Home » » Maalim seif afungua mkutano wa Kimataifa wa wapatanishi wa migogoro wa nchi za Afrika

Maalim seif afungua mkutano wa Kimataifa wa wapatanishi wa migogoro wa nchi za Afrika

Written By JAK on Wednesday, November 20, 2013 | 8:45 AM


Na Hassan Hamad wa OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema nchi za Afrika zinaweza kujifunza usuluhishi wa migogoro kupitia maridhiano yaliyofiwa Zanzibar na kupelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 
Amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizokumbwa na migogoro ya kisiasa kwa kipindi kirefu, lakini baada ya viongozi wazalendo kukaa pamoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, suluhu ya maridhiano ilipatikana, na kwamba matunda ya umoja huo yanaendelea kuistawisha Zanzibar kijamii na kiuchumi. 
Akifungua mkutano wa Kimataifa wa wapatanishi wa migogoro kutoka nchi za Afrika unaofanyika hoteli ya MELIA Zanzibar, Maalim Seif amesema migogoro ya Afrika itatatuliwa na Waafrika wenyewe. Amefafanua kuwa hii haina maana ya kuzitenga nchi na Jumuiya za Kimataifa kusaidia kusuluhisha migogoro ya Afrika, lakini msingi mkubwa wa utatuzi wa migogoro hiyo uko kwa nchi husika. 
Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili vyanzo vya migogoro inayozikabili nchi za Afrika, ili kuweza kutambua kwa urahisi njia muafaka za kusuluhisha migogoro hiyo. 
Amewashukuru waandaaji wa mkutano huo kwa kuamua kuufanya tena Zanzibar kwa mara ya nne, hali ambayo inadhihirisha mazingira bora na salama ya kufanyika mikutano ya Kimataifa. Ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za usuluhishi wa migogoro zinazochukuliwa barani Afrika, ili kuliwezesha bara hilo na sehemu nyengine duniani kuwa katika hali ya amani, utulivu na usalama. 
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt. Salim Ahmed Salim amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imekuja baada ya mgogoro wa muda mrefu, na kwamba ni mafanikio ya kujivunia kwa bara zima la Afrika. 
Nae Mkurugenzi wa kituo cha misaada ya kibinadamu chenye makao makuu yake Mjini Geneva Dr. David Harland amesema mkutano huo utajadili mambo mbali mbali yakiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya, utawala wa sheria, haki za binadamu, demokrasia na utawala bora. 
Amesema matatizo mengi ya Afrika yatapatiwa ufumbuzi kutokana na juhudi za Waafrika wenyewe kuweza kusimamia usuluhishi wa matatizo yanayowakabili. 
Mkutano huo unawashirikisha wapatanishi waandamizi wa migogoro kutoka nchi za Afrika akiwemo Mwenykiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt. Salim Ahmed Salim.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dr. Salim Ahmed Salim (kushoto), pamoja na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa wapatanishi wa Afrika huko hoteli ya MELIA Mkoa wa Kaskazini Unguja
 Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dr. Salim Ahmed Salim, akitoa hotuba ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Maalim Seif kufungua mkutano huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wapatanishi wa Afrika huko hoteli ya MELIA Mkoa wa Kaskazini Unguja. 
Picha na Salmin Said wa OMKR


Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger