Home » » JK: Rushwa itaizika CCM

JK: Rushwa itaizika CCM

Written By JAK on Saturday, October 26, 2013 | 6:14 PM



RAIS Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema tatizo la rushwa ndani ya chama hicho lisipodhibitiwa litakiondoa chama hicho madarakani.

Amesema chama hicho kikishinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na tatizo la rushwa likaendelea, litakifanya chama hicho kutoshinda tena katika uchaguzi wa mwaka 2020.

“Tukiendelea hivyo, tukishinda uchaguzi ujao wa mwaka 2015 ni bahati, lakini tukifanikiwa kupenya uchaguzi wa mwaka 2020 hatutoki,” alisema.

Alisema hayo juzi mjini hapa wakati akifunga mafunzo maalumu ya watendaji wa wilaya na mikoa wa CCM na kumpa rungu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kuwashughulikia viongozi wala rushwa ndani ya chama hicho.

“Tusipoangalia hili la rushwa tutaiondoa madarakani CCM na mambo yote mazuri tuliyofanya hayataonekana, hapo lazima wananchi watawauliza je, ugonjwa huu mmeshindwa kuachana nao, basi tumeamua kuwapumzisha,” alisema.

Mwenyekiti wa chama hicho kilicho madarakani tangu Tanzania ipate uhuru, alisema rushwa itaizika CCM kwani hiyo ni hila ambayo itakifanya chama hicho kishindwe kuongoza kwa muda mrefu.

“Acheni kuvutavuta, mtu anarushiwa Sh 200,000 ya air time (muda wa maongezi wa simu ya mkononi) hiyo ni nini acheni hicho kitu,” alisema na kuongeza kuwa tatizo la rushwa limewachosha wananchi na kutishia chama kuendelea kuongoza.

Alisema wanaotoa fedha ndio wanapokewa kwa shangwe na viongozi hao ndio wamekuwa wakiwatafutia watu ushindi, kitu ambacho wananchi wamekichoka na kuwa na chuki na chama hicho.

“Nakupa Mangula (Phillip) rungu la kuhangaika nao,” alisema Rais Kiwete huku akishangiliwa na wajumbe hao wa mkutano.

Alisema dawa ya viongozi kama hao ni kuachana nao kwani kuna makada wengi ambao hawana makandokando lakini wale wenye maradhi hayo chama hakiwezi kuendelea nao.

“Njaa taabu sana, ukiendekeza sana njaa ndiyo inakuwa hivyo, utu unakutoka, tusifanye hivyo chuki ya watu kwa rushwa ni kubwa, kiongozi kuwa wakala wa kusambaza fedha ni aibu kama unatosha utapita tu,” alisema.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuweka sawa ng’we ya pili ya awamu ya nne ya serikali ya CCM na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ushindi ni hakika katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Alisema lengo kuu la CCM kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa ni kushika dola na CCM ipo kwa ajili ya kutawala lakini mtu akitoka kwenye lengo hilo akatafute shughuli nyingine ya kufanya sio hiyo kwani dhumuni kuu ni kushika dola.

Alisema pamoja na majukumu mengine ni lazima kuhakikisha wagombea wa CCM wanashinda na kuendelea kukamata dola na kama viongozi na watendaji wakuu ni kutambua na kuhakikisha chama kinakuwa na nguvu ya kutosha ili kufikia kwenye lengo kuu.

Aliyataja mambo matatu ambayo yakifanyika, CCM itakuwa na nguvu. Mambo hayo ni kuimarisha chama, tabia na mwenendo mzuri wa viongozi na wanachama na utendaji mzuri wa viongozi wa CCM.

Alisema wakifanya hayo chama kitakuwa na nguvu na kila mgombea watakayemweka atasubiri kuapishwa kwani kutakuwa hakuna wa kumpinga na hilo litawezekana iwapo chama kitakuwa na uhai kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya Mkoa hadi taifa.

Pia aliwataka kutunza wanachama waliopo ambao wataendelea kukaribisha wenzao ili chama kiwe na nguvu kwani wingi wa wanachama ni mtaji wa kutafuta ushindi.

“Ukiwa na wanachama milioni sita waaminifu hii itafanya mgombea wako kuwa na kura milioni sita za kuanzia, kazi yenu ni kuhakikisha tunashinda kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura,” alisema.

Aliwataka kuweka mikakati ya kutembelea wanachama katika maeneo yao ya uongozi ili watu wajue wenyewe wapo na kama viongozi wakiogopa kukutana na wanachama, chama hakitashinda.

“Badilikeni kama matawi yako huyajui mnataka uongozi tu na ingekuwa mnaitwa kwa usaili siku hiyo ingekuwa ni aibu maana mnaongoza watu msiowajua,” alisema.

Alisema vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya kazi hiyo kwani hata wakiomba barua kwa makamanda wa polisi ya orodha ya barua ya vyama vya siasa vilivyoomba kufanya mikutano, CCM haimo.

Alisema wapinzani wanazunguka ndiyo maana hata bendera ziko nyingi na wamekuwa wakizungumza na watu na wamekuwa wanafanya kazi ya kutembea ambayo CCM hawaifanyi.

“Mnasubiri wakati wa kampeni wakati watu wakiwa wamejazwa maneno mengi hata muda wa kujitetea unakuwa hakuna na matokeo yake chama kinashindwa kwenye uchaguzi,” alisema.

Pia alishutumu baadhi ya viongozi kutumia vibaya rasilimali za chama, ikiwemo kuuza viwanja na hata kupangisha kwa mikataba yenye utata.

Akitoa mfano alisema kuna mtu kapangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 kitu ambacho ni aibu kubwa. Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema jumla ya mada 19 zilitolewa katika maeneo yote muhimu ndani ya chama na nje ya chama.

Alisema mafunzo hayo yalihusu maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2014 na mwakani yatafanyika mafunzo kama hayo kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa( NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema mafunzo hayo maalumu yalihusisha wilaya 161 za Tanzania bara na Zanzibar ambapo wajumbe 426 walihudhuria kati ya wajumbe 443 waliotarajiwa ikiwa ni sawa na asilimia 96.2.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger