RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea kukerwa na siasa chafu zinazofanyika Arusha ambazo zimeanza kuzorotesha uchumi wa mkoa huo na kutaka wananchi katika Wilaya ya Karatu wasiige mfano huo.
Alisema hayo alipokuwa akizindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Karatu katika Mkoa wa Arusha, mjini Karatu jana.
Aidha, aliwataka viongozi nchini kuacha kuwatumia wananchi kama chambo cha kufanikisha malengo yao ya kisiasa na kusababisha migororo na uvunjifu wa amani.
“Usalama ni jambo muhimu sana na kwa maana hiyo, nawaombeni msiige kabisa mfano wa Arusha, sote tunajua kimetokea nini kule kwa sababu ya fujo za kisiasa ambazo zinachochewa na viongozi na hasa Mbunge wa Arusha mjini, Bwana Lema (Godbless),” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mbunge anayo nafasi kubwa kujenga hoja zake ndani ya Bunge na ndani ya mikutano ya halmashauri. Lakini kwa Mbunge kuwachochea wananchi na kuwachukua na kuwatembeza barabarani ambako wanakumbana na virugu vya polisi siyo uongozi wa busara hata kidogo.”
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Lazaro Titus Massey amewaambia wananchi kuwa moja ya mwelekeo mkuu wa Chadema wilayani Karatu ni kushirikiana na Serikali na Polisi katika kudumisha amani.
“Tunawakaribisha Arusha waje kujifunza kwetu namna ya kudumisha amani. Tunamkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, John Mongella kuja kujifunza namna ya kurejesha na kudumisha amani mjini humo,” alisema.
Post a Comment