Home » » RASIMU YA KATIBA KUTANGAZWA KWENYE GAZETI LA SERIKALI

RASIMU YA KATIBA KUTANGAZWA KWENYE GAZETI LA SERIKALI

Written By JAK on Wednesday, January 22, 2014 | 10:53 PM

Flag of Tanzania in Africa, Tanzanian Flag

Kifungu 20 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo la 2013 inamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali Rasimu ya Katiba ndani ya siku thelathini (30) baada ya kukabidhiwa rasimu hiyo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.


Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue inaeleza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alikabidhiwa Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013, na ataichapisha kwenye Gazeti la Serikali litakalotolewa Ijumaa, tarehe 24 Januari 2014.

Aidha, kifungu 22 (1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo la 2013, kinampa madaraka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuteua wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka miongoni mwa majina yanayopendekezwa kwao na makundi yaliyotajwa ndani ya Sheria hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakusudia kukamilisha uteuzi wa Wajumbe hao baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwanzoni mwa wiki ijayo na majina hayo kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama kifungu 22 (3) cha Sheria iliyotajwa inavyomtaka kufanya.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
Dar es Salaam.
22 Januari, 2014
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger