Home » » Mashine za EFDs ‘kung’ata’ mabasi ya abiria

Mashine za EFDs ‘kung’ata’ mabasi ya abiria

Written By JAK on Sunday, February 23, 2014 | 9:33 AM

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh1CZxWmuSFIwgj5AmFNNlQMyh1oQqEQehvC_i2DAuO3uDsMUKdcOvAXMDIcY0L0lDCoPYQBbQNkmgbkFZjPvDLyss09PtZKkaw8leQd_dLcCsJnAbjMhKilL9ER24SmFPffnSSijZ6/s640/IMG_0119.jpg
 Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) ipo katika mchakato wa kuanzisha mfumo wa mashine za kieletroniki (EFD) katika utoaji wa risiti kwenye mabasi ya abiria, kasino na magari ya mizigo. Pamoja na kuelezea utanuzi wa wigo wa matumizi, pia imesema itapambana na wafanyabiashara wote watakaokataa kutumia mashine hizo kwa lengo la ‘kukwepa kodi’.

Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya ameonya kuwa kusiwe na visingizio vyovyote ambavyo vinataka kusiwe na utekelezaji wa sheria ya matumizi ya mashine hiyo inayosaidia katika ukusanyaji wa kodi kwani kuna taratibu za kufuata katika kukabiliana na changamoto zozote na kusema migomo na maandamano hayatasaidia.

Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Elimu kutoka TRA Makao Makuu, Hamisi Lupenja, alibainisha mpango huo wa kutumia mashine hizo kwenye magari ya abiria alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari mkoani Mbeya wakati wa semina waliyoandaa kwa ajili ya kutoa elimu juu ya faida na matumizi ya mashine za kielektroniki katika kutoa risiti kwa walaji.

Alisema kwa sasa mamlaka hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha mfumo wa utoaji wa risiti katika mabasi ya abiria, kasino na magari ya mizigo kwa kutumia mashine za EFD, jambo litakalosaidia serikali kudhibiti mapato yake.

Hata hivyo alisema changamoto inayowakabili ni namna ya utoaji wa mashine hizo, “tunaangalia kama labda moja ifungwe kituo cha mabasi Ubungo na nyingine kituo cha mabasi Mbeya.”

“Lakini pia tunaangalia uwezekano wa kutoa mashine zinazotembea (EFD Mobile) ili kama mtu alikata tiketi Dar es Salaam, akishuka Morogoro akipanda abiria mwingine anakatiwa risiti,” alisema.

Katika siku za hivi karibuni wafanyabiashara wa kati ambao mauzo yao yanafikia Sh milioni 14 nchini wamekuwa wakizipinga na hata kugoma kufungua maduka yao, kwa madai mashine hizo zinauzwa bei kubwa hadi Sh 800,000.

Walidai pia mashine hizo za kutolea risiti zinaharibika mara kwa mara na zinashindwa kutoa risiti kwa wakati. 

Matumizi ya mashine hizo yaliyokuwa yaanze rasmi Mei mwaka jana yalisogezwa mbele mara tatu na kutakiwa kuanza kwa wafanyabiashara kununua mashine Januari 31 mwaka huu na sheria kuanza kufanya kazi Februari mosi mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Lupenja alisema kuwa wafanyabiashara wanaogomea matumizi ya mashine za EFD wana hofu kuwa wakitumia mashine hizo mauzo yao ya mwaka mzima yatafahamika kuwa ni kiasi gani na kodi watakayokadiriwa itakuwa ni kubwa.

“Ambacho hawafahamu ni kuwa kodi haikatwi kwenye mauzo ya mwaka mzima bali inakatwa asilimia 30 ya faida, kwa kuwa katika mauzo ya mwaka mzima kuna mtaji na gharama za uendeshaji,” alisema.

Kadhalika alisema baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakishiriki migomo ya kununua mashine hizo walikuwa wanakosea kwa kuwa mashine hizo zinawahusu wafanyabiashara wenye mauzo ya zaidi ya Sh milioni 14 kwa mwaka na si chini ya hapo.

Wakati Lupenja anabainisha mpango huo wa TRA, Waziri Saada akizungumza kwenye Mahafali ya sita ya Chuo cha kodi ambapo wanafunzi 660 walihitimu masomo yao alisisitiza kuwa sheria zitaendelea kufuatwa bila kusita.

Alisema serikali inakabiliwa na changamoto ya wananchi kutokubali kudai risiti wakati wa manunuzi pamoja na wafanyabiashara kuwa wagumu katika kutoa risiti kwa kutafuta visingizio.

“Hivyo wahitimu mnatakiwa kuwa mabalozi wetu katika kuelimisha watu kulipa kodi, lakini licha ya changamoto tunazokabiliana nazo serikali haitarudi nyuma katika kutumia mfumo uliopitishwa kisheria na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Alisema ikiwa kuna wafanyabiashara wanataka kupambana kisheria, serikali iko tayari kupambana nao lakini haiwezekani kurudi nyuma na kuendesha shughuli kama miaka 50 iliyopita.

Alisema, “sasa tunaenda na matumizi ya Sayansi na Teknolojia, hivyo lazima yaende katika kila sekta hususan ukusanyaji wa kodi kwani miaka 50 ya uhuru haiwezekani tukakubali kuendelea kufanya shughuli zetu bila teknolojia”.

Alisema wakati serikali inaendelea kutekeleza sheria hiyo, pia itaendeleza kutoa elimu kwa wale wasiofahamu vizuri mfumo huo au walioelewa vibaya kuhusu matumizi ya mfumo huo wa ukusanyaji mapato.
Alisema kuna nchi watu wake wanajivunia kulipa kodi lakini nchini watu wanajitahidi kutafuta mbinu za kukwepa ulipaji kodi, hivyo sheria hiyo iliyotungwa na bunge lazima itekelezwe.

Pia Waziri huyo alisema wizara yake katika bajeti ijayo itatenga Sh bilioni 4.6 katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuboresha na upanuzi wa chuo hicho cha kodi. Waziri huyo alisema amefarijika kusikia idadi ya wahitimu kuongezeka hasa wanawake ambao wamefikia 200 ambapo mwaka jana walikuwa 136 na kati yao wapo waliofanya vizuri.

Awali, Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Charles Sabuni alisema mahafali hayo yamehudhuriwa na Makamishna wa kodi toka Malawi, Zambia, Kenya na Lesotho.

Alisema kati ya wahitimu hao 200 wanawake na 460 wanaume waliohitimu Cheti cha Uwakala wa Forodha cha Afrika Mashariki, Cheti cha Usimamizi wa Forodha na Kodi, Stashahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi na Stashahada ya Uzamili katika Kodi.

Alisema mwaka huu wamedahili wanafunzi 963 na kati yao 25 kutoka za China, Botswana, Malawi, Uganda na Sudan Kusini tofauti na mwaka jana walipodahili wanafunzi 706.

Alisema chuo hicho kinatarajia kutoa mafunzo kwa njia ya kisasa ya kutumia mtandao wa intaneti itakayowezesha wanafunzi wengi wa TRA na wadau wa masuala ya mapato kupata elimu.

Pia wanatarajia kujenga chumba cha kutolea mafunzo chenye uwezo wa kuingiza wanafunzi 300 kwa wakati mmoja pamoja na ujenzi wa hosteli itakayokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 100 jambo ambalo mkandarasi ameishapatikana.

Source Habari Leo
Imeandikwa na Merali Chawe, Mbeya na Theopista Nsanzugwanko, Dar
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger