Home » » Kambi ya urais Kanda ya Ziwa yaingia kiwewe

Kambi ya urais Kanda ya Ziwa yaingia kiwewe

Written By JAK on Friday, January 3, 2014 | 5:33 PM



Source Raia Mwema

ZIARA ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba jijini Mwanza imeishtusha kambi ya mmoja wa mawaziri wakuu wa zamani anayetajwa kuweza kugombea urais, kiasi cha kuanza mikakati ya kudhibiti kile wanachokiita upepo mbaya wa ziara hiyo kwa kambi yao.

Chanzo chetu cha uhakika kutoka ndani ya kambi hiyo kimeeleza kuwa ziara aliyoifanya wakati wa Krismasi kwa mwaliko wa Jilili Gospel Sound na Umoja wa Waendesha Pikipiki Mwanza, kwa ajili ya tamasha la muziki wa Injili na kukutana na wachungaji wa madhehebu ya Kikristo na kuzungumza na waendesha pikipiki hao, imewafanya wafuasi wa kambi ya waziri mkuu huyo wa zamani kupanga mikakati mipya.

Katika kikao chake na wachungaji kilichofanyika katika hoteli moja jijini Mwanza iliyo maeneo ya Capripoint wakati wa ziara hiyo, Makamba alinukuliwa akinukuu mistari ya Biblia kutoka kitabu cha Yeremia kilichokuwa kikimtabiria nabii huyo ufalme kwa wana wa Israel na wengine kuhusisha utabiri huo na harakati zake za urais 2015.



Akizungumza na waendesha pikipiki, ambao pamoja na kuwafanyia mpango kwa kampuni moja ya jijini Dar es Salaam kuweza kukopeshwa pikipiki zaidi ya 1,700, aliwalipia bima za ajali wapanda pikipiki 100 zenye thamani ya shilingi 5,000 kila moja, Januari alisema japo wengine wanawatumia vijana wa boda boda kisiasa, mpango wake huo ulianza zamani kwa dhamira ya kuwasadia na si vinginevyo.

“Baada ya vikao hivyo wameingia mchecheto kuwa kambi yao inaweza kupunguzwa nguvu zaidi, hasa ukizingatia kuna mikakati ya Kanda ya Ziwa kuwa na mgombea wao, ujio huu umewashitua wanahisi wanaweza kuanza kuyumba, na wanaamini hii ni moja ya ngome zao kubwa, wamejipanga kuanza kushambulia na kudhibiti kila hali inayojitokeza kutishia hatma yao,” kilieleza chanzo chetu hicho cha habari.
Mwishoni mwa wiki jana alijitokeza mchungaji mmoja ambaye alidai ni mmoja wa wachungaji waliohudhuria na kushiriki kikao hicho cha wachungaji kilichoitishwa na Makamba, akihoji uhalali na mantiki ya kikao hicho, akikihusisha na mbio za naibu waziri huyo kuwania urais.

Juhudi za Raia Mwema kuonana au hata kuwasiliana na mchungaji huyo hazikuzaa matunda.

“Hizo zilikuwa ni mbinu chafu za kutaka kulinda kambi yao, unajua ilifika wakati kambi ya (anamtaja) wakaamini kwamba hawana tena mpinzani Kanda ya Ziwa, unajua mambo ya ushindi kabla ya mechi sasa ujio huo walihofia mustakabali wa kambi yao. Huyu mchungaji unaweza usimpate kwa sababu anatumika tu kutibua mambo, huu ni wakati wa kuharibiana,” kilieleza chanzo hicho.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa kazi ya kumpata mchungaji huyo ili kuhoji uhalali wa kikao hicho ilikuwa ikisimamiwa na mbunge mmoja wa zamani wa moja ya majimbo ya mkoani Mwanza, ambaye sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) anayetajwa kuwa kiongozi wa kambi ya waziri mkuu huyo wa zamani mkoani Mwanza.

“Huyu Bwana alikuwa na kazi maalumu kuelekea mwisho wa mwaka uliopita, na watakuwa na kikao kikubwa cha kambi yao mwanzoni mwa mwaka mpya, sasa ilikuwa lazima ahakikishe kuwa kanda yake iko salama, ndiyo akaamua kupika hiyo fitna,” alieleza mmoja wa wajumbe wa NEC wa moja ya wilaya mkoani hapa ambaye pia amealikwa kushirki kikao hicho.

Juhudi za kumpata mbunge huyo wa zamani hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa kijijini kwa mapumziko ya Krismasi na simu zake kutopokelwa.

Askofu Seleman Kilinga wa Kanisa la Goshen (nyumba ya makimbilio) liliko Mabatini jijini Mwanza ambaye pia alihudhuria hafla iliyoandaliwa na Makamba alisema hamjui mchungaji huyo aliyekitokeza na kushusha shutuma za kuwalaumu wachungaji wenzake kudhuria shughuli hiyo na kwamba amekuwa akisikia tu tetesi kuhusu kuwepo kwa tamko hilo.

Alipoulizwa ni kwa nini kama viongozi wa dini walihudhuria shughuli hiyo iliyokuwa ikihusishwa na siasa na kama haoni hilo litawashushia heshima alisema kuhudhuria kwao katika kikao hicho hakukuwa na uhusiano wowote na suala la kuwania urais.

“Tuliwahoji pia juu ya mabango tuliyoona yanachapishwa kuhusu Makamba, tukauliza na haya yamo kwenye ziara hii hii, wakasema hawayajui, tukawaambia yapo lakini tusiyaone,” aliongeza.

Anaeleza kuwa kwa upande wake alikubali kuhudhuria kikao hicho baada ya kuona dhamira ya waandaaji ni njema.

Mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza (jina linahifadhiwa kama alivyotaka) akizungumzia mvutano na kuhujumiana huko alisema; “Unajua yako mambo yanashangaza sana, wao ndiyo mabingwa wa kupita kwenye nyumba za Ibada na kutafuta kuungwa mkono tena hadharani, lakini huyu (Januari Makamba) kaja mara moja tu imeshakuwa tatizo.”
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger