Home » » Kanisa la Mkunazini Zanzibar lalipuliwa

Kanisa la Mkunazini Zanzibar lalipuliwa

Written By JAK on Tuesday, February 25, 2014 | 12:00 PM

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam

Source Habari Leo -Khatib Suleiman, Zanzibar

MILIPUKO minne imelipuka mjini Zanzibar na kujeruhi watu wanne.

Milipuko miwili imelipuka kwa wakati mmoja karibu na Kanisa la Mkunazini, mwingine kwa mfanyabiashara wa chuma chakavu na mwingine katika mgahawa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kutokea kwa milipuko hiyo na kuongeza kuwa uchunguzi zaidi wa matukio hayo unaendelea.

“Ni kweli milipuko miwili imetokea karibu kwa wakati mmoja, katika Kanisa la Mkunazini Unguja pamoja na mgahawa wa Mercury uliopo jirani na Bandari Kuu ya Malindi...tumechukua baadhi ya mabaki kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema.

Jeshi la Polisi limesema hakuna mtu aliyekamatwa hadi sasa na kuhusishwa na tukio hilo la milipuko ya mabomu.

Milipuko miwili katika Kanisa la Mkunazini imesababishwa na gari mmoja lililoegeshwa jirani la lango kuu la Kanisa ambalo mmiliki wake, Mohamed Ibrahim alijeruhiwa kidogo.

Msaidizi wa Kanisa la Mkunazini, aliyejitambulisha kwa jina moja la Fadha Masoud, alikiri kutokea kwa milipuko hiyo miwili katika kipindi cha dakika tano nje ya lango kuu la Kanisa ambapo huegeshwa magari mbalimbali.

“Tumesikia milipuko miwili katika kipindi cha dakika tano nje ya lango kuu la Kanisa, lakini tunamshukuru Mungu ndani ya eneo la Kanisa ni salama,” alisema Masoud.

Mlipuko wa nne umetokea Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo mvuvi mmoja aliokota chuma chakavu na kupeleka kwa fundi kwa ajili ya kuangaliwa, ndipo kilipolipuka na kusababisha majeruhi kwa watu waliokuwepo jirani na tukio hilo akiwemo fundi Juma Abdallah.

Msaidizi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Hamad Said Masoud alithibitisha kutokea kwa mlipuko huo. Alisema uchunguzi kujua chuma hicho kama ni bomu au kifaa kingine, unaendelea kwa sasa.

“Tumechukua sampuli ya kifaa kinachodhaniwa kuwa ni bomu kwa ajili ya kukifanyia uchunguzi zaidi na tutatoa taarifa zaidi,” alisema.

Kamanda Masoud aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Fundi Abdallah, ambaye ameumia vibaya na kulazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Wengine ni Shaaban Khamis, Simai Hussein na Pandu Haji Pandu ambaye ameumia sehemu ya mguu.

Hilo ni tukio la tatu katika kijiji cha Unguja Ukuu, ambapo watu huokota vyuma chakavu vinavyodhaniwa kuwa masalia ya mabomu, ambayo hutumiwa katika mazoezi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Eneo la kijiji cha Unguja Ukuu, limekuwa likitumiwa na JWTZ kwa ajili ya mazoezi ya kivita kwa wapiganaji wake.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger