Home » » Mwanafunzi Mtanzania auawa Kenya

Mwanafunzi Mtanzania auawa Kenya

Written By JAK on Sunday, November 24, 2013 | 12:06 AM

http://www.capitalfm.co.ke/campus/wp-content/uploads/2013/08/Jerry.jpg
MWANAFUNZI wa kitanzania aliyekuwa anasoma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani (USIU) jijini Nairobi, Jerry Mruma amekutwa amekufa. Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari jijini Nairobi kutoka kwa Naibu Makamu wa Chuo Kikuu hicho anayeshughulikia mambo ya wanafunzi na Usimamizi wa Udahili, Ritah Asunda, ilisema mwili wa Jerry ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) ulipatikana jana.

Taarifa ya awali iliyotolewa na chuo hicho kuhusu kutoweka kwa Jerry tangu Jumamosi iliyopita, ilisema alikuwa akitafutwa, kabla ya jana kupatikana amekufa baada ya msako ulioongozwa na Kaimu Mkuu wa Usalama wa Chuo, Polisi na wanajumuiya ya chuo hicho.

Hata hivyo taarifa hiyo haikubainisha mwili wake ulikutwa eneo gani na ukiwa katika mazingira yapi na nini chanzo cha kifo chake.

“Msako huo ulianza baada ya ofisi ya mlezi wa wanafunzi kupokea taarifa za kutoweka kwa Jerry (23). Kifo chake kimekuja kabla jamii haijapoteza majonzi ya kuondokewa na mwanafunzi mwingine, Brian Frisby ambaye alipoteza maisha kwa ajali ya gari.

“Vifo vya wanafunzi hao wawili ni pigo kubwa kwa jumuiya ya USIU na tunatoa pole kwa familia na marafiki zao,” ilisema taarifa.

Jerry alitoweka usiku wa Jumamosi baada ya kutoka katika hoteli ya Pan Afrique ambako alikuwa akihudhuria hafla ya Usiku wa Mtanzania na kwa mara ya mwisho alizungumza na rafiki yake aitwaye Ogwellah saa 5.40 usiku.

“Rafiki yake mwingine wa kike alisema Jerry alimpigia simu kumjulisha kuwa alikuwa njiani kurudi nyumbani. Bahati mbaya, hakufika. Hakumsikia wala kumwona tena Jerry tangu usiku huo na kila alipopiga simu yake haikupatikana na alikwenda kutoa taarifa Polisi,” ilisema taarifa.

Jerry ambaye ni mtoto wa aliyepata kuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Isaac Mruma, alikuwa pia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kilimo Yetu jijini Nairobi ambayo inajishughulisha na masuala ya kilimo.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger