By Mwandishi Maalumu, Warsaw, Poland (Habari Leo)
RAIS Jakaya Kikwete amesema wajibu mkuu wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi badala ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kuishi kwa Watanzania nje ya nchi kutaonekana jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa wanazozipata ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao waliobakia Tanzania.
Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya wenyewe kwa kuiga tamaduni za kigeni kupita kiasi.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipozungumza na Watanzania waishio nchini Poland usiku wa Alhamisi wiki hii kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne katika Poland. Aliwaambia Watanzania hao na familia zao:
“Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea vizuri nchi yetu, mtaitetea nchi yenu, mtaihangaikia nchi na kuleta faida nyumbani. Ni jambo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi yenu wenyewe. Nchi mbaya, viongozi hawafai...mnapata faida gani. Mnazo nchi ngapi?” Aliongeza:
“Kuhangaikia nchi yetu ni wajibu wenu ambao hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba mtasukuma mbele maslahi ya nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui. Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”
Aidha, Rais Kikwete alisisitiza:
“Mbona kazi za ma-Ngos mnazifanya vizuri bila kusukumwa ama kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi? Kama hata hamwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?” Rais alisema kuwa, kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na kutetea nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa kuanzishwa kwa uraia wa nchi mbili ambao Watanzania waishio nje wanaulilia.
“Mnaweza kuhalalisha hoja ya uraia pacha kwa kuwa watu wenye faida kwa nchi.”
Kuhusu ombi lao la uraia wa nchi mbili, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Watanzania waishio nje kuongeza kasi ya kuchangia mjadala kuhusu suala hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye Katiba Mpya.
“Rasimu ya kwanza ya Katiba ililikataa jambo hilo kwa sababu hili ni jambo lisilokuwa na ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu kwenu ni jipangeni vizuri kutetea hoja yenu hii. Saidieni mjadala wa jambo hilo badala ya kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na hivyo kusahau yenye maslahi kwenu.”
Kuhusu kuiga tamaduni za nchi nyingine na kusahau za nyumbani, Rais Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea kuwa baadhi wachache wanaoishi nje ya nchi, wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya kwao. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa suala zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni kuwauza watoto wa kike. Rais ambaye alionesha kushangazwa na kauli hiyo, alijibu:
“Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”
Post a Comment