ALIYEKUWA
Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, amesema wanachama wa CCM na wananchi wamepata
matumaini mapya, kwa kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ya kutaka
watoa rushwa ndani ya chama hicho washughulikiwe.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, Sumaye alisema kauli ya Rais Kikwete
dhidi ya rushwa ndani ya CCM haitapotea hewani; bali itatekelezwa na italeta
mabadiliko makubwa katika vita dhidi ya rushwa nchini na ndani ya chama hicho
ambako alidai rushwa ni tatizo sugu.
“Mwenyekiti
wangu nakupongeza sana sana kwa kukemea rushwa na ninakuunga mkono katika vita
hii na ninaamini unajua kuwa mimi ni askari wako mmojawapo wa mstari wa mbele
kupambana na tatizo hilo,” alisema Sumaye.
Sumaye
alisema kwa vile Mwenyekiti amekabidhi jukumu la utekelezaji kwa Makamu wake wa
Bara, Phillip Mangula, ambaye anajulikana kwa ujemedari imara katika vita dhidi
ya rushwa, ni imani ya wanachama kwamba hatalionea haya suala hilo.
“Tunaamini
kuwa Mangula hutaangalia sura ya mhusika wakati wa kuchukua hatua, maana ni
kweli usiofichika wengi wa watoa rushwa ni watu wazito kwa kila namna,” alisema
na kuongeza kuwa Sekretarieti na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,
wanapaswa kumpa Mangula ushirikiano usioyumba wakati wa kutatua tatizo hilo la
rushwa ndani ya CCM.
Kwingine
Lakini licha ya pongezi hizo kwa Rais Kikwete, Sumaye pia alihadharisha kuwa
rushwa haiko ndani ya CCM peke yake, bali iko katika vyama vingine vya siasa,
katika taasisi zinazojitegemea, serikalini na maeneo mengine mengi nchini.
“Kama
Mwenyekiti alivyomwagiza Makamu wake kushughulikia rushwa CCM, namwomba
Mwenyekiti asikomee hapo, bali aendelee kushughulikia rushwa katika Serikali na
vyombo vyote vilivyoko chini ya Serikali,” alisema Sumaye.
Aliongeza
kuwa katika vita ya rushwa, nchi itashinda iwapo askari wote watashikamana na
kuunganisha nguvu pamoja.
“Ni
vita kali, kubwa na ya hatari, lakini tukiwa pamoja tutashinda kwa uhakika.
Alipoulizwa maoni yake kuwa iwapo watoa rushwa hao wakiteuliwa kupeperusha
bendera ya chama chake katika uchaguzi matokeo yake yatakuwaje? Sumaye alisema
iwapo chama kitapitisha majina ya watoa rushwa kwa kufumbia macho suala hilo,
ni wazi kitaanguka.
“Siamini
kama watapitisha watoa rushwa wanaonunua watu wengine, CCM itaepuka hilo, ila
wakifumbia macho wajue tutaanguka katika uchaguzi kwani wananchi wamechoshwa na
kelele za rushwa,” alisisitiza Sumaye.
Alisema
anaamini watoa rushwa hawatapitishwa, kwani kati ya viongozi wa juu wa CCM,
hakuna anayetaka chama kianguke katika uchaguzi mkuu ujao.
Alitishia
kuwa iwapo watoa rushwa watapitishwa, hatathubutu kukaa nao, maana ni waovu
ambao wananunua watu wapate madaraka. Sumaye alisema wana CCM wote wanapaswa
kusema rushwa ni adui wa haki, kwani unapompa mtu rushwa ujue kuna
anayedhulumika na kuumia na hiyo rushwa iliyotolewa.
Alisema
rushwa inahamisha uhalali kwa anayestahili na kupewa asiyestahili na katika
mchakato huo, mtoa rushwa anatenda dhambi ya kudhulumu haki kwa anayestahili.
"Unapofanya
ufisadi kwa mradi wa Serikali, unaumiza Taifa katika siku zijazo kwa kuruhusu
kiharusi cha uchumi na huduma kwa jamii," alisema Sumaye ambaye pia jana
alitumia mkutano wake kuelezea mchezo mchafu unaofanywa na wanasiasa wenzake
katika kuchafuana katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu 2015.
Jumuiya
Akizungumzia suala la Tanzania kutengwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), Sumaye alisema itakuwa ni makosa makubwa iwapo Tanzania itaamua
kujiondoa. Alisema Jumuiya ya sasa wakati inaundwa, ilishirikisha wananchi
katika hatua zote kabla ya viongozi wakuu wa nchi tatu kusaini makubaliano.
Alikumbusha,
kuwa duniani kote nchi zinafirikia kuungana, ili kujiongeza nguvu, hivyo suala
la Tanzania kuondoka kwenye Jumuiya hiyo yeye halishabikii hata kidogo. Alihoji
wanaoangalia uwezekano wa kuunda ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo
(DRC), wajiulize kuwa nchi hiyo tangu ipate uhuru ni lini imekuwa na amani.
“Hivi
sisi ndio mwarobaini wa kutuliza vurugu za DRC, nani kasema hawa majirani zetu
si muhimu kwa sasa?” Alihoji Sumaye. Alisema kama suala ni ardhi, si dhambi kwa
Wakenya kuimiliki, wakati ameshuhudia Kilosa kuna maeneo makubwa na
wamemilikishwa Wachina.
“Kwa
nini ni haramu kwa Wakenya? Nenda Arusha, ardhi yote imechukuliwa na wageni, na
si kwa sababu ya EAC, iweje leo tuogope?” Waziri Mkuu huyo mstaafu, alisema huu
si muda wa kuangalia nyuma, bali kusonga mbele kwa kuimarisha uchumi ikiwa ni
pamoja na kuboresha bandari na reli.
Alisema
bahati mbaya bandari hazifanyi kazi kwa ufanisi mkubwa, lakini kama Serikali
itajipanga kuboresha bandari za Tanga, Mtwara na Dar es Salaam, uchumi wa nchi
utaimarika zaidi. Alisema nchi ambazo hazina bahari, ndizo zitakazoifanya
Tanzania isonge mbele kiuchumi kwa kutumia bandari zake kupitisha mizigo yao.
Alisema
hoja hiyo inayoibuliwa sasa, inamuuma sana kwani walihangaika kuanzisha Jumuiya
hiyo kwa kushirikisha wananchi na akahoji; “Iweje leo tuivunje miaka michache
tu baada ya kuundwa? “Samahani kwa hili sikubaliani na msimamo wa kujiondoa,
eti sisi ndio tutatoa talaka, nchi zote hizi ziko sawa hakuna wa kutalikiwa
wala wa kutoa talaka,” alisema.
Hivi
karibuni Wabunge waliitaka Serikali ijiondoe EAC kwa maelezo kuwa inatengwa na
viongozi wa nchi za Kenya, Rwanda na Uganda.
Hata
hivyo, Waziri Sitta alisema wakati ukifika, watatoa tamko na Tanzania ndio nchi
kubwa hivyo kama ni talaka ndiyo itakayotoa kwa nchi hizo akipinga kauli ya
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye
alitaka Tanzania ipewe talaka. Pia kumekuwa na taarifa kuwa Tanzania inaangalia
uwezekano wa kuunda Jumuiya nyingine na nchi za DRC na Burundi.
Post a Comment