Home » » Kwa nini Mangu IGP mpya?

Kwa nini Mangu IGP mpya?

Written By JAK on Friday, January 3, 2014 | 5:51 PM


Kamishina wa Polisi (IGP), Ernest Mangu

Source Raia Mwema - Ezekiel Kamwaga

UTEUZI wa Kamishina wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuwa Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi (IGP) umetokana na sababu kubwa tano, Raia Mwema limeelezwa.

Katika mahojiano ambayo gazeti hili limefanya na watu mbalimbali walio karibu na Mangu pamoja na mamlaka zinazohusika na uteuzi wake tangu alipotangazwa juzi, sababu kubwa tano zimekuwa zikijirudia.

Mangu ambaye alitangazwa na Ikulu Jumatatu jioni wiki hii kuwa IGP mpya akichukua nafasi ya Said Mwema, alikuwa mara zote akipewa nafasi ya pili kuchukua nafasi hiyo-akiwa nyuma ya Mkuu wa Utawala wa Polisi, Kamishina Thobias Andengenye.

“Sababu ya kwanza ambayo imetolewa na watu waliozungumza na gazeti hili ni Utamaduni. Gazeti hili limeelezwa kwamba upo utamaduni uliojijenga kwenye jeshi hilo kwamba wakuu wake wote wamepitia katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP).

“Miongoni mwa watu waliokuwa wakitajwa kupata nafasi hiyo akiwamo Andengenye, wote hawakuwa wamepitia CCP. Kwenye rank and file (askari wa kawaida), ina maana kubwa kama askari amepitia CCP.

“Maana yake ni kwamba Mangu anajua taabu za askari wa ngazi za chini. Anajua mahitaji yao na analifahamu jeshi kuanzia juu mpaka chini.

“Ni tofauti na askari kama Andengenye ambao wao wameanzia kwenye uofisa moja kwa moja. Hivyo kitamaduni, Mangu alikuwa na maksi nyingi,” kilieleza chanzo hicho ambacho ni mmoja wa maofisa wastaafu wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi.

Suala la pili lililomfanya Mangu apate alama nyingi kwenye kupata wadhifa wake huo ni namna anavyofahamika kwa usimamizi wake wa Kanuni za Polisi (Police General Order, PGO).

Akiwa kama Kamanda wa Polisi katika mikoa mbalimbali hapa nchini, Mangu ametajwa kama mtu aliyekuwa akisimamia vizuri zaidi utekelezaji wa PGO ambayo maana yake haswa ni usimamizi wa maadili ya uaskari.

“Katika kizazi cha sasa, maadili ya uaskari yameshuka. Mangu ndiye pekee anayeonekana ana uwezo wa kuhakikisha nidhamu na maadili ya Polisi yanarejea kwa vile amepigania hili kwa muda mrefu kabla hata hajawa IGP,” kilieleza chanzo kingine cha gazeti hili.

Sifa nyingine ya Mangu imetajwa kuwa ni kufanya kazi kwake kama kachero wa polisi kwa muda mrefu, taaluma inayodaiwa kuwa muhimu kwa IGP.

Mwema anaelezwa kupanda chati katika miaka ya nyuma akiwa kachero ndani ya jeshi hilo na wapo wanaodai kwamba IGP bora kuwahi kutokea nchini, Haruni Mahundi, alifanikiwa kwa sababu ya ukachero wake na namna alivyowaamini makachero.

Raia Mwema limeambiwa kwamba kwa sasa, kachero mwenye uwezo mkubwa zaidi ndani ya Jeshi la Polisi kwa sasa ni Hussein Laizer aliye katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID) lakini kutokana na matatizo ya kiafya aliyonayo hawezi kupewa cheo cha IGP wala DCI na kwamba ukiondoa huyo hakuna mwenye sifa zaidi ya Mangu.

“Unajua Mangu ni kachero na makachero wanafanya kazi zao vizuri sana kwa sababu wanachunguza kila kitu kabla ya kuamua. IGP Omar Mahita hakufanya vizuri sana kwa sababu yeye historia yake ilikuwa ni Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), sasa hata maamuzi yake yalikuwa ya hivyo,” gazeti hili limeambiwa.

Sababu ya nne imeelezwa ni ukweli kwamba kama Andengenye angeteuliwa kushika wadhifa huo, maana yake ni kwamba Mkoa wa Mbeya ungekuwa na watu wawili katika ngazi za juu za vyombo vya dola.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, anatoka katika Mkoa wa Mbeya na mamlaka za uteuzi ziliona haingekuwa vema kwa mkoa mmoja (kabila moja?) kutoa viongozi wawili wa majeshi hapa nchini.

Sababu ya mwisho inayodaiwa kumpa Mangu nafasi kulinganisha na washindani wake imeelezwa kuwa ni tabia ya Rais Jakaya Kikwete kutopenda kuvuja kwa siri kuhusu uteuzi wake.

Taarifa za Andengenye kuwa IGP zilianza kuvuja mwezi uliopita na kwa kawaida, Kikwete au mfumo wa utawala haupendi kuvuja kwa taarifa.

Itakumbukwa kwamba miaka ya nyuma, kuna kamanda alifanya sherehe kabisa baada ya kuarifiwa mapema kwamba atakuwa IGP. Taarifa zilipofuja tu, Ikulu ikabadili uamuzi na akachaguliwa Mahita wakati huo.

“Kuna taarifa tumesikia kwamba kuna watu waliwahi kupewa taarifa na Ikulu kuhusu kupewa kwao nafasi na taarifa zilivyovuja tu Kikwete akabadili uamuzi. Kwa ufupi, ukitaka Kikwete abadili uamuzi au kumharibia mtu, vujisha jina lake kabla ya kutangazwa,” kilisema chanzo cha gazeti kilicho ndani ya Ikulu.

Uteuzi wa Mangu unamfanya kuwa IGP wa tisa katika historia ya Tanzania. Waliomtangulia ni Elengwa Shaidi, Hamza Aziz, Samson Pundugu, Philemon Mgaya, Solomon Liani, Harun Mahundi, Omar Mahita na Saidi Mwema.

Wasifu wa IGP Mangu

IGP Ernest Jumbe Mangu alizaliwa mwaka 1959 mkoani Singida na alipata elimu ya Sekondari katika Shule ya Tumaini mwaka 1981.

Alijiunga na Jeshi la Polisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP) Agosti 17 mwaka 1982 na kuhitimu Juni, mwaka 1983 ambapo alipata mafunzo ya awali ya Polisi.

Mwaka 1987 alipata mafunzo ya sheria kwa ngazi ya cheti katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Novemba mwaka 1992 alitunukiwa shahada ya kwanza ya sheria (LLB) katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Juni mwaka 2010, alitunukiwa shahada ya udhamili katika masuala ya usalama katika Chuo Kikuu Cha Usalama cha Marekani.

Akiwa ndani ya Jeshi la Polisi amepandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo Koplo wa Polisi (1988), Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1992), Mkaguzi wa Polisi (1995), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (1997), Mrakibu wa Polisi (2002), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (2004), Kamishna Msaidizi wa Polisi (2006), Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi (2010), Naibu Kamishna wa Polisi (2013) na Kamishna wa Polisi (2013).

Amewahi kufanya kazi Dar es Salaam katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OCCID) na pia Naibu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza mwaka 1996 akimsaidia Aliyekua RCO wakati huo, Said Mwema. Pia amefanya kazi Dodoma.

Alipoteuliwa kuwa IGP Saidi Mwema alifanya kazi kwa karibu na Mangu akiwa mmoja wa wasaidizi wake muhimu makao mkuu ya Polisi kabla ya hupewa majukumu ya kiuongozi.

Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger