Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akiapishwa rasmi rais wa nchi hiyo mjini Antananarivo kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwezi Desemba 2013.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akisani kiapo chake tayari kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi wa Madagascar mbele ya Jaji Mkuu wan chi hiyo Jean –Michael Rasolonjatovo (kushoto) wakati wa sherehe za kumuapisha rais huyo zilizofanyika mjini Antananarivo.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akizungumza na wananchi wa Madagascar waliofurika ndani ya uwanja wa Antananarivo mara baada ya kuapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo mjini.
Picha na 5 na 6. Viongozi mbalimbali na wanachi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina mjini Antananarivo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe akimuwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za kumuapisha rais mpya wa Madagascar akiwa kwenye jukwaa kuu pamoja na viongozi wengine wa nchi za Afrika waliohudhuria sherehe hizo mjini Antananarivo.Wengine wanaoonekana kutoka kulia ni Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chisano, Rais wa Zambia Ipikefunye Pohamba na aliyekuwa rais wa Madagascar Andry Raojolina.
Viongozi mbalimbali na wanachi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina mjini Antananarivo.
Gwaride maalum la jeshi la Madagascar wakati wa sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo Hery Rajaonarimampianina.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akikagua gwaride la majeshi ya Madagascar baada ya kuapishwa.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akiwasili Ikulu ya nchi hiyo mjini Antananarivo.
Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO, Antananarivo, Madagascar.
Tanzania imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Madagascar katika masuala mbalimbali na kuhakikisha kuwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo na jumuiya za kimataifa vinaondolewa kufuatia nchi hiyo kurejesha utawala wa kidemokrasia.
Akizungumza katika mahojiano maalum mjini Antananarivo, Madagascar, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe amesema kuwa sasa serikali ya Madagascar imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano sio tu na Tanzania bali nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya za kimataifa.
Waziri Membe ambaye alikuwa amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Madagascar Bw. Hery Rajaonarimampianina zilizofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo jana amesema kuwa Tanzania imefurahishwa na hatua hiyo na kuongeza kuwa huo ni ushindi mkubwa kwa SADC.
Amesema kuwa mwaka 2009 Madagascar iliingia katika machafuko yaliyosababisha serikali halali iliyokuwepo madarakani ya Rais Mark Ravalomanana kupinduliwa na kufafanua kuwa Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Amani na Usalama cha nchi za jumuiya ya SADC (TROIKA) imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa amani ya kudumu inapatikana nchini humo.
“Kiongozi mpya wa Madagascar aliyepatikana na kuapishwa ni ushindi kwa Tanzania kwa sababu Rais Jakaya Kikwete amejihusisha sana na upatikanaji wa kiongozi huyo, kama tunakumbuka rais Kikwete alimuita nchini Tanzania kwa mazungumzo rais aliyekuwa madarakani Bw. Andry Rajoelina mara nne, mazungumzo haya yamezaa matunda tunayoyaona leo” amesema Mh. Membe.
Amefafanua kuwa yapo mambo makubwa ambayo Tanzania imeyafanya kufanikisha kupatikana kwa amani ya kudumu nchini Madagascar ikiwemo upatikanaji wa katiba ambayo ilikamilika mwezi wa 8 mwaka 2013 ,kufanikiwa kuwashawishi Andry Rajoelina na Mark Ravalomanana waliokuwa mahasimu kutoshiriki kugombea katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Amesema Tanzania imefurahishwa na kitendo cha rais Andry Rajoelina aliyeingia madarakani kwa kufanya mapinduzi kukubali kuachia madaraka na kuachia utawala wa demokrasia utawale nchini humo.
Ameeleza kuwa Tanzania sasa iko tayari kushirikiana na Madagascar na kama mjumbe wa SADC itahakikisha kuwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo vinaondolewa pia kuhakikisha kuwa kiongozi huyo mpya anashiriki mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika utakaoanza tarehe 30 mwezi huu.
“Tulimwahidi rais aliyekuwa madarakani Bw. Andry Rajolina kuwa atakapotekeleza hayo tunayoyataka ikiwemo kuanzisha mchakato wa katiba, kuruhusu utawala wa demokrasia, na kuruhusu uchaguzi ili kupata rais mpya sisi tutakuwa mstari wa mbele kushawishi nchi za SADC na nchi za AU kuwaruhusu kushiriki mikutano yote ili waweze kuijenga nchi yao na jambo hilo tutalifanya ” amesisitiza Mh.Membe.
Katika houtuba yake mara baada ya kuapishwa rais Rajaonarimampianina amesema kuwa utawala wake unaanza ukurasa mpya wa kuijenga upya nchi hiyo iliyokuwa imegawanyika kisiasa na kusababisha chumi wake kudorora huku akiueleza umati mkubwa wa watu waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake kuwa ataongeza mapambano dhidi ya rushwa na kuleta amani, utulivu na maridhiano kwa mustakabali wa taifa hilo.
Madagascar ambayo sasa inaingia katika utawala mpya wa rais Hery Rajaonarimampianina ambaye hapo awali alikuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo iliingia katika machafuko yaliyosababisha kuondolewa kwa utawala wa rais Mark Ravalomanana aliyekimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini.
Hery Rajaonarimampianina akiungwa mkono na rais aliyepita Andry Rajoulina anakuwa rais wa 4 wa nchi hiyo kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwezi Desemba 2013 uliompatia asilimia 53.3 dhidi ya mpinzani wake Bw. Jean Louis Robinson aliyepata asilimia 46.5.
Post a Comment