Home » » Kigogo Chadema asimamishwa - TANZANIA

Kigogo Chadema asimamishwa - TANZANIA

Written By JAK on Sunday, October 27, 2013 | 12:48 AM


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha, Samson Mwigamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana.

Amesimamishwa kwa tuhuma ya kutumia vibaya mtandao wa kijamii wa Jamiiforums. Anatuhumiwa kutumia mtandao huo, kuleta uchonganishi kwa viongozi wa chama hicho.

Pia, uongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini, ulimfikisha polisi Mwigamba kwa tuhuma ya kutumia mtandao wa kijamii, kukichafua chama na viongozi wake.

Uamuzi huo ulichukuliwa juzi jijini hapa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu. Natse alisema wakati Mwigamba amesimamishwa, chama kitaendelea na uchunguzi dhidi yake.

Alisema Mwigamba alisimamishwa juzi jioni baada ya kikao cha Baraza la Uongozi Kanda ya Kaskazini, akituhumiwa kutuma kwenye Jamiiforums taarifa za kuwatuhumu viongozi wa juu wa chama, kuwa wamechakachua katiba ya chama chao.

Katika taarifa hiyo inayopatikana kwenye mtandao huo, inayosema ‘Kwa nini mabadiliko ya Chadema ni lazima’, Mwigamba anaelezea kuwa nafasi za uongozi kwenye chama hicho zinatolewa kwa upendeleo, kauli ambayo chama hicho kimesema ni za uzushi na uchonganishi.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema watamkabidhi Mwigamba barua ya kusimamishwa na baada ya hapo chama kitaamua kichukue hatua gani dhidi yake.

Lakini, alisema juzi (jana) walimpeleka Mwigamba polisi kwa usalama wake, kwa sababu hilo linahusu chama; na Chadema ni taasisi.

Akizungumzia hali ilivyokuwa wakati wa kikao chao, Golugwa alisema wakati wakiendelea, Mwigamba alitoa mada kuhusu ‘Hali ya Uhai wa Chama katika Mkoa wake’, ambapo aliwapongeza viongozi wakuu wa chama hicho.

‘’Sisi tunashangaa tulipokuwa ndani ya mkutano, wakati kikao kinaendelea, tunaona mambo hayo yapo kwenye mtandao, hapo ndipo vijana wa IT (Teknolojia ya Habari) walipoanza kufuatilia suala hilo na kumbaini Mwigamba ndiye anahusika,”alisema.

Alisema, awali Mwigamba alibisha, kwa kutoa maneno ya vitisho na kumtishia Mbunge wa Arusha, Godbless Lema kwa maneno ya uchonganishi.

Pamoja na mambo mengine, Mwigamba anadaiwa kutoa taarifa za kuwashutumu Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na maofisa wengine wa chama kuwa wanatumia fedha nyingi, kuzunguka na kufanya vitu ambavyo havieleweki.

“Siamini kama mtu wangu wa karibu, ambaye nimefanya naye kazi kwa muda mrefu, anaweza kurusha mambo ambayo yanaleta migongano ndani ya chama, baada ya kumbaini, ilinishtua sana na tulimwonea huruma kwa sababu hata yeye mwenyewe alionesha kusikitika,’’alisema na kuongeza: “Mwigamba alikuwa mtu mwenye sifa nzuri ndani ya chama na alikuwa anapambana hasa, lakini tunaamini amedanganywa na watu ambao hawaitakii mema nchi”.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema kosa analotuhumiwa nalo, linaangukia kwenye Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa kutumia vibaya mitandao, hivyo polisi wanatakiwa kuangalia sheria inasemaje kuhusu suala kama hilo na wamchukulie hatua.

Mwigamba alikuwa pia Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa, Mjumbe kwa Baraza la Uongozi la Kanda na Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alikataa kuzungumzia suala hilo. Kwa upande wake, Mwigamba alipopigiwa simu yake ya mkononi, iliita na baadaye kuzimwa.
By Veronica Mheta, Arusha
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger