Sehemu ya wasomi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini Tanzania,
wakifuatilia mjadala wa Rasimu ya Katiba mpya ulioandaliwa na Taasisi ya
Utafiti ya Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP)
jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Mroki Mroki).
By Halima Mlacha
WAKATI Bunge la Katiba likiendelea mjini Dodoma, makundi mbalimbali yamekuwa yakiendelea kuibuka na kutoa msimamo wao kuhusu moja ya ajenda inayojadiliwa sana ya mfumo wa serikali unaofaa kwa Tanzania.
Makundi hayo ambayo ni pamoja na vyama vya siasa, wasomi na wanaharakati yamekuwa yakitoa misimamo tofauti ambapo baadhi yao wanataka Katiba itambue mfumo wa Serikali moja, wengine mfumo wa Serikali mbili na makundi mengine mfumo wa Serikali tatu.
Wakati makundi hayo yakigawanyika katika matakwa ya aina ya Serikali itakayowafaa Watanzania, tayari Rasimu ya Katiba mpya iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya katiba, imebainisha wazi kuwa Watanzania wanataka muundo wa Serikali tatu.
Wakati akiwasilisha Rasimu hiyo ya pili mbele ya Rais Jakaya Kikwete, Jaji Joseph Warioba alibainisha kuwa utafiti wa Tume hiyo umebaini kuwa kwa Tanzania Bara asilimia 13 wanataka Serikali moja, asilimia 24 wanapendekeza Serikali mbili, asilimia 61 wanapenda kuona serikali tatu.
Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza Serikali mbili na asilimia 60 wakapendekeza Muungano wa mkataba huku watu 25 sawa na asilimia 0.1 wakitaka Serikali moja. Alisema vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na baadhi ya taasisi za Serikali zilipendekeza muundo wa Serikali tatu, huku akitolea mfano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Baraza la Katiba Ofisi ya Waziri Mkuu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Jaji Warioba alisema: “Kupendekezwa kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika haina maana ya kuunda nchi mpya. Kinachopendekezwa ni kutenganisha mamlaka ya Mambo ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika. Tanganyika na Zanzibar hazina hadhi ya Jamhuri, na kwa hiyo si “Sovereign States” kama ilivyo Jamhuri ya Muungano.”
Jaji Warioba alisema Serikali mbili inawezekana lakini kwa masharti kwamba Katiba ya Zanzibar inayotamka kwamba Zanzibar ni nchi ifanyiwe marekebisho na kuonekana kwamba ni sehemu inayounda Tanzania.
Hata baada ya kutoka kwa Rasimu hiyo, mjadala wake ulitawala katika eneo la muundo wa Serikali ambapo tayari, vyama vya siasa vya upinzani Chadema, CUF na DP vimetoa misimamo yao na kutaka Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wakati vyama hivyo vikiweka msimamo huo, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyokutana kwa siku mbili mjini Dodoma imeondoka na msimamo wa kutaka wajumbe wake wa bunge hilo la Katiba kutetea hoja ya Serikali mbili. Hata hivyo, pamoja na misimamo ya vyama hivyo vya siasa, pia makundi mbalimbali yamekuwa yakikutana kujadili Rasimu hiyo na kuibuka na misimamo yao kulingana na wanavyoona na kati ya makundi hayo ni pamoja na kundi la wasomi nchini.
Kundi hilo, ambalo liliwasilishwa na Taasisi ya Utafiti ya Vyuo Vikuu vya Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAURP), lilikutana na kujadili rasimu hiyo ya pili ya Katiba hasa eneo la muundo wa Serikali kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inapata Katiba bora.
Katika mjadala huo kulikuwa na mada 12 zilizowasilishwa ikiwemo inayoelezea historia ya mfumo wa Serikali tatu nchini Tanzania, muundo wa Serikali moja, uzoefu wa mchakato wa Katiba katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Nigeria, Afrika Kusini na Kenya.
Akizungumza kwa niaba ya wasomi hao mara baada ya kumaliza mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa ESAURP, Profesa Ted Maliyamkono, anaweka wazi kuwa baada ya mjadala huo wasomi hao wameweka msimamo wao wa kutaka mfumo wa Serikali moja ama katika katiba ijayo au hata hapo baadaye.
Anasema uamuzi huo umetokana na athari ambazo wasomi hao wamezianisha za mfumo wa Serikali tatu ambazo ni pamoja na ubaguzi kwa watanzania ikiwemo gharama za uendeshaji wa Serikali hizo tatu.
“Ukweli ni kwamba kwa nchi inayoendelea kama Tanzania kamwe haiwezi kuendelea ikiwa na mfumo wa Serikali tatu au nne,” anasisitiza Maliyamkono. Anasema wao kama wasomi msimamo na mapendekezo yao katika mchakato wa Katiba unaoendelea ni Serikali moja, kwa kuwa hiyo ndio Serikali pekee yenye uwezo wa kujenga umoja wa Watanzania na kuwatatulia matatizo yao yaliyopo kwa muda mrefu.
