Na Kelvin Matandiko,
Gumzo wiki iliyopita lilikuwa ni juu ya mechi ya Simba na Yanga. Wiki hii inamalizika na gumzo la Tamasha la Fiesta ambalo linafikia tamati leo, baada ya kuzunguka katika mikoa 13 ya Tanzania kwa kipindi cha miezi miwili.
Gumzo wiki iliyopita lilikuwa ni juu ya mechi ya Simba na Yanga. Wiki hii inamalizika na gumzo la Tamasha la Fiesta ambalo linafikia tamati leo, baada ya kuzunguka katika mikoa 13 ya Tanzania kwa kipindi cha miezi miwili.
Leo katika Viwanja vya Leaders Club wasanii wanne wa kimataifa na wasanii 48 wa hapa nyumbani watawasha moto katika jukwaa moja.
Bodaboda, teksi, daladala leo hii zimejaza watu wakielekea katika Viwanja vya Leaders Club ambako hitimisho la Tamasha la Fiesta 2013 linafanyika. Ni siku ya neema kwani wasafirishaji lakini hata wenye kiingilio tu nao wanasonga ‘mdogo mdogo’ kuelekea eneo la tukio. Jukwanii wasanii kutoka Nigeria, Ghana, Jamaica, Norway watawasha moto wakisindikizwa na wasanii kutoka nyumbani.
Kinachotarajiwa siku ya leo ni burudani na neema kwa mashabiki, neema kwa wafanyabiashara wakiwemo wakaanga chipsi, wasafirishaji, wasanii wenyewe na vibaka ambao pia ukiwakalia vibaya lazima watakukwapua.
Watakaopamba jukwaa
Itakuwa hatari sana kwa jukwaa litakalokuwa limeandaliwa kwa ajili ya wasanii wanne wa kimataifa na 48 wa hapa bongo.
Jukwaa hilo litapambwa na wasanii wa kimataifa akiwamo Davido wa Nigeria, Iyanya kutoka Ghana, Alaine kutoka Jamaica na Mohombi wa Sweden watakaoonyesha uwezo wao katikati ya wasanii wakali wa nyumbani.
Kwa hapa Bongo vijana hatari watakaokuwepo ni pamoja na Ommy Dimpoz, Mwana FA na AY, Rich Mavoko, Makomando, Weusi, Lina, Shilole, Snura, Recho, Young Killer, Stamina, Country Boy, Godzilla, Cassim, Quick Rocka, Juma Nature, Ney wa Mitego, Madee, Nikki Mbishi, Kala Jeremiah na Linex.
Wengine ni pamoja na Chidi Benz, Shettah, H Baba, Samir, Darasa, Afande Sele, Baba Levo, Peter Msechu, Mabeste, Mirror, Menina, Walter, Nuhu, Cliff Mitindo, Blue, Young D, Dully, Amini, Christian Bella, TID, Kala Pina, Ney Lee, Fid Q, Ben Pol, Vanessa, Chege na Temba, Diamond na Gosby.
‘Kolabo’ kwa wasanii wetu
Kwa upande wa wasanii wetu hapa bongo tunatarajia kuona mafanikio makubwa baada ya kutengeneza uhusiano wa karibu na wasanii hao wa kimataifa kwa lengo la kukuza kazi zao.
Tunachotarajia kusikia ni ‘kolabo’ la Dully na msanii kutoka Jamaica, Alaine au Ben Pol akitengeneza traki na msanii kutoka Sweden, Mohombi, siku zijazo.
Tunachotarajia pia kama sehemu ya mabadiliko ni kuona wasanii wanapewa nafasi kubwa ya kuonyesha uwezo wao na kuthaminiwa kama ilivyo kwa wasanii wanaotoka katika mataifa hayo, ikiwemo kulipwa fedha nyingi.
‘Brazameni na Sista Du’
Kumbuka kuwa, tukio la leo linaweza kukufanya umsahau kila unayekutana naye kutokana na vipodozi au mavazi yakayovaliwa leo. Wakati huu wengi wako saluni huku wengine wakiranda kutoka duka moja kwenda jingine kutafuta cha kuvaa.
Mpaka dakika hii kila mmoja anajipanga na jinsi atakavyolipuka kwa namna yoyote ile ilimradi tu siku ya leo aweze kupendeza kuliko wenzake.
Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unatunisha mfuko wako ili uweze kufurahia vya kutosha na ukiwa na jamaa, ndugu, mshkaji, familia au mpenzi wako.
Kumbuka pamoja na starehe zote za leo, Ukimwi upo na unaua hivyo kila wakati jikumbushe ili siku moja ya leo isikuharibie ndoto zako.
Mbali na hatua hiyo, katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama inavyotarajiwa kwa leo, ni lazima kuwepo na makundi ya watu matapeli hivyo usidanganywe na mwonekano wa yeyote.
Wapo wale wanaopenda fujo, ukimkanyaga anarusha ngumi. Siku ya leo ni ya kistaarabu hivyo jiepushe na mtu anayeanzisha shari kwani huwezi jua ana silaha gani au anaweza kukudhuru.
Post a Comment