Amina Mohamed,waziri wa mambo ya nje wa Kenya ... na Waziri mwenzie wa mambo ya nje Tanzania Bernard Membe
By Halima Mlacha
SERIKALI ya Kenya imetuma ujumbe wa kuunga mkono msimamo wa Tanzania wa kutojitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha ya baadhi ya nchi ikiwemo nchi hiyo, kwenda kinyume na Mkataba wa Jumuiya hiyo. Ujumbe huo umeletwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, aliyewasili nchini juzi ambapo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema Serikali ya Kenya imesoma kwa undani hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na imefurahishwa na namna Tanzania inavyoisaidia Kenya.
Katika hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita, alihoji hatua ya Kenya, Uganda na Rwanda kukutana na kufanya uamuzi wa masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, bila kushirikisha Tanzania na Burundi.
Katika mikutano ya nchi hizo tatu, wakuu wa nchi hizo tatu walizungumzia na kuamua pamoja na mambo mengine, kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura na ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
Mengine ni kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote na kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
Pia wamezungumza na kuamua kuharakisha uanzishwaji wa hati moja ya kuishi (visa) katika nchi hizo kwa ajili ya utalii, kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao na kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Tanzania kwa mujibu wa Rais Kikwete, haipingi kukutana kwa nchi hizo kwa kuwa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na kuamuliwa, yako yasiyo ya Jumuiya, ila inapinga mambo ya Jumuiya kufanyiwa uamuzi katika vikao hivyo vya utatu. Miongoni mwa mambo ambayo Tanzania inapinga, ni kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete suala hilo lilijadiliwa katika Mkutano Maalum wa 11 wa wakuu wa nchi wanachama, uliofanyika Aprili 28, mwaka jana jijini Arusha ambapo nchi zote wanachama ziliridhia mapendekezo ya kuanzisha himaya hiyo. Jambo lingine ambalo Tanzania inapinga kufanyiwa uamuzi katika vikao hivyo vya utatu, ni kuanzishwa kwa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
Rais Kikwete katika hutoba hiyo, alisema suala hilo lilizungumzwa katika mkutano wa 14 wa wakuu wa nchi wanachama uliofanyika Novemba 30, mwaka jana Nairobi, Kenya na walipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kuanzishwa kwa Shirikisho.
“Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia shirikisho la kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu.
“Inatarajiwa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi mwezi huu. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki?”
Alihoji Rais Kikwete na kusisitiza kuwa Tanzania haitajitoa katika Jumuiya pamoja na kuwepo kwa mazingira hayo ya kutengwa. Waziri wa Kenya Akitetea uamuzi wa Serikali yake na baadhi ya nchi wanachama kufanya mkutano bila kuishirikisha Tanzania, Mohamed alisema masuala yaliyojadiliwa yalihusu wanachama hao na yalikuwa ni masuala madogo ambayo hayakulenga kuingilia mikutano au makubaliano mengine ya Jumuiya hiyo.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alifafanua kuwa mkutano uliofanyika Mombasa, ulilenga kujadili suala la mizigo katika bandari ya Mombasa huku akisisitiza kuwa katika bandari hiyo, mizigo huchukua zaidi ya siku 28 kuwasili Kampala na huchukua muda mrefu zaidi kuwasili katika nchi nyingine zisizo na bahari.
“Kutokana na kutofanya vizuri kwa bandari, ilikuwa ni muhimu suala hilo kujadiliwa na marais hao na hakukuwa na ajenda nyingine zaidi ya hapo. Tunafahamu kuwaTanzania ni moja ya waanzilishi muhimu wa EAC.
“Hili ni jambo zuri, mikutano kama hii inajikita katika maeneo ambayo huenda hayajaguswa katika mikutano ya EAC. Ki ukweli jambo hili si geni na wala halihusu kabisa kutenga mwanachama mmoja kwa kuwa ni muhimu kwa wanachama wote. “Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha Jumuiya inadumu ikiwa na wanachama wake watano kwa ajili ya kujiletea maendeleo kwa wananchi wote,” alisisitiza Mohamed.
Waziri huyo alimpongeza Rais Kikwete kwa mchango wake na msaada kwa nchi ya Kenya, huku akisisitiza kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuzungumza kwa uwazi suala la Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Mbali na katika mikutano ya AU, msimamo wa Tanzania kuhusu ICC uliwekwa wazi na Rais Kikwete hata katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) hivi karibuni.
“Kenya inategemea msaada wenu, bila msaada huu hatuwezi kukabiliana na suala la ICC,” alisema na kuongeza kuwa kati ya Januari na Februari mwakani, nchi wanachama wa EAC zinatarajiwa kufanya mkutano jijini Nairobi au Dar es Salaam kujadili masuala ya Jumuiya.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini, Bernard Membe, alipongeza hatua hiyo ya Serikali ya Kenya kuja nchini kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete kuhusu EAC.
Membe alisema Kenya ni nchi ya kwanza kuchukua hatua ya kupongeza hotuba ya Rais Kikwete bungeni ambayo ililenga kuhakikisha kuwa Jumuiya hiyo inarejea katika malengo yake ya zamani ya kuhakikisha kila mwanachama ananufaika.
Alisema mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika Aprili mwaka huu, ulijadili mambo mengi ya maendeleo ikiwemo masuala ya umeme, reli na bandari na ripoti ya masuala hayo ilitakiwa itolewe rasmi mwezi huu.
Katika mkutano huo kwa mujibu wa Membe, kulikuwa na masuala ambayo Tanzania haikuyaunga mkono pamoja na kuungwa mkono na wanachama wengine, ambayo ni masuala ya ardhi ambayo yanatakiwa yabaki chini ya mamlaka ya nchi husika.
“Tanzania haijawahi kupinga ajenda za jumuiya hiyo isipokuwa suala la ardhi ambalo, nchi yetu inaamini kuwa ni lazima lisiwe ajenda ya EAC, lakini masuala mengine tutafuata hatua zote zitakazokubaliwa na Jumuiya,” alisisitiza Membe.
Kuhusu suala la ICC, Membe alisema Tanzania imeomba rufaa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kesi inayoendelea dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambapo imeomba muda wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, uongezwe kwa mwaka mmoja ili kutoa muda kwa Rais huyo kushughulikia masuala ya nchi yake. Kwa sasa mahakama hiyo, imeahirisha kesi hiyo dhidi ya Rais Kenyatta hadi Februari 5, mwakani.

Post a Comment