Anasema kwa sasa mfumo wa Serikali mbili unaotekelezwa kupitia Katiba ya mwaka 1977 una walakini ambao ni pamoja na ubaguzi kwa kuwa upande wa Zanzibar wameonekana kunufaika zaidi na muungano kuliko Watanganyika. Katika mfumo huo wa Serikali mbili ambao ni muunganiko wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar, ni Zanzibar pekee inayojiendesha kama nchi ikiwa na Rais, Bunge, bendera yake, wimbo wa taifa pamoja na Katiba tofauti na Tanganyika.
“Tanzania bara wanatumia fedha nyingi kujijenga na faida tunatumia wote na Wazanzibari wakati Watanganyika hawanufaiki na chochote upande wa Zanzibar, hii ni kero kubwa kwetu, lazima Katiba iyaangalie mambo kama haya ambayo utatuzi wake ni Serikali moja tu,” anasisitiza.
Wakati akiwasilisha mada yake kuhusu kifungu hicho cha rasimu kinachotamka uwepo wa Serikali tatu kwenye Katiba ijayo, Profesa Bonaventura Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasisitiza kuwa suluhisho pekee la matatizo yanayowakabili Watanzania kwa muda mrefu ni Serikali moja.
Anasema serikali moja itaondoa utata uliopo sasa wa kero takribani 28 za muungano ambazo kila siku zinaongezeka ikiwemo utata wa Rais yupi mwenye mamlaka kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali za Zanzibar (SMZ).
Profesa Rutinwa anakumbushia kuwa kwa sasa tayari kuna Katiba mbili ya Tanzania bara na Katiba ya Zanzibar hivyo itakapoundwa Serikali ya tatu lazima kutakuwa na Katiba ya Tanganyika ambayo kama ilivyo kwa Zanzibar nayo itawatambua Watanganyika pekee.
“Katiba ya sasa ya Zanzibar ina fasili ya Mzanzibari na haki zake hivyo hivyo itakapoundwa Serikali ya tatu kutakuwa na Katiba ya Tanganyika itakayokuwa inamfasili Mtanganyika na haki zake,” anasisitiza.
Anabainisha kuwa jambo la muhimu kwa sasa ni kuwepo kwa Katiba itakayowaunganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja hasa katika eneo la haki zao zinazotambulika duniani kote.
Hizi ni pamoja na raia kuwa na haki ya kupiga kura, haki ya kwenda kokote nchini kwake, haki ya kufanya kazi na upatikanaji wa soko. “Serikali mbili za sasa bado zina uwalakini kwa kuwa pamoja na kuwepo kwa Katiba ya Tanzania, bado Katiba ya Zanzibar inatoa haki kwa Wanzazibari zaidi kuliko wabara, huku wabara wakikosa haki ya kuwa na ardhi wala kupiga kura lakini Wazanzibar wana-enjoy haki zote za bara,” anasema.
Kwa upande wake, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine, Dk Charles Kitima, anasisitiza kuwa msomi yeyote duniani akiulizwa achague aina ya Serikali kwa ajili ya nchi yake lazima achague mfumo wa Serikali moja kwa kuwa ndio kiungo cha umoja, amani na utulivu kwa nchi yeyote.
Anasema kwa upande wa Tanzania ni vyema ikajikita katika mfumo wa Serikali moja kwa kuwa ndio matakwa ya waasisi wa nchi hiyo ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Dk Abeid Amani Karume.
“Waasisi hawa matakwa yao yalikuwa ni kuwa na Serikali moja itakayounganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja, walianza na Serikali ikiwa ni utaratibu wa kujiandaa tu na lengo lilikuwa hapo baadaye nchi hizi mbili ziwe kitu kimoja, sasa sisi leo kweli ni haki kuja na mfumo wetu?” Anahoji.
Akiwasilisha mada kuhusu uzoefu wa Kenya katika mchakato wa kuanzisha Katiba mpya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sera Afrika iliyopo Nairobi Kenya, Profesa Peter Kagwanja, anasema Tanzania inao uwezo wa kutengeneza Katiba bora yenye maslahi ya wananchi wake, iwapo matakwa ya wananchi yatazingatiwa hasa matatizo yao.
“Sisi mchakato wetu ulichukua muda mrefu tangu mwaka 1988 na Katiba ikapatikana 2010, lengo lilikuwa si kuwa na Katiba mpya ili kujiendeleza kiuchumi, lengo lilikuwa ni kuwa na Katiba mpya ili kukabiliana na matatizo ya kutokuwa na utulivu wa kisiasa, Tanzania inaweza kuwa na Katiba pia itakayoangalia matatizo yao,” anasisitiza.
Dola moja, serikali mbili Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akiandika katika mtandao wa kijamii wa Facebook anapendekeza mfumo wa Dola moja yenye serikali mbili ya Zanzibar na Tanganyika ambazo kimsingi unakaribiana na mfumo wa serikali tatu.
Zitto anasena pengine mjadala kuhusu idadi ya serikali usijibu kero za Muungano kama wengi wanavyoamini ikiwemo Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Ni kweli Wazanzibari wanataka uhuru zaidi na wengine hawataki kabisa Muungano. Unawalalia. Unawanyima uhuru wa kuamua baadhi ya mambo yao na japo halisemwi unawanyima wanasiasa wa Zanzibar mamlaka ya masuala mengine ambayo yangewafanya wajilimbikizie madaraka,” anasema.
Anasema kwa upande wa Bara pia kuna watu ambao wanaongezeka kila kukicha wakitaka “Tanganyika yao. Wamechoshwa na kelele za Wazanzibari. Hawawataki Wazanzibari kujaa kwenye Bunge la Muungano wakati wapo idadi yao ni kiduchu.” Anasema wanasiasa nao, japo hawasemi waziwazi wanataka wawe na mamlaka zaidi bila kulazimika kushauriana na wanasiasa wa Zanzibar na hasa linapokuja suala la wagombea urais.
“Kimsingi idadi ya wapinga Muungano inazidi kuongezeka siku hata siku. Ukiwauliza kwa nini hawataki Muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni Mzanzibari atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema Wazanzibari wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu.”
Anasema hata wapenda Muungano hawana majibu ya kuridhisha sana na ya kukonga nyoyo za wapinga muungano wanaoongezeka. Anasema majibu kwamba Muungano huu ni wa aina yake Afrika na duniani na kwamba ni alama pekee ya kuonesha Mwafrika kupinga mipaka ya kikoloni hayawaingii sana kichwani baadhi ya watu.
Zitto anasema kinachotakiwa ni kuurekebishe Muungano wetu ambao ni muhimu kwani ulivyo sasa unaibua kero kila kukicha. “Sasa tufanyeje? Serikali moja itaimeza Zanzibar. Serikali Tatu ni gharama kuendesha na Serikali mbili zimeimeza Tanganyika na watu wanataka Tanganyika yao na zinainyima uhuru Zanzibar na watu wanataka wawe huru zaidi.
Mfumo wa Serikali ngapi na kadhalika ni moja ya mikakati ya wanasiasa katika kusaka vyeo. Sisemi sio halali kujadili lakini kiukweli mfumo gani wa Muungano hautaongeza fungu la dagaa kwa mwananchi wa Kagongo au sinia la ubwabwa kwa mwananchi wa Mkanyageni,” anasema.
Zitto katika andiko lake anapendekeza tuwe na Dola Moja tu yaani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Shirikisho la Tanzania. Anafafanua: “Tuwe na Rais mmoja tu mwenye mamlaka kamili ya asasi za dola – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Uhamiaji, Sera za Fedha na jukumu la jumla la kusimamia ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Zitto anapendekeza Rais huyo achaguliwe na Watanzania wote wa pande zote mbili za Muungano kwa kupata zaidi ya nusu ya kura za pande zote za Muungano huku tukiachana na mgombea mwenza. Kisha anasema: “Zanzibar iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya Muungano. Tanganyika iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya Muungano.
Hawa watateuliwa na Rais wa Muungano kutoka chama chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi Tanganyika na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Wote watakuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa utaratibu kwamba iwapo Rais anatoka Zanzibar, basi Waziri Mkuu wa Tanganyika atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa Rais.”
Anasema Mawaziri wakuu hao wataongoza mabaraza yao ya mawaziri na watakuwa na nguvu ya kuteua na kufukuza mawaziri lakini hawatakuwa wabunge katika Bunge la Muungano. Anapendekeza kwamba Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye Wajumbe wasiozidi 101 pamoja na Rais wa Bunge la Muungano.
“Wabunge wa Muungano watatoka kwenye mikoa (au Majimbo kama sera ya Majimbo itakubalika). Kwa utaratibu wa sasa kila mkoa utachagua wabunge wawili, mmoja mwanamke mmoja mwanamume kwenda Bunge la Muungano. Wajumbe wa ziada watatokana na uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata kwenye kura za Rais wa Muungano,” anasema.
Anasema Rais wa masuala ya Muungano atakuwa Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Bunge la Muungano na Rais huyo kwa mwaka mara moja atahutubia Baraza la Taifa (Wabunge wa Bunge la Muungano na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka kila upande wa Muungano kitu ambacho hali ya taifa.
Zitto anamalizia andiko lake kwa kusema: “Mkuu wa nchi mmoja, Dola moja ya Jamhuri ya Muungano. Serikali mbili na kila upande una Serikali yake yenye mamlaka kamili ya maisha ya watu wao ya kila siku.
Haya matatu pamoja na Serikali ndogo ya Muungano, lakini tutakuwa tumepata kila kitu labda. Wenye kutaka Uhuru mpaka Zanzibar watapata. Wenye kutaka Tanganyika watapata na wenye kutaka Muungano kama Dola yenye nguvu watapata.”
Post a Comment