By Mohamed Akida Habari Leo
ISMAIL Aden Rage amewasili nchini jana saa 1.35 usiku akitokea Sudan Kusini na kuwaambia mashabiki wa klabu ya Simba waliojitokeza kumlaki kwamba yeye bado ni Mwenyekiti halali wa klabu hiyo na mapinduzi yaliyofanywa na Kamati ya Utendaji hayana uwezo huo kisheria.
Mapema wiki hii, Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo chini ya Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ ilitangaza kumsimamisha Rage kutokana na kikao ilichokaa usiku wa Jumatatu kutokuwa na imani naye katika mambo mbalimbali yanayoihusu timu hiyo.
Rage alipokewa na mashabiki wa Simba zaidi ya 200 ambao walikuwa kwenye mabasi madogo zaidi ya matatu na alibebwa na mashabiki hao, na baadaye wakaondoka kwenda Makao Makuu ya Simba, Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo ambako alikuwa akisubiriwa kwa hamu na wanachama.
“Nashukuru sana mashabiki na wanachama kwa kuja kunipokea. Hii inaonesha namna mlivyokuwa na imani na mimi Mwenyekiti wenu ila kwa kifupi kikao kilichotumika kunitoa madarakani siyo halali, kwa kuwa ukisoma Katiba ya Simba na ile ya FIFA na CAF zinaonesha wazi kwamba Kamati ya Utendaji haina uwezo wa wa kumsimamisha Mwenyekiti au Rais,” alisema Rage ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini.
Rage ambaye alikuwa kikazi Juba, Sudan Kusini kwa wadhifa wake huo wa ubunge, alisema kwa jana asingeweza kuzungumza mengi kwa sababu rafiki yake mpendwa, Kabwe Zitto ameondolewa kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, hivyo mengi atayazungumza leo mchana klabuni.
Zitto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo Rage ni Mjumbe wake na walikuwa pamoja Juba, lakini mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, aliwahi kurejea nchini ili kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu ya chama chake kilichomvua nyadhifa zake jana.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope aliwasili uwanja wa ndege saa 1.10 usiku na alipofuatwa na waandishi kutaka kufahamu kilichomfikisha hapo, alisema yeye siyo Rage ila amefika hapo kwa ndege moja na Rage. Alishiriki katika kikao kilichomsimamisha mwenyekiti huyo.
Post a Comment