Rais Jakaya Kikwete (wa pili kushoto) akiwa na mkewe Mama
Salma pamoja na Mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi James Mbatia, na daktari
wa zamu wakimwangalia mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, Dk Sengondo
Mvungi, aliyelazwa katika taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI) jana, baada ya
kujeruhiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi. Picha na Ikulu
Kwa ufupi
Dk Mvungi, ambaye pia
ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi aliwahishwa
kwenye Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Muhimbili (MOI), ambako amelazwa katika
wodi maalumu huku hali yake ikiwa mbaya.
Dar es Salaam. Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
nchini, Dk Sengondo Mvungi amejeruhiwa usiku wa kuamkia jana, baada ya kukatwa
kwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake Mpiji-Magohe,
jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na
Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi aliwahishwa kwenye Taasisi ya Mifupa Hospitali
ya Muhimbili (MOI), ambako amelazwa katika wodi maalumu huku hali yake ikiwa
mbaya.
Taarifa kutoka kwa ndugu na watu waliomtembelea hospitalini
hapo wanasema kwamba hali ya Dk Mvungi ni mbaya kwani alikuwa hawezi hata
kuzungumza.
Akisimulia tukio hilo, dereva wa Dk Mvungi anayeitwa
Emmanuel Ntaro, alisema akiwa nyumbani kwake majira ya saa 6:30 usiku, alisikia
mlipuko mkubwa kisha zikasikika kelele zikitokea nyumbani kwa bosi wake.
“Nilifika na kukuta hajitambui, tukampeleka Hospitali ya
Tumbi Kibaha mkoani Pwani alikopatiwa huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka MOI
ambako anaendelea kuchunguzwa na kupatiwa matibabu,” alieleza Ntaro
Alisema kuwa watu wapatao sita, walivamia nyumbani kwa Dk
Mvungi ambako baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani, walimjeruhi kwa kutumia
mapanga huku wakidai wapatiwe fedha. Watu hao walimsababishia majeraha usoni,
kichwani na sehemu nyingine za mwili.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia alisema mbali na kupata matibabu MOI, pia walilazimika kumpeleka
Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya vipimo zaidi katika mashine ya CT Scan kama
walivyoshauriwa na madaktari wa zamu.
Mbatia alisema kuwa baada ya Dk Mvungi kufanyiwa kipimo
hicho alirudishwa tena MOI kwa matibabu na uangalizi maalumu. “Hali yake
inaanza kuimarika tofauti na nilivyomuona saa nne asubuhi, “ alisema Mbatia
muda wa saa 12 jioni jana alipozungumza na gazeti hili.
Alisema kwamba pia watu waliohusika na tukio hilo waliiba
kompyuta mpakato (laptop) pamoja na bastola ya Dk Mvungi.
Kamanda wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Cammilius Wambura
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kweli hilo ni tukio la kihalifu na sisi tunaendelea
kulifanyia kazi. Tunawahakikishia Watanzania kuwa watu hao watapatikana na
kufikishwa kwenye mkono wa kisheria,” alisema.
Kilichotokea
Akisimulia tukio hilo, mtoto wa Dk Mvungi anayeitwa
Deogratius Mwarabu, alisema kuwa walipigiwa simu na mdogo wao saa 7.00 usiku wa
kuamkia jana na aliwaeleza kuwa baba yao alikuwa amevamiwa na watu wanaodhaniwa
kuwa majambazi.
Mwarabu alisema watu wapatao sita walivamia katika nyumba ya
Dk Mvungi na kwenda chumba cha nje cha nyumba hiyo anachoishi fundi wa nyumba
hiyo.
Watu wanne ndio walikwenda katika chumba hicho na kumpiga na
nondo mfanyakazi huyo na kumlazimisha awaonyeshe chumba cha Dk Mvungi. Mwarabu
alisema baada ya kumpiga walimfunga kamba mfanyakazi huyo kisha kwenda kwenye
nyumba kubwa kwa kupitia mlango wa jikoni. Alisema kuwa baada ya Dk Mvungi
kusikia kelele aliamua kutoka chumbani na ndio akakutana na watu hao wakiwa
tayari kwenye nyumba anayoishi.
“Walimkata panga utosini halafu wakampiga usoni kwa kutumia
ubapa wa panga. Aliangukia upande wa uso,” alisimulia Mwarabu.
Baada ya tukio hilo, watu hao walimwamuru mfanyakazi
aliyekuwa amefungwa kamba alale chini huku wengine wakiendelea kufanya upekuzi
kwenye nyumba hiyo.
Alisema baada ya hapo walikwenda kwenye chumba anacholala Dk
Mvungi na kumkuta mkewe, ambaye walimwamuru awape fedha.
“Mama alitoa fedha, lakini hatukuweza kujua ni kiasi gani
alichotoa. Maana tumemwacha apumzike kwanza,” aliongeza Mwarabu.
Kwa mujibu wa Mwarabu, majambazi hao baada ya kupewa fedha,
walidai kuwa fedha hizo hazitoshi na kutaka mke wa Dk Mvungi awaongezee zaidi.
“Walimtishia mama kuwa wangemchinja kama asingetoa fedha
zaidi, naye akasisitiza hakuwa na fedha na kuwaruhusu wamchinje,” alisema
Mwarabu.
Katika kushinikiza atoe kiasi cha fedha zaidi, watu hao
walimpiga kwa stuli Mama Mvungi na kumuumiza miguu yake ndipo wakaanza kupekua
kwenye makabati ya chumba chao cha kulala.
Kwa mujibu wa mtoto huyo wa Dk Mvungi, mbali na kuchukua
kompyuta na bastola watu hao walichukua simu tano, ambapo mbili zikiwa za Dk
Mvungi, mbili za mama yao na moja ya mfanyakazi wao. Alisema katika nyumba hiyo
wanaishi watu sita. Dk Mvungi, mkewe, fundi wa nyumba na wajukuu watatu.
Mwananchi ilipomtafuta tena Mwarabu jana jioni kujua hali ya
Dk Mvungi, alisema kwamba bado baba yake yuko mahututi na kwamba alikuwa hawezi
kuzungumza
JK amjulia hali
Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi waliokwenda
kumwona Dk Mvungi hospitalini alikolazwa.
Viongozi wengine waliokwenda kumtazama ni pamoja na Mkuu wa
Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Joseph Warioba na Makamu wake Jaji Agustino Ramadhan.
Warioba asikitika
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba alisema tukio hilo ni baya na limewashtua na kuwaachia simanzi. Alisema
kuwa wanasubiri taarifa itakayotolewa na vyombo vya usalama kuhusu tukio hilo.
“Hali ya mwenzetu ni mbaya, nimemwona hospitalini na kwa
kuwa alikuwa bado anahudumiwa na madaktari, sina cha kueleza zaidi ya kuwaomba
matabibu wetu waendelee kupigania afya yake ili arejee katika hali yake ya
kawaida,” alieleza Jaji Warioba.
Jaji Warioba aliwaomba Watanzania wote waungane kumwombea
mjumbe huyo, ambaye ni kiungo muhimu katika tume hiyo na kwamba kumkosa katika
kipindi hiki ni dhahiri kutaongeza pengo katika utendaji wa kila siku.
Naibu Katibu wa Tume hiyo, Casmir Kyuki alisema tukio hilo
analichukulia kuwa ni la kihalifu na kwamba kuna uwezekano ndio athari za kauli
zinazotolewa na wanasiasa dhidi yao (watumishi wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba), kwamba wanalipwa pesa nyingi.
“Hawa watu walilenga kupata pesa ambazo waliamini mwenzetu
alikuwa nazo. Hii inatokana na watu hasa wanasiasa kusema maneno bila hata
kujiridhisha,” alieleza Kyuki.
Kyuki alisema wajumbe wa tume wanaishi uraiani bila ulinzi
wowote kwa sababu wanafahamu hali zao ni za kawaida, lakini kutokana na maneno
dhidi yao jamii inadhani kuwa wana fedha nyingi sana.
“Magari tunayotumia yana nembo, watu wanafanya kazi mpaka
usiku, matokeo yake ndiyo hayo,” alisema Kyuki.
Post a Comment