By John Nditi, Morogoro
WIMBI la kuuawa kwa tembo limeendelea kushika kasi katika hifadhi za Taifa, baada ya vipande 34 vya meno yenye uzito wa kilo 82.20 na thamani ya Sh milioni 408 kukamatwa na askari wa Idara ya Wanyamapori yakiwa ndani ya gari la mizigo eneo la Lupiro wilayani Ulanga, mkoani hapa.
Meno hayo yalikutwa ndani ya lori namba T 647 AAT aina ya Isuzu Forward, ambalo lilitelekezwa kwenye gereji inayomilikiwa na Pastor Kamota, mkazi wa tarafa ya Lupiro baada ya dereva ambaye hakufahamika jina kutoweka katika mazingira ya utatanishi eneo hilo.
Ofisa Wanyamapori wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa, alilithibitishia gazeti hili jana, kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 18 jioni ambapo mmiliki wa gari hilo kwa mujibu wa kadi ya usajili limetambulika kwa jina la Hussein Sulva, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo, vipande hivyo vya meno ya tembo vilivyokutwa ndani ya gari ni sawa na idadi ya tembo 17 waliouawa kwenye hifadhi ya Taifa, ambapo gari hilo liliegeshwa kwenye gereji hiyo kwa kisingizio cha ubovu.
Hata hivyo, alisema Polisi inamshikilia mmiliki wa gereji hiyo kwa uchunguzi na mahojiano ya kina wakishirikiana na maofisa wa wanyamapori.
Post a Comment