Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wakati umefika kwa Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa sera itakayozingatia maslahi ya walimu wa madrasa, ili kuthamini juhudi zao za kuwafundisha watoto.
Amesema walimu wa madrasa wana kazi kubwa ya kuisaidia jamii katika malezi na kuwajenga watoto kimaadili, hivyo hakuna budi kuthaminiwa kwa kazi hiyo ambayo muda wote wamekuwa wakiifanya kwa kujitolea.
Akizungumza katika hafla ya maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na madrasat- Muumin Islamiya ya Muembeshauri, Maalim Seif amesema hatua hiyo itasaidia kuwapa moyo walimu hao na kuzidisha ari ya kufundisha.
Kwa upande mwengine Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesisitiza suala la umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi, na kuwashauri viongozi wa kijamii kuacha tabia ya kutoa kauli zinazoweza kuchochea chuki miongoni mwa wanajamii.
Aidha amesisitiza haja kwa wanajamii kuhimizana na kukumbushana juu ya kulinda mila, silka, kuuenzi na kuuendeleza utamaduni wa Zanzibar.
Amefahamisha kuwa katika kuuenzi utamaduni na silka za Wazanzibari, hakuna budi kwa wazazi kuwasomesha vizuri watoto wao, ili wajue elimu zote pamoja na historia ya utamaduni wao.
Ameonya kuwa iwapo juhudi hizo za kuwaelimisha watoto hazitoungwa mkono na jamii nzima hasa katika ngazi za familia, jamii itaendelea kushuhudia mporomoko mkubwa wa maadili, ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya malezi iko katika ngazi ya familia.
Katika kuunga mkono juhudi za madrasa hiyo, Maalim Seif ameahidi kutoa kompyuta mbili pamoja na mifuko ya saruji kwa ajili ya kuiendeleza madrasa hiyo.
Mapema akisoma risala ya madrasa hiyo ustadh Baiya Maulid, amesema madrasa hiyo iliyoanzishwa mwaka 1995, kwa sasa inakusudia kuanzisha miradi itakayosaidia kukidhi mahitaji ya kuendeleza madrasa yao.
Amesema tokea kuanzishwa kwa madrasa hiyo wameweza kupata mafanikio mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha jengo la madrasa, kuhifadhisha kur’an, pamoja na kukuza mashirikiano baina ya walimu na wazazi.
Hata hivyo wamesema bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uchakavu wa vifaa vyao vya ofisi pamoja na kutaka kunyanyua jengo lao.
Hivyo wameiomba serikali pamoja na wahisani wengine kuweza kuungana nao katika kutatua kero hizo, ili kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira mazuri.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na waumini wa dini ya Kiislamu wakati akiwasili katika viwanja vya Alabama Michenzani Unguja, kwa ajili ya maulid yaliyoandaliwa na madrasat Muumin Islamiya ya Mwembeshauri.
Vijana wa Maulid ya home kutoka Chumbuni, wakisoma kasida kwenye maulid yaliyoandaliwa na madrasat Muumin Islamiya ya Mwembeshauri.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia “maulid ya home” kutoka Chumbuni, kwenye maulid yaliyoandaliwa na madrasat Muumin Islamiya ya Mwembeshauri.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza kwenye hafla ya maulid yaliyoandaliwa na madrasat Muumin Islamiya ya Mwembeshauri, katika viwanja vya Alabama Michenzani Unguja.
Wanafunzi wa madrasa mbali mbali wakisikiliza maulid yaliyoandaliwa na madrasat Muumin Islamiya ya Mwembeshauri. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Post a Comment