Source Habari Leo, By Peti Siyame, Mpanda
MGOGORO wa uongozi ndani ya Chadema umeendelea hatua kwa hatua kwa makada wa chama hicho wanaopinga uongozi wa Mwenyekiti, Freeman Mbowe, kuadhibiwa mmoja baada ya mwingine ambapo sasa imefika zamu ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Said Arfi.
Adhabu zilinza kuchukuliwa kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe kwa kuvuliwa nafasi zote za uongozi ndani ya chama, kabla ya kukimbilia mahakamani kunusuru uanachama wake na ubunge, ambavyo kama si Mahakama, leo asingekuwa navyo.
Walifuata wafuasi wakuu wa Zitto ndani ya Chadema ambao wanadaiwa kuwa maadui wa Mbowe, waliopewa jina la uhaini na wafuasi wa Mwenyekiti huyo, Samson Mwigamba na Dk Kitila Mkumbo, ambao pamoja na utumishi wao katika nafasi nyeti za chama hicho, leo si wanachama.
Kutokana na mgogoro huo, ambao ni wazi upande wa Mbowe ndio uliokuwa umeshika mpini na kuutumia vizuri dhidi ya upande wa Zitto, uliokuwa umeshika makali, Arfi aliamua kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa, hatua iliyotafsiriwa kuwa alikuwa mfuasi wa Zitto.
Tafsiri hiyo ilijidhihirisha pale chama hicho kilipoamua kufanya ziara zilizoitwa za kuimarisha chama, lakini zilizotumika kuwashughulikia wafuasi wa Zitto waliosalia mikoani, kutomshirikisha Arfi, ambaye bado ni Mbunge.
Katika ziara hizo, makada wanaomuunga mkono Mbowe, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mkurugenzi wa Uenezi na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, walifanya mkutano wa hadhara katika Jimbo la Mpanda Mjini, bila hata kuwepo kwa mwenyeji wao, Arfi.
Malalamiko
Katika mkutano huo uliofanyika mwezi uliopita, inadaiwa Lema na Mnyika walimkashifu Arfi katika mkutano wao wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kashaulili kuwa Arfi ni mnafiki kwamba alimsaidia Waziri Mkuu Mizengo Pinda apite bila kupingwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita katika Jimbo la Katavi wilayani Mlele.
Kutokana na madai hayo, viongozi wa Chadema katika jimbo hilo na mkoa huo, walifanya mkutano katika viwanja vya Maridadi, kuwaomba radhi wananchi wa Mpanda kutokana na kauli za viongozi hao wa Kitaifa.
Katika mkutano huo, viongozi hao akiwemo Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Katavi, John Malack na Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoani hapa , John Matongo, walielezea kushangazwa na kauli za Mnyika na Lema kwa kusafiri kwa gharama kubwa kwa helikopta ya kukodi kwa lengo la kuwakashifu viongozi wao akiwemo Arfi.
Washughulikiwa
Mwezi mmoja baada ya viongozi hao wa Mpanda kuomba radhi wananchi, kikao cha Halmashauri Kuu ya Chadema mkoani Katavi kimewasimamisha uongozi viongozi hao wawili na wenzao wanne.
Sababu za kusimamishwa zimetajwa kuwa ni kuwakashifu viongozi wakuu wa Kitaifa, Mnyika na Lema katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Mpanda mwezi uliopita.
Waliosimamishwa uongozi ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Katavi, Malack, Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoani hapa , Matongo na Mwenyekiti wa Jimbo la Mpanda Mjini, Seif Sipia.
Wengine ni Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini Joseph Mona, ambaye pia ndiye Katibu wa Mbunge, Arfi na Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini, Godfrey Kapufi.
Kapufi na Diwani wa Kata ya Makanyagio, Idd Nziguye mbali ya kusimamishwa uongozi, kikao hicho kimependekeza wavuliwe uachama kabisa kama ilivyokuwa kwa akina Dk Mkumbo na Mwigamba.
Aidha, kikao hicho pia kiliazimia Arfi achunguzwe wakimtuhumu kudhamini mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Maridadi mjini hapa unaodaiwa kutumika kuwakashifu Lema na Mnyika.
Uamuzi huo mzito ulifikiwa katika kikao hicho kilichofanyika jana kwenye ofisi zilizopo katika mtaa wa Mji wa Zamani mjini hapa kikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Magharibi, Masanja Katabi.
Ulinzi mkali wa walinzi wengi wa chama hicho uliowekwa wakati kikao hicho kikiendelea na Mwenyekiti wa jimbo la Mpanda Mjini, Sipia alilazimika kuhoji uhalali wa kikao hicho kwa madai wajumbe wake wengi hawakuwa wajumbe halali wa kikao hicho.
Kutokana na hoja hiyo Mwenyekiti wa kikao hicho, Katabi alimuamuru Mwenyekiti huyo wa Jimbo atoke nje kwa kile alichodai kuwa analeta vurugu ndani ya kikao.
Hata hivyo Sipia alikaidi agizo lake hilo ambapo vijana wa ulinzi wa chama hicho waliamriwa kuingia ndani ya kikako na kumwamuru Sipia atoke kwenye kikao hicho kwa nguvu.
Makonde
Kitendo hicho kilimkasirisha Sipia ambaye aliamua kuwashambulia kwa makonde na kuwazidi nguvu walinzi wawili wa ‘Red Guard’ wakaaanguka chini kisha Mwenyekiti huyo wa Jimbo la Mpanda Mjini aliamua kutoka kwenye kikao hicho ambacho kililazimika kusimama kwa muda kutokana na vurugu hizo.
Post a Comment