KUTOKANA NA UFINYU NA ONGEZEKO LA UUAZAJI BIDHAA KANDO KANDO MWA BARABARANI ,WAENDESHA MAGARI HUPATA ADHA KUBWA NA HATA KAUPATA AJALI.
Source Raia Mwema ; Paul Sarwatt - Arusha
WAFANYABIASHARA wanaomiliki maduka makubwa katikati ya mji wa Arusha wamemlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kutokana na hatua yake ya kuruhusu wafanyabiashara wadogo (wamachinga) kufanya biashara zao nje ya maduka yao, kinyume cha sheria za Jiji.
Katika barua hiyo ya Desemba 3, mwaka jana, iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Kitwana Mnaro na Katibu wake Ahmednoor Jamal, wanamlalamikia Mulongo kwa uamuzi wake wenye “malengo ya kisiasa” wa kuwaacha wamachinga wafanye biashara zao nje ya maduka yao.
Barua hiyo inaeleza kuwa uamuzi huo wa Mkuu wa Mkoa umelenga kukidhi matakwa ya kisiasa, wakimkariri kuwa uamuzi huo unatokana na kile kinachotajwa kuwa “hali ya kisiasa kutokuwa nzuri mjini Arusha.”
“Mheshimiwa sisi wafanyabiashara wa Arusha tumeshangazwa na uamuzi wako wa kuwaacha (kuwaruhusu) wamachinga wafanye biashara zao nje ya maduka yetu eti hali ya siasa si nzuri,” ilieleza sehemu ya kwanza ya barua hiyo.
Arusha ni kati ya majimbo yenye siasa za ushindani nchini, kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ushindani ambao unatajwa kutokuwa na maslahi yoyote kwa wananchi wa Arusha.
Barua hiyo inaendelea kueleza; “Mheshimiwa uamuzi huo si sawa kabisa, itakuwa haujatutendea haki kwa kuwa sisi tunalipa kodi ya nyumba ambazo tumepangishwa, tunalipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi ya mapato TRA na wenzetu hawachangii hata kidogo, halafu unasema hali ya siasa si nzuri waachiwe wafanyabiashara, kweli ndiyo sawa?” wanaohoji kupitia barua yao hiyo.
Wamsifu Mkurugenzi wa Jiji
Katika barua yao hiyo, wafanyabiashara hao wamemsifu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Zipora Liana, kwa uamuzi wake na mpango aliopanga kuhusu wamachinga kwamba ni mzuri na ungeiletea heshima serikali.
“Tunakushukuru mkurugenzi kwa nia yako nzuri kutusaidia kilio chetu hata kama umekwamishwa, tumeona juhudi zako wewe ni kiongozi si mtawala,” iliendelea kusomeka barua hiyo.
Wafanyabiashara hao wanaeleza kuwa, kabla mkurugenzi hajapanga kuwaondoa wamachinga alifanya utafiti na kuelewa walikuwa wanatozwa fedha kama malipo ya ushuru na ndiyo maana walikuwa wanajiona wana haki ya kufanyabiashara zao nje ya maduka.
“Mkurugenzi, Mwanasheria na Ofisa Biashara walifanya kazi ya kukomesha wamachinga kilipishwa fedha na wanaokamatwa walitozwa faini na wakapanga mpango ambao wewe (Mulongo) umeukataa,” walieleza wafanyabiashara hao.
Mulongo ajibu mapigo
Akijibu madai ya wafanyabiashara hao katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Raia Mwema, Mulongo alikiri kuandikiwa barua ya malalamiko.
“Ni kweli nimepokea barua hiyo, ikieleza matatizo ya wamachinga kufanya biashara zao katika mitaa ya katikati ya mji, lakini hata hivyo nina shaka na uhalali wa walioandika barua hiyo, maana tuliwaagiza wafike ofisini kwangu kwa mashauriano lakini hawakutokea kabisa hadi leo,”
“Hilo la hali ya kisiasa ni masuala yanayotungwa tu na kutaka kunibebesha dhambi ambayo sihusiki nayo. Suala la msingi ni njia bora ya kuondoa wafanyabiashara hao na si vinginevyo,” alisema.
