Na Hassan Hamad, OMKR
Jeshi la polisi Zanzibar limehimizwa kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi, ili wananchi waendelee kuishi katika hali ya amani na usalama.
Akizungumza na kamishna mpya wa jeshi la polisi Zanzibar ofisini kwake Migombani, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema licha ya polisi kuwa na jukumu kubwa la kulinda usalama wa raia na mali zao, jeshi hilo pia linapaswa kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji na usimamizi wa sheria.
Amesema licha ya kuwepo sheria nzuri katika nchi lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua, hali inayopelekea kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria na kupelekea kuwepo kwa vitendo vya uhalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Amelitaka jeshi hilo kuondosha muhali katika kusimamia utekelezaji wa sheria, ili kuona kwamba sheria zilizotungwa zinafuatwa na kuleta ufanisi katika jeshi hilo na taifa kwa ujumla.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesisitiza kuwa iwapo sheria zilizopo zitatekelezwa ipasavyo, jamii itaziheshimu na kuepukana na vitendo vya uvunjaji wa sheria, na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Hata haya matuta tanayowekwa kila pahala barabarani sio dawa ya kuzuia ajali, lakini naamini alama za barabarani iwapo zitafuatwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti mwendo wa madereva, basi ajali nyingi zingeepukwa”, alisema Maalim Seif.
Aidha Maalim Seif amelishauri jeshi hilo kuimarisha uhusiano wake na raia wema, ili kusaidia kuwafichua wahalifu na watu wanaojihusisha na vitendo viovu vikiwemo uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
Amesema ofisi yake bado inakabiliwa na changamoto ya dawa za kulevya, na kulitaka jeshi la polisi kufanya juhudi za makusudi kuona kuwa changamoto hiyo inatatuliwa.
Amesema serikali itatoa kila ushirikiano kwa kamishna huyo mpya, ili kuhakikisha kuwa anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa atatekeleza majukumu yake ya kusimamia sheria, ili wananchi waendelee kuishi katika hali ya amani na usalama.
Aidha amesema jeshi la polisi kupitia kitengo chake cha “Intelijensia” kitaimarisha utafiti ili kupata taarifa za uhakika za kuweza kukabiliana na wahalifu na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Ameongeza kuwa atatumia uzoefu alionao katika masuala ya teknolojia ya mawasiliano ili kuona kuwa kitengo hicho kinafanya kazi kwa uhakika na kuleta ufanisi uliokusudiwa.
Kamishna Hamdani amesema mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha miaka 30 ndani ya jeshi la polisi, yametokana na mashirikiano aliyopata kutoka kwa viongozi na wananchi, na kuomba mashirikiano zaidi ili aweze kuyafikia matumaini na matarajio ya taifa katika ulinzi wa raia na mali zao.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa pamoja na Kamishna mpya wa jeshi la polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na Kamishna mpya wa jeshi la polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na Kamishna mpya wa jeshi la polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, ofisini kwake Migombani.
Picha na Salmin Said, OMKR).
Post a Comment