Na Daniel Mjema, Mwananchi
Kwa ufupi
Mgawanyiko huo
unatokana na madiwani walio wengi kuwashtukia wenzao wawili kwamba wanacheza
mchezo mchafu wa kutaka kumpa mwekezaji mmoja eneo la katikati ya mji bila
masilahi ya Halmashauri kuwekwa wazi.
Moshi. Suala la mgawanyiko wa madiwani wa Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi, limechukua sura mpya baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Mipango Miji, Genesis Kiwelu kufungua taarifa Polisi akidai kutishiwa kuuawa.
Mgawanyiko huo unatokana na madiwani walio wengi kuwashtukia
wenzao wawili kwamba wanacheza mchezo mchafu wa kutaka kumpa mwekezaji mmoja
eneo la katikati ya mji bila masilahi ya Halmashauri kuwekwa wazi.
Kiwelu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ng’ambo (Chadema),
alipokea vitisho hivyo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) uliotumwa kwenye
simu yake ya mkononi na watu wasiojulikana wiki iliyopita.
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, wamegawanyika
katika makundi mawili huku wengi zaidi wakipinga utaratibu wa chini kwa chini
wa kutaka kumpa mwekezaji eneo lililopo katikati ya mji wa Moshi.
Moja ya SMS hiyo inasomeka; ”Mheshimiwa Kiwelu hatukuamini
kuwa wewe ni mtu mbaya na ovyo namna hiyo na sasa tutakuonyesha na utatujua
sisi ni akina nani…Unajitia hutaki rushwa huku unanuka shida”.
SMS nyingine inasomeka”Ukisikia watu wanachomewa nyumba ama
kumwagiwa tindikali ni mambo ya kipuuzi namna hii, nakuhakikishia
tutakufanyizia”, SMS zinazodaiwa kutumwa na kundi linalomuunga mwekezaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuelezea
sakata hilo, lakini Kiwelu mwenyewe alipotafutwa alilithibitishia gazeti hili
na kwamba alifungua jalada la uchunguzi Kituo cha Polisi Majengo.
“Ni kweli nimetumiwa hizo meseji na namba nisiyoijua na ukiipiga
haipatikani… Polisi waliniambia jalada litahamishiwa ofisi ya RCO (mkuu wa
upelelezi) lakini nahisi kiini ni hilo suala la uwekezaji”alisema Kiwelu.

Post a Comment