Akielezea tatizo hilo la wamachinga, Mulongo alisema kabla ya suala hilo kulalamikiwa na wafanyabiashara, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alitaka kufahamu kwa kina, ofisi ya Jiji ilivyojipanga kutatua tatizo hilo.
“Katika kikao cha viongozi wa serikali za mitaa kilichofanyika kabla ya Desemba, tuliwauliza watu wa Jiji (Mkurugenzi na wakuu wa Idara) kuhusu mpango wao wa kuwaondoa wamachinga waliozagaa katika mitaa ya Jiji, lakini majibu yao yalikuwa ya kubabaisha tu,” alisema Mulongo.
Alisema Mwanasheria wa Jiji alieleza kuwa tayari wameandaa mpango wa kuwaondoa wamachinga kwa kuwatumia polisi ambao watakuwa na kazi ya kuwakamata, mahakimu watatu ambao watakuwa na kazi ya kuwahukumu wafanyabiashara hao.
“Hapa ndiyo tulipotofautiana na watu wa jiji, haingii akilini polisi wakamate wafanyabiashara na hapo hapo hakimu awahukumu, si katika nchi kama Tanzania ambayo inafahamika duniani kote kwa kuheshimu utawala wa kidemokrasia,” alieleza Mulongo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema: “Kama Mkuu wa Mkoa niliwashauri kuwa ni vyema wakaja na mipango ya kueleweka kutatua tatizo hilo moja kwa moja kwa kuwapatia wamachinga maeneo ya kufanyia biashara zao na kuwahamisha kwa njia za kistaarabu.”
“Hadi sasa unapozungumza nami, Jiji bado hawajaleta mpango wowote unaoeleza mpango muafaka wa kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo ya katikati ya Jiji kwa njia za kiusalama,” alisema Mulongo.
Mulongo alisema kwa mujibu wa uzoefu wake wa muda mrefu serikalini, njia za kuwaondoa wafanyabiashara hao wadogo zinahitaji maelewano na si nguvu.
Aliongeza kuwa halmashauri ya jiji inapaswa kutambua wajibu wake, kwa kutenga maeneo ya wafanyabiashara wadogo, na pia kuboresha baadhi ya masoko ikiwemo soko jipya la uliokuwa uwanja wa wazi wa Unga Limited.
“Tulitarajia kwamba halmashauri ya jiji wangeboresha mazingira ya soko hilo kwa kuweka paa na kutengeneza mifumo ya maji safi na majitaka kwasababu uwezo huo wanao lakini hawajafanya hivyo na soko hilo halitumiki ipasavyo hasa kipindi cha mvua kutokana na mazingira magumu ya kibiashara”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Zipora Liana hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Liana na Mkuu huyo wa Mkoa wanaelezwa kuwa katika mgogoro mkubwa kikazi na hivi karibuni Mulongo alikaririwa na vyombo vya habari akitoa siku sita kwa Mkurugenzi huyo kumwomba radhi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, Meya Gaudance Lyimo na viongozi wengine, kwa madai ya kurekodi mazungumzo yao na kuyapeleka ofisi ya Waziri Mkuu, kuwachongea.
Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Mipango Miji ambaye pia ni diwani wa kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro, aliwatupia lawama Mulongo na John Mongela.
“Mwaka 2011 halmashauri ilipitisha maazimio ya kuwajengea wamachinga jengo kwa kupanua zaidi soko la Kilombero, kwa kukopa fedha kutoka benki ya TIB na upanuzi huo ungechukua hadi wamachinga 800,” alikumbusha Ephata.
Alisema wakati mipango hiyo ikiwa imeiva, Mulongo na Mongela walihamishiwa Arusha na kwa pamoja, walikataa mpango huo kwa sababu zilizoaminika ni za kisiasa na hivyo kushinikiza wamachinga kuahamishiwa uwanja wa NMC Unga Limited.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela naye hakupatikana kuzungumzia suala hilo, zikiwamo lawama zinazoelekezwa kwake.
Wafanyabiashara wadogo (wamachinga) wameuvamia mji wa Arusha tangu Julai, mwaka jana, wakifanya biashara kiholela.
Post a Comment