By Halima Mlacha, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, amehadharisha juu ya kauli zinazotolewa na viongozi wa Serikali yake kuhusu masuala muhimu yanayoihusu Zanzibar. Amesema ni pamoja na msimamo wa visiwa hivyo kuhusu Katiba mpya, na kusema wanayoyatoa ni maoni yao binafsi na si msimamo wa Serikali.
Amesisitiza kuwa msimamo wowote wa Serikali, mwenye mamlaka ya kuusemea ni yeye na si mtu mwingine, kulingana na mamlaka ya kikatiba aliyopewa. Dk Shein alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya kuelezea mafanikio ya Serikali ya SMZ awamu ya saba katika kipindi cha miaka mitatu tangu aingie madarakani.
“Naomba niliweke hili wazi, hakuna kiongozi yeyote awe waziri, makamu wa kwanza au wa pili wa Rais anayeweza kuisemea Zanzibar kuhusu jambo lolote isipokuwa mimi kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Katiba,” alisisitiza.
Moja ya maswali ya waandishi wa habari hao ni pamoja na kauli za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni, akizungumza kuwa msimamo wa Zanzibar ni muundo wa Serikali ya Mkataba.
“Kama Makamu wa Kwanza wa Rais alizungumza kuhusu msimamo wetu wa Katiba, basi alikuwa akisema yake, au alikuwa akizungumzia chama chake, Katiba yetu iko wazi, kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake, hivyo kama ametoa msimamo kuhusu Katiba ni wake na si wa Serikali,” alisisitiza.
Dk Shein alisema anachojua yeye ni kwamba hadi sasa mchakato wa Katiba unaendelea vizuri na maoni ya Watanzania wakiwamo Wazanzibari ndiyo yatakayoamua muundo wa Serikali kwani hata yeye hana mamlaka ya kusemea Wazanzibari.
Aidha, Dk Shein alisema katika kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), unahitajika uvumilivu mkubwa na ushirikiano ili kuwa na nchi yenye amani na utulivu na inayotawalika.
Alisema jambo la msingi ambalo Serikali yake inalipa kipaumbele ni kuhakikisha kila kiongozi na mwananchi wa kawaida anafuata Katiba.
Kusaini mkataba Alitumia fursa hiyo kuvunja ukimya juu ya watu wanaomtuhumu kuwa alikwenda kinyume cha Katiba kusaini mkataba wa masuala ya utafiti wa mafuta akiwa Uholanzi na kutaka waliomzushia wafanye utafiti kwanza kabla ya kuropoka.
“Sijawahi kuvunja Katiba wala sitoivunja, nimefanya kazi serikalini tangu kipindi cha Rais Benjamin Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete, naifahamu vema Katiba,” alisisitiza.
Alisema akiwa Uholanzi hakusaini Mkataba wa Nishati bali alisaini maelewano ya awali ya mkataba huo na kama kuna mtu ana ushahidi kuwa alisaini mkataba awasilishe ushahidi.
“Nimesikia haya kwenye vyombo vya habari tena cha kushangaza, wanaosema haya ni wanasheria, naomba wakilete hicho wanachokisema kuwa nimefanya, na maelewano ya aina hii si ya kwanza kusaini yapo niliyosaini mwaka 2011 mbona hawakusema?” Alihoji.
Pamoja na hayo, Rais pia alizungumzia masuala ya Muungano hasa eneo la mapato ambapo alisema masuala hayo mengi yako katika hatua ya mazungumzo, ili kufikia mwafaka kwa pande zote mbili.
“Si kweli kuwa tunasubiri Katiba kushughulikia masuala nyeti ya Muungano kama vile mgawanyo wa mapato, kwa sasa Zanzibar inapata asilimia 4.5 ya mgawo wa mapato kutoka Tanzania Bara, lakini kuna maeneo nyeti ambayo gharama za kuyaendesha nchi zote mbili zinagharimia, hivyo suala hilo linatafutiwa ufumbuzi kwa sasa,” alisema.
Mafanikio SMZ Katika kikao hicho, pia Dk Shein alizungumzia mafanikio ya Serikali yake kwa miaka mitatu tangu ishike uongozi kuwa ni makubwa katika maeneo mengi, ikiwamo kudumisha amani na utulivu visiwani.
“Hata hivyo, suala la watu kumwagiwa tindikali ndilo lililotia doa SMZ ndani na nje ya nchi hasa kitendo cha raia wa Uingereza kumwagiwa tindikali, kwa kweli nilisikitika sana na kiukweli Tanzania na hasa Zanzibar ilichafuka kwa vitendo hivi,” alisema.
Alifafanua, kwamba vitendo vya kumwagia watu tindikali vilianza mwaka 1995 na kukithiri miaka ya karibuni hadi sasa watu wanane wamekumbwa na mkasa huo, jambo ambalo Serikali imeanza kulifanyia kazi.
Alisema pamoja na changamoto iliyopo ya kutambua wahusika, Serikali zote mbili ya SMZ na Tanzania Bara, ziko katika mchakato wa kuangalia matumizi halisi na sababu za uingizwaji wa kemikali hizo nchini ili kuona namna ya udhibiti wake.
Kitovu cha uchumi Dk Shein alizungumzia pia mpango wa Serikali kuifanya Zanzibar kitovu cha uchumi Afrika Mashariki kwa kuhakikisha kuwa mji wa Unguja unajengwa upya kwa kufuata mipango miji ya kisasa.
Halikadhalika, alizungumzia namna Serikali yake imekuwa ikishughulikia masuala ya afya, elimu, utawala bora, utalii, viwanda na uchumi na kusisitiza kuwa sekta hizo sasa zimeboreshwa zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma kabla ya awamu ya saba ya Serikali yake.
“Niliingia madarakani mambo mengi yakiwa bado hayaridhishi, lakini kwa sasa mambo yanakwenda vizuri, kwani hata uchumi wakati nikiingia madarakani ulikuwa unakua kwa asilimia 6 .7 kwa sasa umepanda na kufikia asilimia 7.5,” alisema.

Post a Comment