Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya makubaliano ya kukabidhi Mgodi wa Tulawaka kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kutoka kwa kampuni ya uchimbaji wa madini ya African Barrick Gold (ABG), katika hafla iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za wizara jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Gray Mwakalukwa (kushoto) na Makamu wa Rais wa Mgodi wa African Barrick Gold (ABG), Deo Mwanyika (katikati) wakitia saini makubaliano ya kukabidhi Mgodi wa Tulawaka kwa STAMICO kutoka ABG, katika hafla iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa ABG, Brad Gordon.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Gray Mwakalukwa (kushoto) akipeana mkono wa pongezi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa African Barrick Gold (ABG), Brad Gordon (kulia) baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini makubaliano ya kukabidhi Mgodi wa Tulawaka kwa STAMICO kutoka ABG, katika hafla iliyofanyika hivi Dar es Salaam. Anayeshuhudia (katikati) ni Makamu wa Rais wa Mgodi wa ABG, Deo Mwanyika.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuanzia sasa serikali itakuwa na hisa katika migodi yote ya madini itakayoanzishwa hapa nchini ikiwa ni hatua ya kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali husika.
Profesa Muhongo aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano ya Serikali kutwaa umiliki wa Mgodi wa dhahabu wa Tulawaka kutoka kwa Kampuni ya African Barrick Gold (ABG).
Katika Makubaliano hayo, ambapo Serikali inawakilishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), shirika hilo limeuchukua mgodi wa Tulawaka na baadhi ya leseni za utafutaji wa madini zinazozunguka eneo husika kwa gharama ya dola za Marekani milioni 4.5.
Aidha, kama sehemu ya makubaliano, STAMICO itachukua umiliki na usimamizi wa mfuko wa fedha za ukarabati wa mazingira, ikiwa kama sehemu ya mpango wa ufungaji wa mgodi huo na itachukua dhamana ya majukumu yaliyopita na ya baadae yanayohusiana na kufunga mgodi na ukarabati wa mazingira.
Waziri Muhongo, ambaye alishuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo alisisitiza kuwa “lengo kuu la serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na kufuta ile dhana iliyojengeka katika jamii kuwa watanzania hawanufaiki na rasilimali ya madini.”
Alifafanua kuwa STAMICO itamiliki na kuendesha mgodi huo kwa niaba ya watanzania na kwamba wataendeleza shughuli za uchimbaji na wakipata faida watauza hisa kwa wananchi wengi ili waweze kushiriki moja kwa moja katika umiliki.
Aidha, Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kusisitizia suala la wamiliki wa vitalu vya madini wasioviendeleza na kusema kuwa serikali imedhamiria kuwanyang’anya maeneo hayo na kuwapatia wachimbaji wadogo kama Rais Jakaya Kikwete alivyoagiza hivi karibuni.
Post a Comment