Home » »

Written By JAK on Sunday, December 8, 2013 | 4:00 AM

MAADHIMISHO YA MIAKA 52 YA UHURU KUFANA, WANANCHI WAOMBWA KUJITOKEZA KWA WINGI.

Na. Aron Msigwa –MAELEZO.

Zikiwa zimebaki siku mbili Tanzania iadhimishe miaka 52 ya Uhuru, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadick ametoa wito kwa watanzania kusherehekea maadhimisho hayo kwa  kuenzi , kulinda na kudumisha mafanikio makubwa yaliyopatikana  tangu Uhuru.

Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam Meck Sadiki amesema kuwa Tanzania katika kipindi cha miaka 52 ya Uhuru imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi, ulinzi, usalama pamoja na uhusiano wa kimataifa na kuongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na umoja na mshikamano ulioonyesha tangu kuasisiwa kwa taifa la Tanzania.

“Kipindi chote cha miaka 52 ya Uhuru  tumepata mafanikio makubwa sana na  ya kujivunia kiuchumi, ulinzi na usalama pamoja na uhusiano wa kimataifa, tuna kila sababu ya kuendeleza mafanikio haya”

Amesema maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru kwa mwaka 2013 kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete chini ya kauli mbiu isemayo “Vijana ni Nguzo ya Rasilimali Watu, Tuwaamini, Tuwawezeshe na Tuwatumie kwa Manufaa ya Taifa Letu”

Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka  huu yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na kupambwa na burudani za vikundi vya ngoma za asili kutoka bara na visiwani,Gwaride maalum la vikosi vya ulinzi na Usalama, kwaya mbalimbali, bendi za muziki, maonyesho ya ndege za kijeshi na halaiki maalum. 

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi  na kuwahi mapema wakati wa maadhimisho hayo   na kubainisha kuwa kutokana na maadalizi mazuri yaliyofanyika milango ya uwanja wa Uhuru itakuwa wazi kuanzia saa 12:30 Asubuhi.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger