MGOMBEA ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa
Source Habari Leo -Frank Leonard, Iringa
MGOMBEA ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa amesema hana chembe yoyote ya uzungu. Amesema anakishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kumtuhumu kwamba si Mtanzania.
"Kama kila Mtanzania anayekwenda nje ya nchi kusoma anapoteza uraia wake, basi nchi hii itakuwa na wanasiasa na Watanzania wengi wanaokosa sifa ya kuendelea kuwa raia wa Tanzania," alisema.
Alisema hayo kwenye mkutano wa kuzindua kampeni za kinyang'anyiro hicho. Uzinduzi huo ulifanyika katika Kijiji cha Mseke, jimboni humo juzi.
Mgimwa alisema; "Mimi ni Mhehe, mtoto wa familia ya marehemu Dakta William Mgimwa, nimezaliwa Iringa, nimesoma Iringa na baadaye nikabahatika kwenda Uingereza nilikopata Shahada yangu ya Kwanza na ya Pili."
Alisema kwa mara ya mwisho kuitumia Pasipoti yake ya Tanzania, ilikuwa Desemba mwaka jana alipokuwa anakwenda Afrika Kusini kumuuguza marehemu baba yake Dk Mgimwa.
Mgimwa alisema Chadema hawana sera na katika shughuli zao za siasa za kila siku, wamekuwa wakipoteza muda mwingi, kuzungumza habari binafsi za watu, badala ya kuzungumzia jinsi wanavyoweza kuyakabili matatizo ya Watanzania.
"Jimbo la Kalenga limepiga hatua kubwa ya kimaendeleo, lakini pia lina changamoto zake; waseme kabla ya kuja Kalenga wao na mgombea wao wamechangia shughuli ipi ya maendeleo katika jimbo letu hili?" Alihoji.
Alisema akichaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo, kazi yake itakuwa kumalizia utekelezaji wa Ilani ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 na ahadi mbalimbali zilizoahidiwa na marehemu baba yake.
"Kipaumbele changu cha kwanza ni elimu, cha pili kilimo, cha tatu miundombinu na mawasiliano; hizo ni baadhi ya kazi nitakazofanya ili kuwaletea watu wangu maendeleo," alisema.
Kabla mauti hayajamkuta Januari 1, mwaka huu, Dk Mgimwa alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo la Kalenga na Waziri wa Fedha. Uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo utafanyika Machi 16, mwaka huu katika kinyang'anyiro kinachoshirikisha vyama vitatu vya siasa.
Mbali na CCM, vyama vingine ni Chadema ambacho mgombea wake ni Grace Tendega na Chausta, kilichomsimamisha Richard Minja.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisema wanaoituhumu Chadema wakiihusisha na ubaguzi, hawakosei ;na ndio maana kwa ubaguzi ule ule, wamemkataa Mtanzania mwenzao, kwamba si raia.
Post a Comment