UPANDE wa maombi katika kesi ya kikatiba dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana ulianza kujibu hoja za pingamizi la awali lililowasilishwa na upande wa serikali.
Kesi hiyo ya kikatiba dhidi ya Waziri Pinda, ilifunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam mbele ya jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakhi Jundu.
Majaji wengine ni Augustine Mwarija na Dk Fauz Twaib. Katika pingamizi la awali, upande wa serikali ulikuwa na hoja tano ambazo mawakili wa LHRC na TLS walitakiwa kuzitolea majibu.
Hoja hizo za upande wa serikali ni pamoja na ile iliyosema kuwa mahakama hiyo haiwezi kutolea maamuzi maombi ya LHRC na TLS. Wakili wa upande wa waleta maombi (LHRC na TLS) Jeremia Mtobesya, akitoa majibu alidai kuizungumzia hoja hiyo ni sawa na kuifanya mahakama kuingia katika msingi wa shauri lenyewe.
“Hatua ya serikali kusema kuwa mahakama hiyo haiwezi kusikiliza na kutolea uamuzi maombi yao ni sawa na kuongelea suala la maombi ambayo yanatokana na kesi ya msingi katika hatua za awali,” alidai Mtobesya.
Mtobesya alidai kuwa kutokana na sababu hiyo aliiomba mahakama hiyo itupilie mbali hoja hiyo ya serikali kwakuwa haina msingi wowote.
Katika pingamizi lao la awali, upande wa serikali unadai kuwa kesi hiyo ni batili Kikatiba kwa sababu inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Haki, Mamlaka na Kinga za Bunge ambazo zinakataa suala lililotokea wakati wa shughuli za Bunge kutohojiwa au kujadiliwa na chombo chochote.

Post a Comment