Home » » MH. SUMAYE ACHANGISHA MILIONI 225 UJENZI WA UKUMBI, KANISA KATOLIKI MAWELA

MH. SUMAYE ACHANGISHA MILIONI 225 UJENZI WA UKUMBI, KANISA KATOLIKI MAWELA

Written By JAK on Monday, December 30, 2013 | 7:05 AM


Waumini wa kanisa katoriki Parokia ya Maonano, Mawela wakiwa katika ibada.
Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye akitembelea ukumbi wa kisasa unaojngwa katika Parokia hiyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Baadhi ya waumini pamoja na wageni mbalimbali waliojitokeza katika harambee ya ujenzi wa ukumbi wa kisasa katika Parokia ya Maonano Mawela.
Mshereheshaji wa shughuli hiyo ya harambee ya ujenzi wa Ukumbi wa kisasa Godwin Gondwe akijaribu kuweka mambo sawa .
Paroko wa parokia ya Maonano ,Mawela Padre Anthony Marunda akisoma risala kwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ukumbi wa kisasa katika kanisa hilo.
Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye akizungumza katika harambee ya ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa kanisa katoliki Parokia ya Maonano Mawela jana.
Waziri mkuu mstaafu Sumaye pamoja na mshereheshaji wa shughuli hiyo Godwin Gondwe wakijadiliana jambo na mmoja wa wajumbe wa kamati ya harambee ya Ujenzi wa ukumbi huo wa kisasa Anthony Komu.
Waziri mkuu mstaafu Sumaye akimkaribisha Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Dk Cyril Chami kuchangia katika harambee ya Ujenzi wa Ukumbi wa kisasa katika kanisa katoliki Parokia ya Maonano Mawela .

Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii Moshi

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema kuwa mwaka 2014 ni mwaka muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi katika ngazi za serikali za mitaa na ni mwaka wa maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2015, hivyo watanzania wamwombe Mungu awajalie hekima na busara, na kuwapa ujasiri waweze kuchagua viongozi watakaofaa kuongoza kwa hekima, busara, upendo na haki.

Akizungumza na Mamia ya Waumini mbalimbali waliojitokeza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Ukumbi wa Parokia ya Maonano, Mawela katika Jimbo Katoliki la Moshi Sumaye alisema ni ukweli ulio wazi kuwa chaguzi za kitanzania sasa zimegubigwa na rushwa na vishawishi vingi wala siyo ubora, uhodari wala tabia ya anayetaka nafasi ya uongozi.

“Hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha za kuwanunua wapiga kura vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata viongozi wetu wa ngazi zote kuanzia ngazi za vijiji na mitaa hadi ngazi ya Urais, utaratibu huuu ni wa hatari na lazima tuupige vita kwa pamoja” alisema Sumaye.

Aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kuwa wacha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukukia mapato ya udhalimu, hao ndio wanaweza kuwa viongozi kwa kutegemea uwezo wao, upeo wao, uhodari wao, ujasiri wao na uaminifu wao kwa Mungu na kwa jamii wanayoiongoza.

Sumaye alisema pia, Katika utaratibu wa demokrasa sahihi na halisi, wapiga kura hutakiwa kuwachagua viongozi kufutana na sifa nzuri za uongozi alizo nazo, na kuonya kuwa Kiongozi anatafutwa na jamii na siyo yeye kusaka uongozi, mbaya zaidi ni pale msaka uongozi anapotafuta nafasi hiyo kwa njia zisizofaa kama vile rushwa na kununua wapiga kura.

“Uongozi hautafutwi kwa udi na uvumba wala kwa rushwa, leo chaguzi zetu zimegubikwa na rushwa na vishawishi vingi na siyo ubora, uhodari wala tabia ya anayetaka nafasi ya uongozi, rushwa na matumizi makubwa ya fedha kununua wapiga kura vinataka kuwa utaratibu wa kawaida tena halali wa kuwapata viongozi wa ngazi zote kuanzia kijiji hadi Urais, huu ni utaratibu wa hatari na lazima upigwe vita kwa pamoja” aliongeza Sumaye.

Sumaye akinukuu Biblia takatifu (Kut.23:8) inayosema “nawe usipokee rushwa kwani rushwa huwapofusha macho hao wanaonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki” alionya kuwa kama Biblia inasema rushwa inapofusha macho, sisi watanzania tukichagua kiongozi mla rushwa au mtoa rushwa au anayenunua wapiga kura, huyo hawezi kutuongoza tufike tunakotaka, tukichagua kiongozi wa aina hiyo atatumia nafasi yake kujinufaisha yeye na rafiki zake.

Katika hotuba hiyo pia Sumaye alisema watu walioiba wakamatwe na kufungwa maana wametenda jinai, hivyo hivyo waliotoa rushwa au kuifisadi nchi, kuuza madawa ya kulevya au kuua wanatakiwa kutubu kwa kuwa hiyo ni dhambi lakini wakikamatwa waadhibiwe maana hayo yote ni makosa ya jinai,

Katika harambee ya ujenzi wa Ukumbi huo Sumaye alifanikiwa kuchangisha pesa taslimu 55,295,500, na ahadi ya 170,000,000 Jumla ni milioni 225,295,500. Akivuka lengo la harambee hiyo ambayo ilikuwa imepangwa 150,000,000. Gharama halisi za Ukumbi huo wa kisasa wa Parokia ya Mawela ili ukamilike utagharimu 450,000,000/.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger