Home » » JUKUMU LA ULINZI WA NCHI NI LA KILA MTANZANIA – MDAU WA POLISI JAMII

JUKUMU LA ULINZI WA NCHI NI LA KILA MTANZANIA – MDAU WA POLISI JAMII

Written By JAK on Friday, February 28, 2014 | 9:42 PM

Mdau wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Bw.Faisal Juma Shahbhai ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe ya Police Family Day akiwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria katika moja ya ukumbi wa Hoteli ya Naura iliyopo jijini hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)


Mmoja wa wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Bw. Neil Karia ambaye alikuwa mwanakamati wa sherehe hiyo akiwaongoza wageni waalikwa katika sehemu ya chakula.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
TPF NET toka Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha wakiwa katika shamra shamra za kumuaga kwa kumpa zawadi aliyekuwa mwanachama mwenzao Mkaguzi Msaidizi wa Polisi mama Kivuyo ambaye amestaafu hivi karibuni.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)


Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Imeelezwa kwamba jukumu la kulinda amani  na usalama wa nchi ni la kila mtanzania yeyote  awe anaishi humu nchini au nje ya nchi. Hayo yameelezwa na Mdau wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Bw. Faisal Juma Shahbhai wakati wa sherehe ya Siku ya Familia za Polisi Mkoa wa Arusha katika kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 iliyofanyika wiki hii katika ukumbi wa Hoteli ya Naura iliyopo jijini hapa.

Bw. Faisal alisema kwamba yeye na wanajamii wengine hawapaswi kukaa pembeni na kuliacha suala la ulinzi kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama pekee bali wao wanatakiwa wawe watu wa kwanza katika kukabiliana na uhalifu ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwapa taarifa za mara kwa mara.

Mdau huyo aliongeza kwa kusema, ni vema kila mtu akatambua kwamba, kama yeye hajaathiriwa na matukio ya uhalifu basi ndugu yake au rafiki yake atakuwa amekumbwa na matatizo kutoka kwa wahalifu hao. Alisema ifikie wakati sasa jamii ijitoe kwa hali na mali katika kushirikiana na Jeshi la Polisi ili takwimu ya vitendo vya uhalifu izidi kupungua siku hadi siku.

“Ulinzi unaanza na wewe pamoja na mimi sio huko juu kwani ndio ambao tunawafahamu wahalifu  hivyo kila mmoja atambue majukumu yake ndani ya nchi na anatakiwa awaze naye ameifanyia nini nchi yake”. Alisema Bw. Faisal.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba, Jeshi la Polisi Mkoani humu lilifanya vizuri sana katika kupunguza vitendo vya uhalifu mwaka 2013 ikilinganishwa na mwaka 2012.

Alisema mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano mkubwa  kati ya Jeshi hilo na wananchi hivyo kutokana na hilo alimshukuru kila mmoja kutokana na mchango wake katika kuimarisha amani ndani ya Mkoa. 

Alisema Jeshi hilo Mkoani hapa litaendelea kufanya kazi kwa weredi na kutoa huduma bora kwa mteja wa ndani na wa nje hali ambayo itasaidia ustawi wa mahusiano bora baina ya wananchi na Jeshi hilo na hivyo kupata taarifa zaidi za uhalifu na wahalifu.

Kamanda Sabas aliwaomba wanasiasa waendelee kutoa ushirikiano zaidi kwa jeshi hilo kwani wao ni watu muhimu sana katika kuimarisha amani ndani ya mkoa huu.

Aidha akitoa takwimu za Usalama Barabarani alisema jeshi hilo mwaka 2013 limepunguza ajali hizo kwa asilimia 52.8 ikilinganishwa na mwaka 2012 lakini pamoja na mafanikio hayo tozo la notification limeongezeka toka Tsh. 1,245,520,000/= mwaka 2012 hadi kufikia Tsh. 2,025,540,000/= mwaka 2013.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger