Home »
Africa
» Giza nene latanda ndani ya Chadema
Giza nene latanda ndani ya Chadema
Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakiwa katika kikao chao kilichomalizika jana Dar es Salaam. Picha na Salhim Shao
Kwa ufupi
- Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema juzi usiku alipata kipigo kutoka kwa maofisa wa kikundi cha ulinzi cha chama hicho akituhumiwa kuvujisha siri za kikao, Dk Kitila ahojiwa, Zitto asema chama kinaendeshwa ovyo
Dar es Salaam. Giza nene limeendelea kutanda ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya juzi kulazimika kuongeza muda wa kikao cha Kamati Kuu kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake Zitto Kabwe.
Kikao hicho kiliendelea jana kikimhoji aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa Zitto Kabwe ameendelea na msimamo wake akituhumu chama hicho kuongozwa kwa ubabe.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kinachofanyika Hoteli ya Mbezi Garden jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa mkutano huo ulianza saa 4:00 asubuhi kwa kujadili ajenda zilizoshindwa kujadiliwa juzi, ambapo Dk Kitila alianza kuhojiwa saa 7:00 mchana.
Hata hivyo, taarifa hizo zinaeleza kuwa baada ya Dk Kitila kuingia kuhojiwa, aliwaomba wajumbe amwite mwanasheria wake, ambaye anazifahamu vyema taratibu na sheria za chama ili amsaidie kujibu hoja.
Kazi hiyo ya Dk Kitila kutafuta mwanasheria ilichukua muda mrefu na akapatikana saa 11;00 jioni ndipo kikao kilipoanza.
Hata hivyo, kabla ya kuingia katika ukumbi huo wa mkutano, Dk Kitila aliliambia gazeti hili kuwa atatoa ufafanuzi wa msimamo wake baada ya kutoka ndani ya kikao hicho.
Hata hivyo, hadi saa 1:00 jioni jana alikuwa bado ndani ya chumba cha mkutano akihojiwa, huku taarifa zaidi zikieleza kuwa wajumbe wengi walikuwa wakimsihi Dk Kitila aombe radhi ili asamehewe, yaishe.
Baada ya kumaliza kuhojiwa saa 1:40 usiku, Dk Kitila alimwambia mwandishi amemaliza kazi yake na anauachia uongozi kutoa uamuzi wake.
Awali akitoa taarifa ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika alisema kuwa Kamati Kuu ilishindwa kuwahoji Dk Kitila na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba baada ya kuondoka mapema eneo la mkutano bila ya kuaga na kuzima simu zao. Alisema kwa sababu Chadema ni chama kinachoamini katika demokrasia, waliamua kuwatafuta kwa namna nyingine na kufanikiwa kuwapata jana asubuhi.
Mnyika alisema kuwa kama mmoja wa watu hao hatafika kuhojiwa mbele ya Kamati Kuu, basi chama kitachukua uamuzi kitakachoona unafaa dhidi yake.
Mjumbe wa Kamati Kuu apigwa
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Shaaban Mwamba, juzi usiku alipata kipigo kutoka kwa maofisa wa kikundi cha ulinzi cha chama hicho waliokuwa katika eneo ambalo mkutano wa Kamati Kuu ulifanyika, baada ya kutuhumiwa alikuwa akiwasiliana na wafuasi wa Zitto.
Post a Comment