Home » » Rais Kikwete aongoza Mahafali WAMA Nakayama TANZANIA

Rais Kikwete aongoza Mahafali WAMA Nakayama TANZANIA

Written By JAK on Sunday, October 27, 2013 | 1:05 AM




Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimpa zawadi ya laptop Mwanafunzi Fadhila Hassan baada ya kuibuka mwanafunzi bora darasani wakati wa mahafali ya Kwanza ya Shule ya Sekondari WAMA Nakayama yaliyofanyika katika shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Nyamisati, Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani leo.Zaidi ya wanafunzi 60 walitunukiwa vyeti vya kumaliza kidato cha nne na zawadi mbalimbali wakati wa mahafali hiyo ambayo ilihudhuriwa pia na viongozi na watu mashuhuri akiwemo balozi wa Japan na wafanyabiashara ambapo mwenyekiti wa IPP Reginald Mengi aliahidi kuisadia shule hiyo shilingi milioni 200 kila mwaka kwa miaka mitano.Pembeni ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA Mama Salma Kikwete. Picha na Freddy Maro.
 


RAIS Jakaya Kikwete amewataka wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne, kuepuka mafataki na mabazazi wenye kuwadanganya na kuolewa mapema na kusababisha kutotimiza lengo lao la kupata elimu.

Alibainisha hayo wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama, iliyo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoendeshwa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete.

Aliwataka wajiepushe na shauku ya kuolewa mapema na kusema, “yapo majamaa mabazazi huko mitaani, dhamirieni kusoma hadi kufika chuo kikuu ili mzikabili changamoto mbalimbali”.

Rais Kikwete aliwataka wanafunzi hao, kuwa na malengo katika elimu ambayo yatawawezesha kuwa wajasiri na uthubutu na kusoma fani, ambazo wanawake sio wengi na ambazo pia zitawawezesha kuwa mabingwa.

“Msisahau mazingira mliyotoka na kubwa zaidi ni shabaha iliyowaleta ya kupata elimu,” alisisitiza Rais Kikwete katika mahafali hayo, ambayo wanafunzi 67 walihitimu.

Kuhusu kuwa na wataalamu mabingwa, Rais Kikwete aliwataka kudhamiria katika elimu kuwa mabingwa wa fani mbalimbali na kusimamia utajiri na rasilimali za nchi.

Akizungumzia kupata nafasi katika shule hiyo, alisema ni kutokana na msaada kutoka kwa halmashauri mbalimbali kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Shule hiyo hutoa elimu bure kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Shule ya Wama Nakayama iko katika kata ya Sarai kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji na ina wanafunzi 332.

Kwa upande wake, Mama Salma Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Wama, alisema alianzisha shule hiyo ikiwa ni juhudi za kumkomboa mtoto wa kike.

Alisema watoto wengi yatima na maskini, hukosa elimu na kwamba hata alipokuwa mwalimu, alishuhudia changamoto zinazowakabili. Aliwapongeza wanafunzi waliopata fursa ya kusoma shuleni hapo na kutakiwa kuzingatia masomo zaidi na kufaulu katika mtihani wa kumaliza kidato cha nne, utakaoanza Novemba 4, mwaka huu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Suma Mensah alisema shule hiyo iliyoanza mwaka 2010 ni shule pekee inayopokea watoto wenye matatizo ya aina hiyo, ambao walifaulu na kukosa uwezo wa kuendelea na elimu na hupata ufadhili wa asilimia 100.

Alisema shule hiyo ina mkakati wa kuanzisha kidato cha tano na sita kuanzia mwakani.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger