BAADA ya kulazwa katika hospitali ya Milpark iliyoko jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwa siku saba, mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi, amefariki dunia. Taarifa za Mhadhiri huyo Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo, kufariki dunia zilianza kusambaa jana alasiri katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, ilipofika saa 11 jioni, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, chama ambacho Dk Mvungi alikuwa si tu mwanachama bali kiongozi, James Mbatia, alilithibitishia gazeti hili juu ya kifo hicho alipopigiwa simu.
“Najua mnachotaka kuuliza…amefariki dunia saa 9.30 alasiri hii, hapa nipo na familia yake ndio tunatafuta jinsi ya kuiambia kwani haijajua mpaka sasa,” alisema Mbatia kwa masikitiko ambayo yalidhihirika wazi hata katika sauti yake kwenye simu.
Kwa kifo hicho washukiwa wa shambulio dhidi yake ambao bila shaka wangefikishwa mahakamani wangeshitakiwa kwa tuhuma za shambulio na kujeruhi, hivi sasa watakuwa wakikabiliwa na tuhuma za mauaji.
Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Polisi inashikilia watu tisa kwa tuhuma za kuvamia nyumbani na kumjeruhi Dk Mvungi ambao baadhi yao walikutwa na simu iliyoporwa na mapanga yanayodaiwa kutumika katika shambulizi hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Suleiman Kova, alitaja waliokamatwa kuwa ni Msigwa Mpopera ambaye ni mlinzi nyumbani kwa Dk Mvungi ambaye kwa mujibu wa Kova ndiye alikuwa kiongozi wa tukio hilo na aliongoza wenzake kufanya shambulio hilo.
Mwingine ni Chibango Magozi ambaye alikamatwa akiwa na simu iliyoibwa nyumbani kwa Dk Mvungi, Ahmed Ali, Zakaria Msesa, Manda Saluwa, Paul Jailos na Juma Khamis ambao wote ni wakazi wa Vingunguti; Longishu Semariki mwuza tumbaku (ugoro) katika eneo la Msimbazi na Msunga Makenza dereva wa bodaboda Kitunda.
Kuvamiwa Dk Mvungi alivamiwa saa 6.30 usiku wa kuamkia Jumapili Novemba 3, nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Uvamizi huo ulifanywa na watu sita wanaodaiwa kuwa vibaka ambao baada ya kufanikiwa kuingia ndani, walimlazimisha mfanyakazi wake aeleze aliko Dk Mvungi.
Akisimulia ilivyokuwa, Mbatia alisema baada ya kumlazimisha mfanyakazi huyo kwa kumpiga, alilazimika kuongozana nao na kuwapeleka chumba alimokuwa amelala Dk Mvungi.
Kati ya vibaka hao, inadaiwa wanne ndio walioongozana na mfanyakazi huyo na wawili kubaki nje na kabla ya kufika katika chumba cha Dk Mvungi, waliobaki nje walilipua baruti.
Mlio wa baruti hiyo ulimshitua Dk Mvungi, aliyekuwa amelala na inaelezwa alitoka chumbani na kukutana na watu wanne waliomkata panga utosini.
Shambulio hilo la ghafla lililamfanya Dk Mvungi kuangukia paji la uso sakafuni na kutokwa na damu puani na masikioni. Kudai fedha Kwa mujibu wa Mbatia, baada ya tukio hilo, watu hao waliingia chumbani na kumtaka mke wa Dk Mvungi atoe fedha vinginevyo wamuue.
Mbatia alifafanua, kuwa mke wa Dk Mvungi, aliwapa kiasi fulani cha fedha lakini hawakuridhika na kupekua kabatini ambako walichukua kompyuta mpakato moja (laptop) na bastola.
Alisema dereva wa Dk Mvungi alipiga simu kwa majirani kuomba msaada ambao walifika na kumpeleka hospitali ya Tumbi, Kibaha na kupatiwa huduma ya kwanza ambako alishonwa nyuzi nne.
Mtoto wa kaka yake Dk Mvungi, Deogratius Mwarabu, alisema baada ya kupewa huduma ya kwanza Tumbi, alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili saa 10 alfajiri kufanyiwa kipimo cha CT-Scan.
Saa 4:15 asubuhi, Dk. Mvungi alitolewa Muhimbili na kupelekwa hospitali ya Aga Khan kufanyiwa kipimo hicho. Kwa mujibu Mwarabu, baada ya uchunguzi huo, alirudishwa Taasisi ya Mifupa (Moi), saa 5:15 asubuhi ambako alilazwa katika Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) na wakati huo hali yake haikuwa nzuri kwa kuwa damu zilikuwa zikitoka puani na masikioni.
Kuhamishiwa Afrika Kusini Baada ya kupata taarifa za matumaini ya maendeleo mazuri ya Dk Mvungi, ingawa alikuwa hajazinduka, Jumatano Novemba 6, alisafirishwa kwenda Afrkka Kusini katika hospitali ya Milpark kwa matibabu zaidi.
Kuhamishiwa katika hospitali hiyo, kulitokana na ushauri wa madaktari kwa ajili ya matibabu zaidi, kutokana na kuendelea kuwa katika hali ya kutojitambua tangu Novemba 3 alipojeruhiwa.
Mwarabu alisafiri naye kwenda Afrika Kusini ambaye alithibitisha kuwa uamuzi wa kumhamishia Milpark, ulitokana na ushauri wa madakari wa Moi ambao walikuwa wakimhudumia tangu alipofikishwa hapo kutoka Tumbi.
Dk Mvungi aliondoka nchini kwa ndege ya kukodi ya kampuni ya Flightlink namba 5H-ETG 560, ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubeba wagonjwa.

Post a Comment