ALIYOITOA BUNGENI KUHUSU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, 7 NOVEMBA, 2013, DODOMA
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze
kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai,
ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa
kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge,
kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo
waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa
matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo
waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa
nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia
waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika
Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo si
makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya
Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa
Tanzania katika Jumuiya hiyo. Lakini,
kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa
niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema
nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa
Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji
wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya
wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia
walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya
Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi
wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe
15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande
wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu
yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya
Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo
itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili
ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na
wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa
tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika
Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge
Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa
Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo
kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni
kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao
umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati,
tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani
350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili
uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980
ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha
Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa ni marehemu)
kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa
Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka
(CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu
nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu
katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu
katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009
kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na
kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na
yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli
huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na
Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu
vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa
zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa.
Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu
vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama
nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru
lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo
zinakabiliwa na matatizo kama yetu.
Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka
na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili.
Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi
zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua
hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na
wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli
ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni
Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na
kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia
itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia
maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa
tutayafanyia kazi. Serikali imeahirisha
kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga
upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na
wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa.
Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza
upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa
mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye
mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na
mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa
taarifa zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua
zipasazo. Pamoja na hayo, napenda
kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori
hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na
kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za
nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe
ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna
adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo
tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge
hili. Pale wanapotenda visivyo tuseme,
watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka
huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha
wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya
kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo
kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka
kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali,
kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo
yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu
wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena
kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu.
Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa
Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO)
na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya
Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili. Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani
tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi
majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami
tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu
hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba
unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo
hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani
ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka
ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni
lazima kufanya hivyo. Maana yake ni
kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi
vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao
wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya
kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na
kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa
pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi
kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu
yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya
tumepoteza vijana wetu watatu shupavu.
Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko
mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii
kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio
ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la
heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga
mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo.
Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa
kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini,
Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa
JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama
nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja
kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu.
Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio
nao. Jambo lililonileta hapa leo ni
kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya
Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona
nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia
matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa
viongozi wa Tanzania na Burundi.
Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25
Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya;
na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba
kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi
kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna
hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya
hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba
hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao
au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia.
Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya
yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari kutekeleza
ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu
wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna
mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo
la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka
Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi
wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3)
Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kutekeleza vipengele vyote;
(5)
Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya
kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya
Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist
Visa);
(7)
Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya
kusafiria katika nchi zao; na
(8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri
kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo
ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati
ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au
kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na
akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na
kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali
kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta
nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya
bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau
wengine. Rais Yoweri Museveni alituarifu
mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na
nyumbani. Alitualika kushiriki katika
ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi
Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo
linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili
kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko.
Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta
kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia
upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi
wa bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa –
Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo
hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama
husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua
ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini
kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha
juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu.
Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African
Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake Victoria
Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi
Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania
kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea
hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini
Tanzania ni mdau muhimu. Lakini
inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya
kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi.
Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24,
2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa
Afrika Mashariki kwa kubaguana,
Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo
manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji
na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya
taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa
pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya
Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika
Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika
Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili,
2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja
ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi
mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama
ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa
zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa
mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika
baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la
Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji
wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi
inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala,
Uganda tarehe 30 Novemba, 2013. Iweje
leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu
Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya
Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa
14 wa Wakuu wa Nchi wanachama
uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua
iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano huo uliagiza nchi wanachama
kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango
wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri
litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa
Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo
wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa
najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na
viongozi wenzangu watatu na kwa nini!
Nakosa majibu ya uhakika. Je
wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda
yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo
wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au
sijui wanachuki na mimi! Napenda
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana
wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na
tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania
haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu,
mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya.
Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu
katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo
yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine
hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari
tutajiunga. Yaani wana Umoja wa
Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing).
Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?) Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya
kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi
wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari.
Madai hayo hayana ukweli. Ni
vyema waseme ukweli. Kama walitualika
tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba
Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu
imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania
tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika
Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au
kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na
hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo
hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata
sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na
Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini
wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha
nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika
na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee
uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni
mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza
Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao
na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo
ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa
sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha
juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama
kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha,
kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza
kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza
na wala hayaingii akilini. Ama kweli
akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo
mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira,
uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi siamini kama kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba
kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu
wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa
tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge
Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna
tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo
yote. Tusiende kasi ya kupindukia.
Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha
Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni kweli
kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha
baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa
nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi huo si mwingine bali utengamano wa
kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha
zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama wote
sawia.
Mheshimiwa Spika;
Lazima
tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi
kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na
kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa
kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu
za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki
ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa
mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni
kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe
moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja.
Kwa msimamo na mtazamo wetu,
Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho.
Na huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa
Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka
2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na
Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake,
Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo
kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa
kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi
zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na
kasi ya utekelezaji wake. Watanzania
wengi sana wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini
wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka.
Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama
ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na
msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na
ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana
tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa
Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya
kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa
Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya
kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu
ya namna ya kufanya hivyo. Kamati
ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali
katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande
wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za
Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki
kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua.
Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato
wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka
mitano. Baada ya hapo muda wa
kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya
kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika
mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza
matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda
Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa
mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa
nchi wanachama wataamua kwa kura.
Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama
tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya
kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa
Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano
kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua
wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki
zake. Kwa kweli kama mwenendo huu
hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu.
Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote
wanachama na watu wake wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato
wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla
hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa
makini katika kila hatua tunayochukua.
Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya
yetu itakuwa imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa
na changamoto nyingi. Hatupendi ya mwaka
1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa
ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa
Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo
itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala
kichocheo chake. Ndiyo maana,
hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo
yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa.
Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba
ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za
Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na
watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment