Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi.PICHA|MAKTABA
Kwa ufupi
Alipopewa nafasi hiyo, Muabhi alianza kusema kuwa amealikwa tu kwenye huo mkutano na kupangiwa ziara za kwenda mikoani kufanya maandamano hayo Pemba na Unguja
Dar es Salaam. Wajumbe wa Kundi la Tanzania Kwanza nje ya Bunge la Maalumu la Katiba jana waligawanyika mbele ya waandishi wa habari waliowaita kueleza mkakati wao wa kuandamana nchi nzima kupingana na mahasimu wao wa Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wajumbe hao walitangaza maandamano nchi nzima kwa lengo la kuwaeleza wananchi wawakatae Ukawa kwa madai kwamba wamewakashifu waasisi wa Muungano.
Kamati ya Tanzania Kwanza nje ya Bunge ilikuwa na wajumbe kutoka vyama saba vya siasa; CCK, Chausta, Tadea, Cuf, NLD, CCM na Chauma.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Augustino Matefu alieleza mpango huo na wakati anaendelea kuzungumza, aliingia Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi na kumfanya akatishe mazungumzo akisema afadhali huyo Katibu wa CCK ameingia, ndiye atakuwa mwongeaji mkuu, kisha akampa nafasi.
Achafua hewa
Alipopewa nafasi hiyo, Muabhi alianza kusema kuwa amealikwa tu kwenye huo mkutano na kupangiwa ziara za kwenda mikoani kufanya maandamano hayo Pemba na Unguja.
Alisema hayuko katika upande wowote wa vyama, akiwa na msimamo wake binafsi wa kusimamia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni.
Alisema anawaunga mkono Ukawa kwa kitendo cha kutoka nje ya Bunge baada ya kuona wanaburuzwa na kutukanwa matusi badala ya kutetea Rasimu ya Katiba ya maoni ya wananchi.
Mwabhi alisema Tanzania Kwanza waliona waunde kamati hiyo ya kufanya mikutano ikiwamo ya maandamano kwa lengo la kuhamasisha wananchi waweze kufikiria kuwa Ukawa walitoka nje ya Bunge ili Katiba Mpya isipatikane.
Wakati anaendelea kuzungumza na kuonekana amekuja na msimamo tofauti, alikatishwa akielezwa muda wake umeisha. Hata aliposema anataka dakika moja zaidi, alikataliwa.
Nje ya mkutano
Akizungumza na ukumbi wa Idara ya Habari (maelezo) ulipokuwa unafanyika mkutano huo, Muabhi alisema imepangwa kuwa katika mikutano yao mikoani watahamasisha mfumo wa serikali mbili ambayo haipo kwenye Rasimu ya Katiba na badala yake, alidai CCM kinataka kuingiza rasimu.
“Mimi niliteuliwa kuwa mjumbe katika kamati ya Tanzania Kwanza nje ya Bunge Maalumu la Katiba baada ya kupewa mwaliko mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka Morogoro.
Alisema atafanya mikutano hiyo kama alivyopangwa, lakini ataangalia uhalali wake. Alisema anataka kuona Ukawa wanapewa fursa ya kufanya maandamano yao ili kuweka uwiano sawa kwa sababu wote wanazunguka kwa lengo la kuelimisha wananchi juu ya mchakato wa Katiba.
Alisema Ukawa wana hoja za msingi, wanachokijadili wao ni Rasimu ya Katiba si kitu kingine, lakini wabunge wa CCM wanataka ifumuliwe hiyo rasimu na kuweka katika mfumo wa serikali mbili ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema atafanya mikutano hiyo akiwa na msimamo wake, hivyo CCM wasitegemee walimchagua ili wapate mteremko kupitia mgongo wake.
Maelezo ya Tanzania Kwanza
Awali, Matefu alisema kamati yake itafanya maandamano ya amani nchi nzima kwa lengo la kuwasihi Watanzania wa Zanzibar wawakatae Ukawa kwani wamewakashifu waasisi wa Muungano.
Alisema wajumbe wa Ukawa hawana mapenzi ya dhati ya kuwapatia Katiba Mpya na kwamba wajumbe wengi wameweka masilahi ya vyama na taasisi zao badala ya nchi.
Alisema watu hao wamekubali kutumiwa na mataifa ya magharibi kwa lengo la kuigawa Tanzania vipandevipande.
Alisema inaeleweka wazi kwamba madai ya kudai Katiba mpya ilibebwa na baadhi ya vyama vya siasa na taasisi fulani kwa lengo kudai kuunda Tume Huru ya Uchaguzi.
Matefu alisema wakiwa vijana wazalendo, wameweka utaifa kwanza, vyama baadaye kulipinga jambo hilo kwa hoja na kwa gharama yeyote.
Alisema watafanya maandamano na mikutano ya hadhara katika Mikoa ya Arusha, Mbeya, Kigoma, Dodoma, Mtwara, Dar es Salaam na Zanzibar.
Wakati huohuo; kundi la Tanzania Kwanza ndani ya Bunge limewataka Ukawa warudi bungeni ambako kazi ya kutengeneza Katiba inafanyika.
Mwenyekiti wa kundi hilo, Said Nkumba alisema muda wa kwenda katika viwanja vya mikutano haujafika na kuendelea kususia mchakato huo ni kuwanyima fursa wananchi wanaowawakilisha wenye matumaini makubwa ya kupata Katiba iliyo bora.
Mmoja wa wajumbe waliofuatana na Nkumba, Dk Emmanuel Nchimbi alisema hata kama ukawa wameondoka bungeni, Katiba mpya itapatikana.
Nyongeza na Sharon Sauwa na Ibrahim Bakari, Dodoma.
Post a Comment