Home » » JK ataka Waafrika wasifarakanishwe

JK ataka Waafrika wasifarakanishwe

Written By JAK on Sunday, November 24, 2013 | 12:12 AM

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjd2-vlc2vQzb5C6tYz1g-OfBgcUarn-nXK5iph_Yo5KSl9O89ZwACVcRiB-8RL32tAezYRGFuKbgs2oVZgx0Ybkt8bPFPqgFeQrF0P82NoyksBQzwrcUwTgp91pyjiB2Fw8S0e5Te33Qw3/s640/ccc2.jpg
 By Mwandishi Maalumu, Warsaw, Poland
 
RAIS Jakaya Kikwete ametaka mawaziri na maofisa waandamizi wa nchi za Afrika wanaoshiriki majadiliano na nchi zilizoendelea, kutafuta njia za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kukataa kufarakanishwa au kugawanywa na nchi tajiri.

Aidha, amesema suala la nchi tajiri kusaidia zinazoendelea katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi si hisani wala fadhila, bali wajibu wa nchi hizo ambazo kimsingi ndizo zinasababisha matatizo makubwa ya tabianchi ambayo dunia inakabiliana nayo.

Rais Kikwete alisema hayo juzi alipohutubia mawaziri wanaounda Umoja wa Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira (AMCEN) pamoja na Kundi la Maofisa Waandamizi wa Afrika Wanaoshiriki Majadiliano kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi – COP19/CMP9, kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Poland mjini Warsaw.

Kikwete anawakilisha bara la Afrika kwa nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mazingira (CAHOSCC), nafasi ambayo aliombwa na viongozi wenzake aitumikie mwanzoni mwa mwaka huu.

Ataishikilia nafasi hiyo kwa miaka miwili. Rais Kikwete alisema ni muhimu kwa Afrika kushiriki majadiliano hayo ikiwa na sauti moja, wakikataa kugawanywa ama kufarakanishwa kama namna ya kuwapunguza nguvu katika majadiliano hayo magumu na ambayo bila shaka yanachukua muda mrefu.

“Nimekuja hapa kukuungeni mkono. Hii ni sawa na vita na nyie ndio askari wa mstari wa mbele. Mimi ni Mkuu wa Majeshi ambaye nimekuja kukutembeleeni na kukuungeni mkono katika vita hii ngumu ya kuiokoa dunia. “Kwetu sisi Waafrika, ushahidi wa mabadiliko ya tabianchi uko wazi kabisa. Leo, tunapata mafuriko hata Somalia, tangu lini tukapata mafuriko makubwa ya kiasi hiki jangwani? Huwezi kujua, siku nyingine itakuwa ni Dar es Salaam au Mombasa.”

Aliongeza: “Ujumbe wangu ni wa umoja, kuweni wamoja, msikubali kugawanywa, wala kufarakanishwa kwa njia yoyote ile. Mimi kazi yangu ni kukutakieni mafanikio katika mapambano haya. Tunachokitaka sisi katika Afrika tunakijua, uwezo wa kukitafuta tunao, mnajua tulikotoka na mnajua tunakokwenda.

Nawaamini sana, naamini katika uwezo wenu.”

Kuhusu uamuzi wa mikutano iliyopita ya nchi tajiri na zilizoendelea duniani kusaidia nchi masikini zaidi duniani kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Rais Kikwete aliwaambia mawaziri hao:

“Huu ni wajibu wao kwa sababu ndiyo wameifikisha dunia kwenye vurugu hii ya hatari. Hivyo, ni lazima wabebe wajibu na jukumu la kutusaidia sisi masikini kukabiliana na hali hiyo, kwa sababu athari hizo zitamfikia kila mtu na kila nchi hata kama zitaanza kwa sisi tusiokuwa na uwezo mkubwa.

“Sisi ni kama sungura aliyekutwa amebeba mishale na upinde akiwa njiani kwenda kupambana na tembo.

Kila mtu alimcheka. Sisi ni kama sungura anayekwenda kupambana na tembo. Kazi yetu ngumu lakini siku moja, mahali fulani, tembo ataanguka,” alisema Rais Kikwete huku mawaziri hao wakiangua kicheko.

Kauli ya Rais Kikwete, iliungwa mkono na mawaziri wa Senegal, Gabon, Uganda, Niger na Angola na Kamishna wa Maendeleo ya Vijijini na Kilimo wa Umoja wa Afrika (AU) Rhoda Peace Tumusiime.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger