Home » » JK aanza safari ya historia

JK aanza safari ya historia

Written By JAK on Monday, December 30, 2013 | 7:51 AM


http://www.bongo5.com/wp-content/uploads/2012/10/Jakaya-Kikwete.jpg

RAIS Jakaya Kikwete, leo anakabidhiwa Rasimu mpya ya Katiba, baada ya kufanyiwa marekebisho na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

Makabidhiano hayo yanafanyika jijini Dar es Salaam, mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, kuashiria kuanza kwa hatua inayofuata ya uundaji wa Bunge Maalumu la Katiba.

Taarifa ya Katibu wa Tume, Assaa Rashid, iliyotumwa juzi kwa vyombo vya habari, ilifafanua kwamba mbali na Dk Shein, makabidhiano hayo yanatarajiwa kushuhudiwa na viongozi wengine wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi za dini, asasi za kiraia na wananchi wa kawaida.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba ndiye atakabidhi ripoti hiyo ya mchakato wa Katiba na Rasimu ya katiba kwa marais. Taarifa hiyo ya tume inatarajiwa kueleza mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika mchakato wa marekebisho ya katiba, changamoto walizozipitia pamoja na mapendekezo ambayo Tume inaona yanafaa kuwepo kwenye katiba.

Hafla hiyo pia inatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa, Taasisi za kidini, Asasi za kiraia na wananchi wa kawaida.

Rasimu hiyo ya Katiba imetokana na maoni ya wananchi, viongozi na makundi mbalimbali waliyowasilisha kwa Tume kupitia njia mbalimbali zikiwemo mikutano, barua pepe, anuani za posta, tovuti na ukurasa wa facebook wa Tume.

Awali rasimu hiyo ilitarajiwa kabla ya Desemba 15 mwaka huu baada ya kuongezewa muda na Rais kwa mara ya kwanza, lakini Tume iliomba kuongezwa muda wa kukabidhi rasimu hiyo kwa mara ya pili na kuongezewa siku 14 kuanzia Desemba 16 mwaka huu.

Kwa hatua hiyo Rais Kikwete alikuwa ameiongezea Tume muda kwa siku 59, kati ya siku 60 ambazo anaruhusiwa kuongeza kisheria. Hata hivyo, Tume hiyo imefanikiwa kumaliza kazi hiyo kabla ya muda ulioongezwa kwa mara ya pili, ambao ulikuwa ukiisha Desemba 29 mwaka huu.

Bunge la Katiba

Kwa mujibu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, baada ya rasimu hiyo kukabidhiwa, tume hiyo itavunjwa ili kutoa nafasi kwa uundwaji wa Bunge Maalumu la Katiba.

Bunge hilo litaundwa na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao ni 357, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar 76 na wajumbe wengine 201 watakaoteuliwa na Rais kutoka katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini.

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini, yatatakiwa kupendekeza majina ya watu wanne hadi tisa, ambayo yatapelekwa kwa Rais, naye atateua majina matatu.

Rais kabla ya uteuzi huo, atakaa na vyombo vyake na kuteua majina ya wajumbe ndani ya mapendekezo ya mashirika na taasisi hizo. Uamuzi wa vipengele vya Katiba mpya ndani ya Bunge hilo, unatarajiwa kufanyika kwa kupigiwa kura ambapo kila kipengele kitapita kwa kupata kura ya zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na hivyo rasimu ya tatu ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi.

Akizungumza juzi na waandishi wa habari, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ametaka makundi kuharakisha kupeleka majina ya wanaopendekeza wayawasilishe kwenye Bunge la Katiba, ili Rais afanye uteuzi wake. Kwa mujibu wa Waziri Chikawe, mwisho wa kupeleka majina Ikulu ni wiki hii, Januari 2.

Kura ya maoni Baada ya Bunge Maalumu la Katiba, kukamilisha kutengeneza rasimu ya tatu ya Katiba, makundi ya watu, vyama na asasi za kiraia wanaokusudia kupinga na kuunga mkono rasimu hiyo yataundwa katika kamati na kusajiliwa katika majimbo mbalimbali.

Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ndizo zitakazowajibika katika kusajili kamati hizo katika majimbo husika. Kamati hizo zitateua mawakala wa kusimamia kura zitakazokataa au zitakazokubali katiba mpya, ambazo zitapigwa na wananchi.

Upigaji kura

Katika upigaji kura wa maoni kwa ajili ya upatikanaji wa Katiba mpya, kutakuwa maswali, likiwemo ambalo wapigakura watatakiwa kujibu ndio, kwamba wanaikubali Katiba mpya au hapana, kwamba wanaikataa.

Swali hilo la kura ya maoni litaandaliwa na NEC na ZEC na litahitaji jibu la ndio au hapana, tofauti na utaratibu wa uchaguzi uliozoeleka wa kupigia kura mtu au chama.

Aidha, NEC na ZEC ndizo zilizopewa wajibu kisheria wa kusimamia uendeshaji wa kura hiyo ya maoni na kusimamia elimu ya wapiga kura katika kura za maoni.

Tume hizo pia ndizo zitakazoteua wasimamizi wa kura ya maoni kwa kila jimbo kusimamia uendeshaji wa kura ambapo kila msimamizi kwa kushirikiana na tume zote mbili, atateua maofisa na Naibu maofisa wa kura ya maoni kwa ajili ya kusimamia vituo vya kupigia kura.

Wapigakura watakuwa waliosajiliwa katika daftari la kudumu la wapiga kura la NEC na ZEC. Hivyo kila mwananchi mwenye sifa na aliyeandikishwa kwenye madaftari hayo ya kupiga kura, atashiriki katika kupiga kura ya maoni.

Source Habari Leo
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger