtwara
na Tanzania sasa vinafunguka zaidi,” alisema, na kuongeza kuwa baada ya
kuanza kazi, kampuni hizo zitazalisha ajira kwa watanzania na kuongeza
wigo wa kodi kwa serikali.
Kwa
upande wake, Dkt. Meru alisema hatua hiyo ni muhimu sana kwa kuwa
kampuni hizo zitatoa huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti na
uzalishaji wa gesi na mafuta katika nchi za Kusini na Mashariki ya
Afrika.Alisema ujio wa kampuni hizo pia utasaidia katika kuendeleza sekta nyingine kama hoteli na kilimo katika mkoa wa Mtwara.
Baadhi ya kampuni zilizoonyesha nia ya dhati kuwekeza katika eneo hilo la hekta 10 ni pamoja na Schlumberger,
Weatherford and Halliburton International Inc toka Marekani; Lena, FFF
(T), Alpha group and Queensway toka Dubai na Uingereza; Altus Tanzania
Ltd toka Singapore; Tans Ocean Industries & Services Ltd toka Dubai
na Intershore Tanzania Ltd ya Afrika ya Kusini.
Post a Comment