Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
ameagiza kukabidhiwa mara moja kwa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma nyumba zote 13
zilizoko katika kambi iliyokuwa ikitumiwa na Wahandisi waliosimamia ujenzi wa
barabara ya Mwandiga hadi Manyovu ambayo ujenzi wake umekamilika kwa kiwango
cha lami.
Hatua hiyo ya Waziri
Magufuli imetokana na nyumba hizo kuachwa bila ya matumizi yoyote kwa muda wa
miaka miwili.
Akimhoji Meneja wa Wakala wa Majengo wa mkoa wa Kigoma
sababu za kuachwa kwa nyumba hizo kwa kipindi chote hicho wakati yapo mahitaji
makubwa ya nyumba kwa ajili ya Watumishi wa Umma na Ofisi za Serikali, Meneja
wa TBA wa mkoa huo Eng. Mashaka Mgallah alibainisha kuwa awali Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA) uliarifiwa kuwa majengo hayo yamekabidhiwa kwa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma.
Katika hali ya
kusikitisha wakati Mheshimiwa Magufuli alipofanya ukaguzi wa kushitukiza katika
eneo hilo alikuta nyumba hizo zikiwa zimetelekezwa huku vifaa vingi vikiwa
vimeibwa vikiwemo viyoyozi na samani mbali mbali. Kutokana na hali hiyo
yakatolewa maelekezo kwa taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi
kutekeleza zoezi maalum la kuhakiki mali zote zilizo katika miradi inayoendelea
ili zithaminiwe mara miradi hiyo inapokamilika tayari kwa kukabidhiwa
Serikalini.
“Ninawaagiza hasa Watendaji Wakuu wa Tanroads, TBA na TEMESA
na Taasisis nyingine katika Wizara ya Ujenzi mfanye ukaguzi wa mali zilizo
katika kila mradi unaoendelea nchi nzima ili pale mradi unapokamilika ifanyike
tathmini ya mali zinazokabidhiwa Serikalini” alisitiza Waziri Magufuli.
Naye Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kigoma ACP Frasser Kashai
kwa upande wake ameshukuru Waziri wa Ujenzi kwa uamuzi huo ambao ameuelezea
kutolewa katika wakati muafaka hasa kutokana na kuwepo kwa tatizo kubwa la
makazi kwa ajili ya askari wa jeshi hilo sio tu katika mji wa Kigoma bali
katika mkoa mzima kwa ujumla wake.
“Nyumba hizo mnapewa
bila ya malipo yoyote kwa ajili ya matumizi ya jeshi la polisi hadi hapo
taarifa nyingine itakapotolewa, TBA na Tanroads wahakikishe kuwa huduma za maji
na umeme zimeunganishwa katika eneo hilo” alimalizia Waziri Magufuli.
Waziri wa Ujenzi (katikati) akiongozana na Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga (kulia) na Eng. Mashaka Mgallah
ambaye ni Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Kigoma, kukagua
eneo lililokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya Mwandiga – Manyovu mkoani
Kigoma. Nyumba hizo zimetelekezwa kwa miaka 2. Wengine katika picha ni
Watendaji kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali.
Moja ya nyumba zilizotelekezwa katika kambi ya ujenzi wa
barabara ya Mwandiga – Manyovu.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipata
maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Eng.Mashaka
Mgallah (wa pili kulia) wakati alipofanya ziara ya ghafla kukagua
nyumba katika kambi iliyokuwa ikitumiwa na Wahandisi wakati
wa ujenzi wabarabara ya Mwandiga – Manyovu mkoani Kigoma.
Post a Comment