BAADA ya kushindwa kumrejesha kundini kipa wake wa zamani, Juma Kaseja, Simba sasa imeelekeza nguvu zake kwa kipa wa Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif ‘Cassilas’. Awali ilidaiwa kuwa Simba ilitaka kumrejesha kipa wake Kaseja baada ya aliyechukua nafasi yake Abel Dhaira kushindwa kufanya vizuri katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliomalizika Novemba 7.
Lakini kabla hilo halijatimia, mwishoni mwa wiki iliyopita, Kaseja alisaini mkataba wa miaka miwili na Yanga na hivyo Simba kubaki njiapanda.
Simba iliachana na Kaseja baada ya kipa huyo kumaliza mkataba wake, ikidai kuwa ameshuka kiwango.
Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilisema kuwa Simba imeanza kumfukuzia Cassilas na tayari imeanza kufanya mazungumzo na watu wa karibu na mchezaji huyo.
“Tayari wameanza mazungumzo na Cassilas, wanataka kumsajili kwa ajili ya mzungukowa pili achukue nafasi ya Dhaira,” kilisema chanzo cha habari. Sharrif yuko kikosi cha Future Young Stars. Hata hivyo, Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema uongozi wake hauna taarifa za Simba kumtaka Cassilas na hata kama ikitokea wametuma maombi, hawatakubali.
“Hatuna taarifa za Simba kumtaka Cassilas, hawajatuma maombi na hawajazungumza na yeyote kuhusu kipa huyo, lakini hata kama wakituma, hatuuzi mchezaji yeyote kwa sasa, tunataka kujiimarisha kwenye ligi hivyo hatuna mpango wa kuuza mchezaji,” alisema Bayser. Mbali na Dhaira ambaye ni raia wa Uganda, makipa wengine wa Simba ni Andrew Ntala na Abuu Hashim.
Aidha, tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hansppope amesema watalazimika kuachana na Dhaira kutokana na kanuni za usajili kutaka wachezaji watatu wa kigeni badala ya watano.
Hansppope alisema wanatafuta kipa, akipatikana kabla ya kuanza mzunguko wa pili na ikipatikana timu ya kumpeleka Dhaira, watafanya hivyo.
Tangu alipoondoka Kaseja, lango la Simba limekuwa likiyumba, hali inayowalazimu vigogo wa timu hiyo kusaka kipa mwingine ili kurekebisha makosa ya mzunguko wa kwanza.

Post a Comment