By Angela Semaya
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakijawasilisha taarifa zake za mapato na matumizi inayoonesha ilivyotumia fedha za ruzuku inayopewa na serikali kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama kilivyokuwa kimedai.
Katika taarifa yake Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyotoa jana kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), vyama vilivyowasilisha taarifa za hesabu zake kwa Msajili ni vinne.
Vyama hivyo ni Chama cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi(CCM), Chama cha Tanzania Labour (TLP) na NCCR-Mageuzi.
Awali katika taarifa yake Chadema ilidai kuwasilisha taarifa zake za fedha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12.
Chama hicho kilisema kina uthibitisho na barua ya Msajili wa vyama yenye kumb. Na CDA.112/123/01a/37 ya Septemba 4, 2012, iliyopelekwa kwa makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa.
Uthibitisho huo ulitolewa kukanusha taarifa ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, iliyosema kuwa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku kutoka serikalini havijawasilisha taarifa yake ya mapato na matumizi kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi na CAG, kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
Post a Comment