Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Kilwa
MABOMBA ya urefu wa kilometa 142 kati ya kilometa 542 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam yameunganishwa.
Mabomba mengine yameongezewa uzito kwa kuwekewa zege kwa ajili ya kufukiwa katika eneo la kilometa 25 baharini katika eneo la Somangafungu kuelekea kisiwa cha Songosongo.
Hayo yalibainika katika ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akiongozana na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba na Benki ya Dunia (WB).
Maswi alisema kazi ya kuunganisha mabomba hayo ilianza Septemba mwaka huu hivyo kutokana na kasi ya ujenzi huo malengo ya serikali ya utandazaji wa gesi kukamilika Julai mwakani.
Alisema wakati kazi ya kuunganisha mabomba ikiendelea kwa utaalamu wa kisasa, mabomba hayo yanaunganishwa yakiwa tayari katika maeneo ya kuchimbiwa huku reli maalumu kwa ajili ya kupeleka mabomba baharini ukiendelea.
Maswi alisema nia ya ziara hiyo kwa wadau wa maendeleo ni kuwaonesha jinsi ujenzi huo unavyoendelea kwani wengi walikuwa wakipinga na kutoamini kama itaweza kujenga bomba hilo huku wengine wakidhani wajenzi wa kichina watalipua ujenzi huo.

Post a Comment